NJOMBE

NJOMBE

Thursday, March 22, 2012

Raia wa Zambia wazua vurugu mpakani Tunduma

Vurugu zimeibuka katika mji mdogo wa Tunduma mpaka wa Tanzania na Zambia kufuatia wananchi wa Zambia kudaiwa kuwazuia wafanyabiashara kutoka Tanzania kuvuka mpaka kwenda kufanyia biashara zao nchini humo.
Kutokana na hatua hiyo, Watanzania nao walijibu mapigo kwa kuwatimua raia wa Zambia waliokuwa wakifanya biashara zao upande wa Tanzania na hivyo kusababisha kuibuka kwa vurugu katika mpaka huo.
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Gabriel Kimolo, akizungumza na NIPASHE jana mjini Vwawa alisema baada ya kujulishwa kutokea kwa vurugu hizo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya imekwenda mjini Tunduma ambako walijadiliana kwa pamoja na hatimaye vurugu hizo kudhibitiwa.
“Ni kweli nimejulishwa kuwapo kwa tukio hilo. Lakini kimsingi hazikuwa vurugu kubwa. Kamati ya Ulinzi na Usalama imeweza kulishughulikia suala hilo na sasa hali imetulia katika mji huo,” alisema Kimolo.
Hata hivyo, alisema vyombo vya ulinzi na usalama vimechukua hatua ya kuimarisha ulinzi katika kila kona ya mji huo ili kusitokee machafuko zaidi yatakayoleta athari kwa wananchi wa Tunduma na wageni kutoka nchi mbalimbali.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji wa Tunduma, Aidan Mwashiga, alisema vurugu hizo ziliibuka baada ya wananchi wa mji wa Nakonde Zambia kuendesha operesheni ya kuwatimua Watanzania wanaofanya biashara zisizokuwa za halali katika mji huo.
Alisema kufuatia hali hiyo, Watanzania nao walichukua hatua ya kuanza kuwatimua wafanyabiashara wa Zambia wanaofanya biashara zao katika mji wa Tunduma na kusababisha kutokea kwa vurugu.
Hata hivyo, alisema vurugu hizo zimedhibitiwa na vyombo vya  ulinzi na usalama na kwamba askari wamewekwa tayari katika mji wa Tunduma ili kama kutaibuka vurugu ziweze kudhibitiwa.
Mji wa Tunduma umekuwa mara kadhaa ukikumbwa na vurugu zinazosababishwa na wafanyabiashara wa pande mbili.
Mwaka 2005, mfanyabiashara wa Tanzania aliuawa na askari polisi wa nchini Zambia na hivyo kusababisha mpaka wa Tanzania kufungwa kwa siku tatu hadi serikali ilipomaliza tatizo hilo kwa kukaa na serikali ya Zambia.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, alipofanya ziara wilayani Mbozi, aliagiza Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kuimarisha ulinzi katika mji wa Tunduma kufuatia kutokea kwa matukio ya vurugu mara kwa mara katika mji huo.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

  1. VEMDIMI UVE AMALANGA AGO AHUFUNDISIDZE YE NANINI?
    VIPI INDONYA YITONYA SANA HUNYUMBA UHO? NDILIMNYALUKOLO VAHO ILA ISAA IDZI NDILI HUMZUMBE NDISOMA HWENUHO.ALL THE BEST!

    ReplyDelete