NJOMBE

NJOMBE

Friday, January 20, 2012

Dina Marius, mrithi wa Amina Chifupa

 Nilikwenda kuzungumza naye Alhamisi mchana nikatambua changamoto niliyoipata muda mfupi kabla ya kuondoka ofisini Mtaa wa Samora, Dar es Salaam, na endapo nisingekuwa na msimamo katika kile ninachokiamini huenda nisingekwenda huko hivyo asingekuwa nyota wetu leo. Nilimtafuta kwa sababu naamini wanawake wengi wanasikiliza kipindi anachokiongoza, Leo Tena, kinachorushwa Clouds FM Jumatatu hadi Ijumaa saa tatu hadi saa saba mchana, na nilizungumza naye kwa saa mbili nikitambua kuwa baadhi ya watu wana mtazamo hasi kuhusu yeye kwa fikra kwamba Dina Marius, ni mbea, na shangingi.

Wakati nakwenda katika ofisi za kampuni ya Clouds Entertainment, ghorofa ya saba katika jengo la Kitega Uchumi, Dar es Salaam nilizingatia zaidi uwezo wake kutangaza kuliko maisha yake binafsi, na nina imani kwamba aliyosimulia msichana huyo mwenye umri wa miaka 25 yanaweza kuwa darasa kwa wengine. Kwa wanaosikiliza kipindi hicho bila shaka mara nyingi wamekuwa wakimsikia akisema ‘ Mimi naitwa Dina Marius wa ukweli zaidi’, wakati mwingine hupenda kusema ‘ Ni leo tena ya Clouds FM, naitwa Dina Marius’ au kibwagizo kisemacho ‘ Dina Marius leo tena’.

Sauti yake ilianza kusikika katika kipindi hicho Februari 26, 2006, akibeba mikoba ya Amina Chifupa, aliyekuwa na majukumu mengine katika Bunge la Jamhuri ya Muungano akiwa Mbunge wa Viti Maalumu. Ni kipindi chenye vionjo vya mambo ya kijamii yanayotokea katika maisha ya kila siku vikiwamo vya Nyumbani Kwetu Leo, Chachandu la Leo, Kiburudisho Chako Leo, Heka Heka za Leo, ‘Kitchen Party’ na ‘Movie’ Leo, wengi wa wanaokisikiliza ni wanawake.

Anasema kufanya kipindi kinachowalenga hasa wanawake ni ‘mtihani’ kwa kuwa amekuwa akitumiwa ujumbe mfupi wa matusi, na wengine wanampigia simu kumtukana kwa sababu wanazozifahamu wao. “Unajua kufanya kipindi ukawalenga wanawake ni kazi, wanawake kama wanawake kuna ambao watakufurahia, kuna wengine mmh,” anasema Dina na kueleza kwamba utangazaji ndiyo maisha yake, hivyo anailinda hadhi yake.

“’Nimefocus’ (nimelenga) kwenye kazi yangu halafu ‘at the end of the day’ (mwisho wa siku) ukifanya kazi kwenye media (chombo cha habari) unakuwa kioo cha jamii,” anasema na kubainisha kwamba, “inabidi ulinde ‘image’ (muonekano) yako kwa msikilizaji. Ukishakuwa mtangazaji huna tofauti na msanii, uwe wa radio au wa TV, huna tofauti na msanii anayeimba muziki. “Saa nyingine kuwa mtangazaji pia ni kujinyima uhuru, inabidi ujinyime ili kulinda maslahi yako,” anasema.

“Kwa hiyo kwa sasa hivi nafanya ‘kui-brand image’ yangu,” anasema Dina na kuongeza kwamba kuna watangazaji ambao si kioo cha jamii. “Mimi nikiwa hewani namfikiria anayenisikiliza, nikitoka pale nakuwa na maisha yangu ya kawaida,” anasema na kujigamba kwamba wanawake wengi wanasilikiza ‘Leo Tena’ kwa kuwa wanajitahidi kubuni vitu vinavyowavutia ikiwa ni pamoja na kuweka wimbo wa taarabu na wao kuweka vionjo studio.

