NJOMBE

NJOMBE

Friday, March 9, 2012

Funza Makete bado ni tatizo sugu

              Kijana huyu ambaye jina lake limehifadhiwa alionyesha namna funza wanavyoshambulia
 
HALMASHAURI ya wilaya ya Makete mkoani Iringa, inakusudia kuendelea kujenga vyoo vya kisasa katika shule za msingi za Ipepo na Kijyombo ziliko tarafa ya Lupila ikiwa ni moja ya harakati za kutokomeza wadudu aina ya funza ambao wameonekana kuathiri watoto na watu wazima.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu kutoka Makete, Ofisa Afya wa Wilaya, Boniface Sanga, alisema kutokana na wadadu aina hiyo kuathiri kwa kiasi kikubwa wakazi wa vijiji hivyo, halmashauri imeamua kujenga vyoo vya kisasa kwa msaada wa Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef) na Tasaf.
Unicef ndiyo inafadhili mradi wa ujenzi wa choo cha Ukange na sasa itafadhili pia mradi wa choo chenye matundu 10 katika Shule ya Msingi Kijyombo.
Sanga alisema viroboto wanaosababisha funza wanapatikana sehemu zenye vumbi nyingi na udongo unaonatanata, hivyo kutokana na hali hiyo wameamua kuanzia sehemu ambayo imekuwa rahisi na kuna mkusanyiko wa watoto.
Alisema kuwa mpango huo wa kudhibiti wadudu hao ulianzia katika kijiji cha Ukange ambako halmashauri ya wilaya kwa kusaidiana na Unicef mwaka 2009 walijenga choo chenye matundu 16 pamoja na kununua matanki manne ya lita 5000 kwa ajili kuhifadhia maji ya kunawa suala ambalo linaonekana kuafikiwa kwa kiasi kikubwa.
Alibainisha kuwa Tasaf imefadhili ujenzi wa choo katika Shule ya Msingi Kijyombo ambacho kitakuwa na matundu 10 na kuweka matanki ya kuvunia maji ya mvua.
Halmashauri ya Makete ni miongoni mwa wilaya zilizoathirika na funza hasa katika vijiji vya Kijyombo, Ukange, Ipepo, Malanduku, Igolwa na Lupila katika tarafa ya Lupila.
 Habari zaidi na Mtanzania daima

No comments:

Post a Comment