NJOMBE

NJOMBE

Friday, March 9, 2012

Muhimbili wafunga huduma zote kwa mgomo taifa la tikisika

                                                       Hospitali ya Taifa Muhimbili
WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikitishia kuchukua hatua nzito juu ya sakata la madaktari, mgomo wa wataalamu hao wa afya ulioanza kwa nguvu juzi, umeshika kasi na kusababisha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ikifunga huduma zote za matibabu kwa wagonjwa wa nje.
                                                   
Habari kutoka sehemu kadhaa nchini, zimebaini kuwa mgomo huo umesababisha wagonjwa wengi kutelekezwa nje ya milango ya hospitali na wengine wakihamishwa na ndugu zao kupelekwa katika hospitali binafsi ama kurudishwa nyumbani.
                                                          Wauguzi hospitali ya Taifa Muhimbili 
Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, idadi kubwa ya madaktari haikufika kabisa kazini, na kukifanya Kitengo cha Mifupa (MOI) kusimamisha huduma zote zinazotolewa kwa wagonjwa wanaotoka nje (OPD).
Msemaji wa kitengo cha MOI, Juma Almasi, aliliambia Tanzania Daima kuwa idadi ya madaktari imepungua kutoka 72 hadi kubakia 10 ambao ni wa vitengo maalumu na wanaohangaika kuwahudumia wagonjwa waliolazwa.
“Tulikuwa tunapokea wagonjwa zaidi ya 100 kwa siku lakini kwa sasa hatuwezi kupokea tena kutokana na mgomo unaoendelea hadi pale utakapositishwa.
“Tumekubaliana kuwa wagonjwa 237 waliolazwa wataendelea kupata huduma hizo, lakini tumefunga kabisa kupokea wagonjwa wengine,” alisema Almas.
Musa Hassan mgonjwa wa miguu pamoja na Kulwa Haroun ambao walikuwa wakipata matibabu ya nje katika Hospitali ya Muhimbili, waliliambia Tanzania Daima jinsi walivyokataliwa kuhudumiwa, wakiambiwa kurejea nyumbani hadi hapo mgomo utakapokwisha.
Hali kama hiyo imezikumba pia hosptali za Amana na Temeke jijini Dar es Salaam, ambako wagonjwa waliofika kupata huduma za tiba walikataliwa kupokelewa.
Kikao kinachodaiwa kuitishwa na maafisa wa Wizara ya Afya, kilikuwa kikiendelea katika ofisi ya mganga mkuu wa hospitali ya Amana, ikidaiwa kuwa walikuwa wakijadili namna ya kukabiliana na madhara ya mgomo.
Uchunguzi wa gazeti hili, umebaini kuwa madaktari waliofika kutoa huduma walikuwa 16 tu kati ya 70, na ambao walikuwa wakifanya kazi za dharura tu zikiwemo za mama wajawazito.
Katika Hospitali ya Temeke, huduma zilitolewa kwa wagonjwa mahututi tu, huku ikidaiwa kuwa madaktari walikuwa kwenye kikao cha dharura.
Waraka wa vitisho wasambazwa
Kutoka Mbeya, habari zinasema kuwa serikali imesambaza waraka ukiwaagiza wakuu wa hospitali zote inazozimiliki kuwabana madaktari wanaoendelea na mgomo.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya umefikishiwa waraka huo, na Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Omary Salehe, ambaye alithibitisha kuupokea kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ukiwataka kupeleka majina ya madaktari wanaoendelea na kazi kila siku katika kipindi chote ambacho madaktari wataendelea na mgomo.
Hata hivyo Dk. Salehe alisema kuwa baadhi ya madaktari ambao juzi walishiriki mgomo katika hospitali hiyo, jana walifika kazini na kuendelea kuwahudumia wagonjwa kama kawaida.
CHADEMA yatishia kuchukua hatua nzito

