NJOMBE

NJOMBE

Sunday, March 11, 2012

Mgombea ubunge CCM awekewa pingamizi Arumeru

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), jana kilimwekea pingamizi mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Arumeru Mashariki, Siyoi Sumariki kikitumia barua iliyoelezwa kuwa ya siri ambayo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo aliandikiwa na Idara ya Uhamiaji mkoani hapa kuhusiana na utata wa uraia mgombea huyo.

Katika kinyang’anyiro cha kura za maoni, Mkuu huyo wa Mkoa, alidaiwa kuwa katika kundi ambalo lilikuwa linampinga mgombea huyo wa CCM kupitishwa.

Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa Chadema, John Mrema alisema jana kwamba barua hizo ambazo mwananchi imeziona zinatoa uthibitisho juu ya utata wa uraia wa mgombea huyo wa CCM na hivyo kupoteza sifa.

Katika barua hiyo, yenye kumbukumbu namba AR/C/32/VOL.1/85 iliyoandikwa na Ofisa Uhamiaji mkoa wa Arusha, D. Namomba kwenda kwa Mkuu huyo wa Mkoa, ilieleza kuwa taratibu mbalimbali za kisheria za mtu kuwa raia au la.

Katika barua hiyo iliyoandikwa Februari 29 mwaka huu, Ofisa Uhamiaji huyo, alitoa ufafanuzi wa sheria hiyo kutokana na maombi ya kufanya hivyo, aliyotakiwa na Mkuu huyo wa mkoa, kupitia barua yenye kumbukumbu namba CFA/18/114/01/20.

Kwa mujibu wa barua hiyo, ofisa huyo ameeleza kuwa mgombea huyo alizaliwa Thika, Kenya, Mei 11, 1979.

Hata hivyo, barua hiyo ilieleza kuwa kulingana na Sheria ya Uhamiaji namba 7 ya mwaka 1995, kuna uraia wa aina tatu, ambao ni wa kuzaliwa, kurithi na kuomba.

Akizungumzia kifungu alisema mtu ambaye anazaliwa nje ya nchi kama atarithi uraia wa wazazi wake mmoja au wote, ukomo wake ni miaka 18.

Alisema kama mtu atakuwa amezaliwa nje ya nchi na amefikisha miaka 18 anapaswa kuukana uraia alionao na kuomba uraia wa nchi ambayo anaishi kwa kuapa kiapo cha utii, jambo ambalo idara hiyo haina kumbukumbu kama Siyoi aliukana uraia wa nchi alikozaliwa au la jambo ambalo hata hivyo, limekuwa halizingatiwi na watu wengi.

Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Trasias Kagenzi alithibitisha jana kupokea pingamizi hilo na kuomba kupewa muda zaidi wa kuupitia kabla ya kulizungumzia jambo hilo... “Naomba tuwasiliane baadaye kidogo ndiyo nazipitia kumbukumbu hizi, nadhani tutatoa taarifa baadaye.”

Chadema kampeni leo

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, leo anatarajiwa kuzindua rasmi kampeni za chama hicho katika kuwania ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kampeni hizo zitazinduliwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Liganga, Usa River na zitahudhuriwa na wabunge wote wa chama hicho na viongozi wa kitaifa na pia zitarushwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha Star TV kuanzia saa 9:00 alasiri.

Kuhusu uchaguzi huo, Mwigamba alisema: “Huu ni tofauti na chaguzi zote zilizopita. Kwanza tuna mtandao mkubwa wa chama hapa, tuna mgombea anayekubalika zaidi na pia tumejipanga kulinda kura zetu.”

Alisema mgombea wao, Joshua Nasari (26) ambaye pia aligombea katika uchaguzi uliopita, atafanya kampeni katika kata zote 17 za jimbo hilo ili kujihakikishia ushindi.

127,000 kupiga kura

Akizungumzia wapiga kura, Kagenzi alisema watu 127,000 wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo akisema kwamba
hao ni wale waliojiandikisha katika daftari lililotumika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Alisema katika uchaguzi huo pia kutakuwa na vituo 327 na kwamba vyote vimeandaliwa sambamba na waratibu wasaidizi wa uchaguzi.

Vyama vinane vinatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo. Mbali na CCM na Chadema, vingine ni TLP kilichomsimamisha Abraham Chipaka, SAU (Shabani Kirita); UPDP (Charles Msuya); DP, (Mohamed Abdallah) na NRA, (Hamis Kieni).

Ombi

Vyama saba vinavyoshiriki uchaguzi huo vimeliomba Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutenda haki kwa vyama vyote badala ya kukipendelea CCM ili kuepusha vurugu.

Wakizungumza wakati wa kikao cha kuwekana sawa, wawakilishi wa Chadema na UPDP walisema uzoefu unaonyesha kuwa vyombo vya dola na NEC huegemea upande wa CCM kwenye malalamiko mengi yanayowasilishwa na vyama vya upinzani, hali inayowafanya wapinzani kuhisi kupuuzwa na wanye dhamana ya kuwatetea.

“Kila mtu, vyama vya siasa, polisi, Takukuru na NEC watekeleze na kusimamia majukumu yao kwa kufuata na kuzingatia sheria na taratibu za uchaguzi. Uchaguzi ufanyike Meru na kuwaacha wananchi wakiwa na amani, umoja na mshikamano. Tusiwaache wakiwa hawasalimiani. Sote tuna jukumu la kuhakikisha tunafanya kampeni za kistaarabu,” alisema Mwakilishi wa Chadema, Basil Lema.

Lema ambaye ni Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, alisema pamoja na kuahidi siasa na kampeni za kistaarabu, kamwe hawatakubali kuonewa na kuonya kuwa chama chake kimejiandaa kukabiliana na dhuluma au hujuma yoyote.

Mwakilishi wa UPDP, Mussa Ayo aliwataka polisi kusimamia utekelezaji wa muda wa kuanza na kumaliza kampeni hasa kwa upande wa CCM ambao alidai kuwa wamekuwa wakiendelea na mikutano yao hata baada ya Saa 12:00.

“Kampeni isihusishe kashfa wala kuponda vyama vingine. Kila chama kitangaze sera zake na kuomba kura, Arumeru isiwe kama Igunga ambako watu walipambana kwa matusi, mapigano na hata kumwagiana tindikali,” alisema Ayo.
Kwa upande wake, Msimamizi wa uchaguzi huo aliwataka wadau wote kuzingatia sheria katika kila jambo wanalofanya na kuahidi kutenda haki kwa vyama vyote ili kuhakikisha unakuwa huru na haki.

Alimwomba kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Arumeru kuwarejeshea shahada zao za kupigia kura wananchi waliozitumia kuwawekea dhamana ndugu zao wenye kesi katika vituo mbalimbali vya polisi wilayani humo ili kuwawezesha kushiriki kupiga kura Aprili Mosi, mwaka huu.

Kikao hicho kiliwashirikisha, Kagenzi pamoja na Kamanda wa Polisi Wilaya ya Arumeru, Benedict Mapujila.

Habari hii imeandaliwa na Mussa Juma, Arumeru na
Peter Saramba, Arusha

Habari na Mwananchi

No comments:

Post a Comment