“Tukitoka pale maisha yanakuwa ya kawaida, maisha yetu ya kawaida yasiyokuwa na mipasho… mimi naishi kivyangu vyangu, mtaani sina mashoga, sina mashosti…mimi maisha yangu ya kawaida, sina magroup (makundi),” anasema na anaamini kwamba ubunifu wa Chifupa ndiyo umefanya nyimbo za taarabu zipendwe katika vituo vya radio na kwamba hadi leo radio nyingi zinaiga ‘style’ ya mtangazaji huyo. “Unavyoizungumzia Chachandu (moja ya vipengele kwenye kipindi cha Leo Tena), unazungumzia wimbo mmoja lakini ‘impact’ yake ni kubwa,” anasema na kueleza kuwa, nyimbo nyingi za mahadhi hayo huchukua dakika 16 hadi 20 lakini wao wamebuni namna ya kufanya usichoshe.

Ingawa alikuwa hafuatilii utangazaji wa Chifupa wanaosema kuwa Dina ni mrithi wake Clouds FM hawakosei kwa kuwa ndiye aliyepewa jukumu la kuongoza kipindi hicho alichokuwa akikiongoza msichana mwenzake ambaye sasa ni marehemu, lakini hafahamu ni kwa nini anafananishwa na mwanasiasa huyo. “I used to like Phina (Phina Mango, ambaye aliwahi kuwa mtangazaji katika kituo hicho cha redio)...sauti yake,” anasema msichana huyo asiyevutiwa na vipindi vya televisheni za Tanzania, na anakunwa zaidi na vipindi vya mahojiano vya Oprah Winfrey.

Anasema hafahamu amefanana nini na Chifupa, labda sauti, na wengine wanasema sura, ila anachofahamu yeye katika utangazaji, mtangulizi wake alikuwa juu hivyo katika hilo si sahihi kuwalinganisha kwa kuwa hawalingani. “Mtu mwingine anaweza akaangalia picha akaona kama Amina, ni akili ya watu,” anasema mtangazaji huyo aliyewahi kuwa na ndoto za kuwa daktari.

Msichana huyo anayeishi Kawe, Dar es Salaam anasema, kuendesha kipindi cha Leo Tena, ilikuwa ni changamoto kubwa kwake lakini imemsaidia kuongeza upeo wa kuelewa mambo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania. “Amina ‘was big’, mimi nilivyoanza kipindi unajua ‘it was so hard’ (ilikuwa kazi ngumu),” anasema na kubainisha kuwa, mlengwa wa kipindi hicho wakati kikiendeshwa na Chifupa ni yuleyule wa sasa ila baadhi ya yanayozungumzwa humo yamebadilika.

Anasema hatarajii kufanya kazi ya kutangaza kwa muda mrefu, ila anaweza kubadili aina ya utangazaji, na hata akiondoka yeye Clouds FM jina la kipindi anachokiongoza halitabadilika. “Entertainment Industry’ inafika kipindi unakuwa ‘out’” anasema msichana huyo mwenye kipaji cha kuchora. Alishiriki mashindano ya uchoraji wakati akisoma katika Shule ya Sekondari Shauritanga mkoani Kilimanjaro.

“Nachora kadi kwa ‘manila paper’, naipaka rangi na ninaitengeneza namna ambayo mtu anaweza kuandika , nilikuwa mpaka nauza,” anasema msichana huyo aliyekuwa akicheza ngoma za utamaduni wakati akisoma Shule ya Msingi Ushindi iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam na Lyalamo ya Iringa. “Kwa sababu radio pia ina mipaka ya umri, ina mlengwa wake…lakini ‘plan’ yangu kubwa ni kuwa na vipindi kama vile vya kina Tyra, au Oprah,” amesema mtangazaji huyo anayeshirikiana na Gea Habib, Zamaradi Mketema, na Antonio Nugas kuendesha kipindi cha Leo Tena.

“Kwa hiyo naona ‘talk show’ ni nzuri lakini inategemea huko mbele upande wa Tanzania inakuwaje,” anasema msichana huyo anayeamini kwamba nyota ya mtu haiji tu, lazima uzungumze na watu mbalimbali, usome au kutazama vitu mbalimbali kuongeza ufahamu wako na kwamba, ingawa kipindi anachokiongoza kinakwisha saa saba, huenda nyumbani kati ya saa 11 hadi saa moja usiku.

