NJOMBE

NJOMBE

clock

Thursday, March 15, 2012

Operesheni ya Magufuli Safisha jiji yatikisa Dar


Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli
OPERESHENI  ya kusafisha jiji la Dar es iliyotangazwa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli imeshika kasi baada ya tingatinga kubomoa vibanda vya biashara kando ya barabara ya Dar- Morogoro, eneo la Kimara jana.
Tukio hilo lilizua taharuki kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaomiliki mabanda hayo, ambao walihaha kuokoa mali zilizokuwa ndani, bila mafanikio.

Msimamizi mwandamizi wa operesheni hiyo, Hamis Abdul alisema kazi hiyo ni endelevu na kwamba baada ya kutoka Kimara, watahamia barabara ya Bagamoyo eneo la Tegeta huku akiwatahadharisha wafanyabiashara waliovamia maeneo hayo, kuhama mara moja.

Abdul aliwataka wafanyabiashara wote wanaofanya shughuli zao katika hifadhi za barabara kuondoka maeneo hayo kwa hiari yao kuepuka hasara ya kubomolewa mabanda yao.

 “Zoezi hili ni endelevu na kwamba baada tu ya kumaliza barabara hii ya Morogoro,  operesheni hii itahamia katika maeneo ya  Tegeta, kwa hiyo ningependa kutumia fursa hii kuwapa tahadhari wafanyabiashara waliovamia  maeneo ya barabara kuondoka kabla hatujafika huko,” alionya.

Wenye vibanda
Baadhi ya waliobomolewa vibanda, walilieleza gazeti hili kuwa pamoja na kufanyika ubomoaji huo, hawako tayari kuondoka.
Walisisitiza kuwa watarudi katika maeneo yao hayo ya awali mara tu baada ya operesheni hiyo kukamilika.
Rwezaura Gerasian mfanyabiashara wa nguo na viatu eneo la Kimara mwisho, alisema Serikali imeshindwa kuwahudumia wananchi na kwamba inakiuka haki za binadamu.

Alisema  kitendo cha Waziri Magufuli kutoa amri ya kuwaondoa katika maeneo hayo si cha  kiungwana, kwani  kinawakandamiza wananchi wa chini na kuendeleza uonevu kwa jamii.

“Sielewi lengo la Serikali yetu, maana inatenda mambo ya ajabu kwa wananchi wake bila hata huruma, huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu, tunahaki ya kufanyabishara kwa uhuru katika nchi yetu, kwanini tuishi kama wakimbizi?” Alihoji Gerasian.

Zoezi hilo la bomoabomoa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Magufuli kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania         (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam, kuwaondoa katika  hifadhi za barabara wafanyabiasha wote waliovamia maeneo hayo.
Dk Magufuli alitoa amri hiyo hivi karibuni wakati akizindua  kituo cha daladala cha Mbezi Mwisho.

Agizo la Magufuli na foleni Dar
Machi 4 mwaka huu, akizungumza wakati wa uzinduzi wa stendi hiyo mpya ya mabasi Mbezi mwisho, Dk Magufuli alisema hakuna sababu ya watu hao kubaki katika hifadhi za barabara wakati sheria zipo na kusisitiza, "Hata kama mkikuta milingoti ya bendera ya CCM vunjeni."

Dk Magufuli alisema, Sheria ya Barabara ya mwaka 1987 inasema wazi kuwa mtu ambaye atakutwa anafanya biashara, kuegesha gari, kumwaga mafuta au uvamizi mwingine wa namna yoyote katika hifadhi ya barabara, adhabu yake ni faini ya Sh1 Milioni.

Alimwagiza meneja huyo kuwa Tanroads haipo kisiasa na wao wapo kusimamia sheria na sio vingine. "Mpo kusimamia sheria, acheni kupiga siasa," alisisitiza.


Dk Magufuli alitoa mfano wa wafanyabiashara wa eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam ambao wamekuwa wakikwaza ujenzi wa barabara ya Bagamoyo kutokana na kupanga bidhaa zao barabarani.

''Ukienda Tegeta watu wamepanga biashara barabarani, Mkuu wa Mkoa upo, Mbunge yupo, Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) yupo, diwani yupo, mkuu wa wilaya naye pia na wote hao wanaangalia tu, ndio Tanzania hiyo?," alihoji na kusisitiza kuwa ifike mahali sheria iachwe ifanye kazi.
Habari na Mwananchi.

No comments:

Post a Comment