NJOMBE

NJOMBE

Wednesday, March 14, 2012

Profesa Lipumba: Hatujuti kuwafukuza kina Hamad

MWENYEKITI wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema chama hicho hakijutii kumfukuza kwenye chama hicho Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed na washirika wake kwa kuwa ni waasi na uamuzi huo umefanywa kulinda nidhamu ndani ya chama.
Uamuzi wa kuwavua uanachama Hamad Rashid na wajumbe wenzake watatu wa Baraza Kuu la CUF, Doyo Hamis Doyo, Juma Saanani na Shoka Khamis Juma, umekuwa ukitajwa kama sababu ya kuanza kuanguka kwa himaya ya kisiasa ya chama hicho kwa upande wa bara.
Lakini, jana, Profesa Lipumba akizungumzia mwelekeo wa chama hicho alipokutana na waandishi wa habari Dar es Salaam, alisema CUF ni chama imara hivyo lazima kifanye uamuzi kwa kufuata vikao na katiba yake.
“Uamuzi wa kuwafukuza uanachama hatuujutii, ulifanywa kwa umakini kwa kufuata taratibu za kufanya uamuzi kwa njia ya vikao na katiba. Nikiwa Marekani nilikuwa nawasiliana na viongozi wenzangu na uamuzi waliofikia ulikuwa na lengo la kukiimarisha chama,” alisema Profesa Lipumba.
Kuhusu wanachama kukihama chama hicho baada ya kuwafukuza kina Hamad, Profesa Lipumba alisema: “Watu wanaweza kuchapisha kadi nyingi na kusema ni za wanachama waliohama kumbe si kweli. Hatuwezi kuchapisha kadi kama zilivyo noti kwa kuwahofia wahalifu wanaozichapisha, jambo la msingi ni kuwafahamu wanachama wetu.”
“Kuna utata katika takwimu za watu wanaokihama chama, maeneo mengine idadi ya wanachama wanaohama inaelezwa kuwa ni kubwa kuliko idadi wanachama tuliowahi kuwa nao. Hizi ni mbinu zinazotumiwa kuonyesha kwamba chama kinaelekea kufa lakini, ukweli ni kwamba kipo imara na kitaendelea kuwepo.”
Jana Hamad Rashid hakupatikana kutwa nzima kujibu tuhuma hizo. Lakini aliwahi kukaririwa akieleza kuwa uamuzi kumfukuza uanachama ulifanyika kwa mizengwe na chuki.
Alithibitisha madai yake hayo kwa kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo na kuiomba Mahakama imtake Katibu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad na Baraza la Wadhamini la chama hicho kueleza kwa nini wasichukuliwe hatua kwa kukiuka amri iliyozuia mkutano wa kumfukuza.
Barua pepe
Akijibu tuhuma za Hamad Rashid kwamba aliwahi kunasa waraka wa barua pepe unaoonyesha mawasiliano kati yake na Maalim Seif, Profesa Lipumba alisema kitendo cha kuanika hadharani mawasiliano binafsi ni kosa la jinai... “Hili ni kosa la jinai mtu anatamba hadharani akionyesha mawasiliano ya barua pepe za watu kinyume na taratibu!”
Mwishoni mwa mwaka jana, Hamad Rashid wakati akiwa katika mvutano na uongozi wa juu wa chama chake, alitoa nakala kwa waandishi ukionyesha kile alichodai kuwa ni waraka wa mawasiliano ya barua pepe kati ya Profesa Lipumba na Maalim Seif ukitaja mbinu za kumng’oa katika CUF.
Azungumzia uchumi
Katika mkutano huo, Profesa Lipumba ambaye ni mchumi aliyebobea, pia alizungumzia hali ya uchumi nchini na kusema chama chake kinafanya uchambuzi na hivi karibuni kitakuja na mkakati kuitaka Serikali kuwafungulia akaunti wananchi na kuwaingizia fedha zinazotokana na rasilimali za taifa.
“Tunaamini kwamba wananchi wakiingiziwa mgawo wa fedha kwenye akaunti zao na kukatwa kodi itakuwa rahisi kufuatilia matumizi ya fedha yanayofanywa na Serikali. Watu wakikatwa kodi watakuwa na uchungu na hizo fedha, watafanya kila njia kuhakikisha kwamba zinatumika vizuri kwa ajili ya maendeleo.”
Profesa Lipumba alisema ili hayo yafanyike, ni lazima nchi iwe na utawala bora wenye kusimamia kikamilifu rasilimali za taifa.
Akizungumzia kilimo, alisema asilimia 80 ya watu wanategemea sekta hiyo lakini bado hakijamsaidia Mtanzania... “Tanzania ina ardhi kubwa, lakini wananchi wanategemea chakula cha aina moja hali ambayo inawafanya wengi wao kuugua utapiamlo.”
Profesa Lipumba alisema suala la kuendeleza kilimo lina umuhimu mkubwa kwa sababu ni eneo linaloweza kutoa ajira kwa wananchi hasa vijana.

No comments:

Post a Comment