“Kama sasa hivi nikitoka lazima nihakikishe kesho nikija kusikosekane kitu… kwa hiyo hata ‘system’ yangu ya maisha imebadilika,” anasema na kubainisha kwamba changamoto kubwa kwake ni kuhakikisha kuwa anachokisema radioni kiwe na matokeo hasi au chanya kwa anayesikiliza. Anaamini anafanya kile alichozaliwa kukifanya na ndiyo maana alikuwa na ndoto nyingi lakini sasa hazipo.

“Yaani iwe na ‘impact’ kwake (msikilizaji), kama alikuwa hajui ajue, kama cha kufurahisha acheke, hiyo ndiyo changamoto niliyonayo, kila nikimaliza kipindi nakaa na timu yangu,” anasema na kuongeza kuwa changamoto nyingine ni kuhakikisha kuwa watu wanasikiliza na amedai kuwa uwezo wa mwanadamu kusikiliza kitu hicho hicho ni dakika nne hivyo lazima umshawishi aendelee kusikiliza na ndiyo maana ‘Leo Tena’ ina vipengele vingi.

Mtangazaji huyo anayependa kula ndizi nyama, ugali dagaa na matembele, pilau kuku, firigisi na ugali hajawahi kujuta kutotimiza ndoto zake na anaamini kuwa si watu wote wanafanya kazi walizopangiwa kufanya wakati wanazaliwa kwa kuwa wakati mwingine unalazimika kufanya kazi kutokana na mazingira ya wakati huo.

“Unajua ndoto zinabadilika kadri mtu anavyokua, mimi nia yangu niliyokuwanayo ni kuwa daktari hivi,” anasema msichana huyo aliyekuwa akipenda masomo ya Kiingereza, Historia, Kiswahili, Siasa, na Elimu ya Viumbe wakati akisoma kidato cha kwanza hadi cha nne na alikuwa na uwezo mkubwa wa kujieleza kulinganisha na wenzake darasani kwao katika Shule ya Shauritanga.

“Mimi kiukweli mpaka namaliza ‘form six’ sikuwahi kufikiria kama nitakuwa mtangazaji,” anasema msichana huyo aliyehitimu ngazi hiyo ya elimu mwaka 2005 mchepuo wa masomo ya Historia, Kiswahili, na Fasihi (HKL). Msichana huyo aliyehitimu darasa la saba mwaka 1998, hajabadilika ndoto tu, waliokuwa wakimfahamu miaka ya nyuma wakiomwona leo watamshangaa, amekuwa mnene na anahitaji kupungua. “Ila chakula kingine ambacho kinaniponza ni chips, kila siku mchana ninakula chips kwa nini nisinenepe?,” anasema mtangazaji.

“Mimi kabla sijawa hivi nilivyo nilikuwa mrefu, mwembamba, mweusi, ‘brown colour’ sijui ndiyo ‘chocolate colour’ wanaita,” anasema msichana huyo aliyebainisha kwamba katika familia yao hakuna mtu mwenye kipaji kama chake. Si shabiki wa michezo, ni msanii, licha ya kipaji cha kuchora, ni mbunifu wa vitu vya kisanii, baada ya kuhitimu kidato cha sita alipanga kuendeleza kipaji hicho, akawa anakwenda katika Nyumba ya Sanaa, Dar es Salaam kujifunza kubuni na kufuma nguo, shanga na hereni.

Kama asingekuwa anafahamiana na, Fidesia Mwakitalema (mtangazaji mwingine wa kituo hicho), pengine asingekuwa alivyo leo, mazoea ya kwenda ofisi za Clouds kumsalimia rafiki yake ndiyo chanzo cha kufanya kazi anayofanya leo, na wakati huo alikuwa hajafikiria kuwa mtangazaji. Siku moja alipokwenda katika ofisi hizo mwaka 2005 alikutana na kijana, Daudi Gladis, wakati wanaongea akamwambia kuwa ana sauti nzuri na endapo angekubali ushauri huo angemtafutia nafasi ‘Radio Times’ ya Dar es Salaam, alikubali, wakaondoka Kitega Uchumi wakaenda mtaa wa Lugoda wakamkuta,Taji Liundi, akampa nafasi ya kufanya mazoezi.

