NJOMBE

NJOMBE

clock

Saturday, January 28, 2012

Pinda alikoroga posho za wabunge

WANANCHI, wanasiasa na wanaharakati wamemjia juu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu kauli yake ya kuhalalisha nyongeza ya posho za wabunge.
Wakizungumza na mwanahabari wetu, jana jijini Dar es Salaam walisema kiongozi huyo ameonyesha namna viongozi walivyoweka mbele maslahi binafsi hasa linapofika suala la fedha.
Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari juzi, Pinda alitetea posho za wabunge akisema kiasi wanachokipata ni kidogo na wengi wao mwisho wa mwezi hawabaki na kitu, kwani fedha zote za mishahara hukatwa kulipia madeni waliyoingia kwa ajili ya kusaidia majimbo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema Pinda atakuwa Waziri Mkuu wa kwanza kuwapotosha Watanzania kuhusu posho.
Alisema posho wanayopewa wabunge ni kwa ajili ya matumizi yao na si kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.
“Nimekuwa mbunge kwa miaka 15 sijawahi kutoa fedha mfukoni mwangu kwa ajili ya kumhudumia Mtanzania mmojammoja kama nitatoa ni kwa hiyari yangu.
“Si kweli kwamba mbunge anaishiwa fedha zake zote kwa ajili ya kumhudumia Mtanzania, kwani Watanzania wanao mfuko wao wa maendeleo ambao wabunge hukaa na wananchi kujadili fedha hizo zitumikaje,” alisema Dk. Slaa.
Kwa mujibu wa Slaa, Pinda alipaswa kuzungumza juu ya ugumu wa maisha ya Watanzania yalivyo sasa na namna ya kuwasaidia na si kuzungumzia wabunge peke yao kwa kuwa wao hawana shinda kama ilivyo kwa Mtanzania wa kawaida.
Akitolea mfano, alisema Pinda alipaswa kuangalia makundi yanayolalamika kuhusu malipo yao kama ilivyo kwa madaktari hivi sasa, kuliko kuchukua jukumu la kuwapotosha Watanzania.
“Kila siku ninasema serikali ya CCM imeshindwa kutafuta njia sahihi ya kupunguza ugumu wa maisha kwa Watanzania badala yake inatumia ujanja ujanja kuonyesha kwamba inashughulikia matatizo yao wakati si kweli,” alisema.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Mbarara Maharagande, alisema suala la nyongeza za posho za wabunge si la kuzungumza kwa wakati huu ambapo maisha ya Watanzania yamegubikwa na mfumko wa kutisha wa bei na kupanda kwa gharama za maisha.
Alisema CUF wanahitaji mfumo wa kisiasa ambao utazaa mfumo mzuri wa kiuchumi utakaowatoa Watanzania kwenye maisha magumu.
Alisema posho ya sh 200,000 kwa siku inayotolewa kwa wabunge 328 ni sawa na sh mil. 65.6 ambazo serikali hutoa kwa siku.
Maharagande alisema fedha hizo ni nyingi na kama zingetumika ipasavyo zingeweza kufanya jambo kubwa la maendeleo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Kijinsia (TGNP) Usu Marya alishangaa serikali na wabunge kushindwa kutambua wajibu wao.
“Sisi kama wanaharakati tunaona kuna tatizo la msingi la dhana nzima ya uwajibikaji, serikali inashindwa kutambua majukumu yake na Bunge pia,” alisema.
Alisema mbunge hapaswi kutoa fedha zake mfukoni kwa ajili ya kusaidia jimbo inayopaswa kufanya hivyo ni serikali na wabunge kazi yao ni kusimamia wajibu huo wa serikali.
“Si kazi ya wabunge kutoa fedha mfukoni kusaidia watu, serikali inapewa dhamana ya kusaidia watu kwa kutoa huduma kwa wananchi kutokana na kodi inazozikusanya…sisi wanaharakati tunaipinga; inakwenda kinyume kabisa, inakuwa kama wabunge wanaihonga serikali.
Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe aliyebobea katika masuala ya uchumi, Prosper Ngowi, amesema Pinda anatakiwa kuelewa kuwa maisha magumu si kwa wabunge peke yake bali ni kwa Watanzania wote.
Alisema alichotakiwa kuzungumza Pinda katika hotuba yake ni kueleza namna serikali itakavyoweza kuwapunguzia ugumu wa maisha Watanzania.
Aliongeza maisha yaliyopanda si katika mkoa wa Dodoma kama wanavyodai wabunge bali ni nchi nzima na hasa watu wenye vipato vya chini.
Mkazi wa mkoa wa Kagera, Yohana Kazimoto, ambaye alipiga simu chumba cha habari cha Tanzania Daima, alisema viongozi wengi wamesahau kutetea maslahi ya wananchi badala yake wanaangalia yanayowahusu.
Naye mkazi wa Yombo Vituka jijini Dar es salaam, Ester Barimi, alisema kama viongozi wa serikali wameamua kujilimbikizia posho, wafanye hivyo pia katika sekta nyingine zikiwemo za afya, elimu na kilimo

No comments:

Post a Comment