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetishia kuchukua hatua nzito zitakazosababisha kuwajibika kwa serikali nzima ikiwa Rais Jakaya Kikwete hatachukua hatua za haraka kumaliza mgomo huo.
Taarifa ya CHADEMA kwa vyombo vya habari jana, imesema kuwa tangu mgogoro wa madaktari uanze Kikwete ameshindwa kutumia ipasavyo mamlaka yake ya Kikatiba kuisafisha serikali yake wala hakuzungumzia kwa kina mgomo wa madaktari Februari 29, 2012 katika hotuba yake kwa taifa, wala hakuchukua hatua za msingi hali inayoashiria ombwe la uongozi.
CHADEMA imesisitiza wito wake wa kumtaka Rais Kikwete kulivunja baraza la mawaziri ili kufanya mabadiliko ya kimsingi ya kuongeza uwajibikaji kama ilivyoazimiwa pia na Kamati Kuu ya chama hicho katika mkutano wake wa Machi 3-4, 2012.
Kimemshutumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kwa madai kuwa amekuwa akitoa kauli zinazopingana katika suala hilo moja la mgomo wa madaktari, ambazo badala ya kushughulikia vyanzo vya mgogoro vimesababisha mgomo mwingine wa madaktari wenye athari kubwa kwa wananchi.
“CHADEMA haijaridhishwa na maelezo yaliyotolewa na serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda Februari 9, 2012 na Machi 7-8, 2012 kuhusu namna ambavyo imeshughulikia mgogoro huu na madai ya madaktari; na watumishi wengine wa umma katika sekta ya afya pamoja na uboreshaji wa huduma katika hospitali, zahanati na vituo vya afya nchini.
Kimesema kuwa serikali imekuwa ikiingia gharama kubwa kupeleka viongozi kutibiwa nje ya nchi, huku huduma katika hospitali za umma zikizidi kuzorota kutokana na ukosefu wa madawa, vifaa tiba na wataalamu wa kutosha katika hospitali za umma.
Aidha serikali inashindwa kuipa kipaumbele sekta ya afya kwa kisingizio cha kutokuwa na uwezo wakati ambapo inafanya matumizi mengine ya anasa kwa kiwango kikubwa kama ilivyokuwa katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru.
“Serikali inachelewa kushughulikia madai ya posho za madaktari kama nyongeza ya posho ya kulala kazini (on call allowance) na posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (risk allowance) wakati huohuo serikali hiyohiyo inazungumzia nyongeza ya fedha katika matumizi mengine ya serikali yasiyokuwa ya lazima.
“Aidha CHADEMA inarudia kuitaka serikali kupanua wigo wa uchunguzi na kuwezesha tathmini huru kufanyika ya athari za mgogoro na mgomo ulioendelea ikiwemo kueleza wazi idadi ya vifo vilivyotokea na madhara yaliyojitokeza katika hospitali za umma tofauti na kauli potofu iliyotolewa bungeni Februari 3, 2012 na waziri husika.
Chama hicho kimeionya serikali kuacha vitisho na matumizi makubwa ya vyombo vya dola kwa madaktari na makundi mengine katika jamii yanapotumia uhuru wa Kikatiba kukusanyika, kujadiliana na kuhoji kuhusu uwajibikaji wa serikali na viongozi wake kwa kuzingatia ibara za 8, 18 na 20 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kikwete kuzungumza leo

Habari zilizotufikia wakati tunaenda mitamboni, zimesema kuwa Rais Jakaya Kikwete leo atakutana na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuzungumzia sakata la madaktari.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadick, amethibitisha kuwa Kikwete atakutana na wazee hao katika Ukumbi wa Diamond Jubilee majira ya saa kumi jioni.
Hata hivyo, Sadick ameonekana kwenda kinyume na hali halisi ilivyo katika hospitali za serikali za mkoa wa Dar es Salaam, baada ya kudai kuwa huduma zilikuwa zikitolewa kama kawaida na pale penye upungufu, kulikuwa kumeandaliwa utaratibu wa kuwapeleka wagonjwa katika hospitali binafsi.
“Baada ya mgomo wa kwanza, serikali imezijengea uwezo hospitali za mkoa ili ziweze kumaliza matatizo bila kupeleka wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Tunaendelea kutafuta suluhisho ili kuhakikisha zoezi hili halitishii maisha ya Watanzania. Tumeshatoa maelekezo kwa waganga wakuu wa hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke linapotokea tatizo lililo nje ya uwezo wao waende wapi hata kwa fedha za serikali,” alisema.
Kwa habari zaidi na mengine soma Mtanzania daima

No comments:

Post a Comment