Baada ya muda fulani wa mazoezi alielezwa asiende hadi atakapoitwa, wakati anasubiri majibu babu yake mzaa mama alifariki dunia akaenda Arusha msibani, akakutana na Meneja wa Radio Triple A, Bashir Mohamed, kwanza alimpata nafasi ya kuendesha kipindi cha ‘Lunch time’, baadaye alikiacha, akaendesha vipindi vya Makala ya Leo, na Taarab. Wakati akiwa Arusha, Meneja wa Clouds FM Arusha, Charles Mhamiji, alimweleza kuwa anahitajika Dar es Salaam akachukue mikoba ya Amina Chifupa kuendesha kipindi cha Leo Tena, ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuwa alivyo leo.

“Sasa hivi nakuwa, najifunza, hata upeo wangu unaongezeka,” anasema na kubainisha kwamba majukumu yake yanamlazimu ajifunze mambo mengi na kwa kuwa baadhi ya wanaomsikiliza wamemzidi umri, inambidi atafute vitu vinavyolingana na umri wao. “Kipindi changu mimi siongei siasa, naongea mambo yaliyopo ndani ya jamii, ‘social issues’ (masuala ya kijamii),” anasema na kuongeza kwamba “‘for my age’ (kwa umri wangu) nimekuwa nikijikuta naongea na watu wazima zaidi yangu.”

Ni mtoto wa pili wa, Peter Marius na Rehema Shaaban Mushi, hafahamu kama asingekuwa mtangazaji leo angekuwa anafanya kazi gani, ila anakumbuka kwamba aliwahi pia kuwa na ndoto za kuwa mwanasheria, zikafutika baada kuhitimu kidato cha sita katika Shule ya Mkwawa, Iringa. Ana kaka watatu, John, Ibrahim, na Marius, mama yao mzazi alifariki dunia wakati Dina akiwa na umri wa miaka mitano, baba yake alioa tena, mama aliyemlea.

Anasema licha ya maendeleo kiasi aliyonayo, safari yake ya mafanikio ndiyo kwanza inaanza, hajafika anapotaka kufika kikazi na kimaisha. Hajaolewa, hana mtoto, anapenda kupata watoto wawili, kapanga azae wa kwanza muda si mrefu ujao ila hajui ataolewa lini, na nani atamwoa. “Ndoa naifikiria lakini mimi sio kama vijana wengine wanaharakisha kuolewa ili mradi tu kuolewa.”

“Unajua sio wanaume wote ni wabaya, kuna wanaume wasikivu, wapole, lakini bahati mbaya wanaangukia kwa wanawake ambao sio,” anasema na kudai kuwa si wanawake wote wana sifa za kuwa mama au mke na amedai kuwa yeye atakuwa mke na mama mzuri na hataki kuzaa mapema kwa kuwa anaandaa maisha ya watoto wake kwanza. “Nitaolewa na mwanamume ambaye anafaa kuwa mume wangu mimi, na ambaye anafaa kuwa baba wa watoto wangu mimi,” anasema na kudai kuwa si wanaume wote wanafaa kuwa mume au baba wa watoto na akasema “ni wanaume tu lakini sio ‘father material’”.

Anasema si lazima aolewe na ikiwa hivyo huenda wengi hawatajua, ila akitimiza dhamira yake, atamwomba padre akafungishe ndoa hiyo studio wakati akiwa katika kipindi cha Leo Tena. Akipata nafasi anapenda kutazama sinema kwa kuwa anajifunza mambo mengi yanayomsaidia kwenye kazi zake. Anapenda kusikiliza nyimbo za Kizungu hasa R&B, za dansi, za Kongo DRC hasa za Koffie Olomide.

“Taarab napenda kama kupenda lakini kuna miziki mingine ambayo napenda kuliko taarab,” anasema na kuwatuhumu baadhi ya waandishi wa habari na wapiga picha kuwa wanatumia kalamu na kamera zao vibaya. Anawashukuru Mkurugenzi wa Kampuni ya Clouds Entertainment, Ruge Mutahaba, Muhamiji, Meneja wa vipindi Clouds, Sebastian Maganga, Meneja Ubunifu katika radio hiyo, Ruben Ndege, Daudi Gladis, na wafanyakazi wenzake kwa kumwezesha kufika alipo leo.

No comments:

Post a Comment