NJOMBE

NJOMBE

Monday, March 19, 2012

BINTI MSAGAJI KATENGENEZWA NA WAZAZI!

Malezi huweza kuwaathiri!



Mwanamke ambaye ana tabia a kujilaumu yeye kama mwanamke na kulaani kuwa kwake mwanamke, yuko kwenye nafasi kubwa ya kumuuwa mtoto wake wa kike kisaikolojia. Kuna wanawake ambao kwa kuudhiwa na waume zao au hata na wanawake wenzao huwa wanapenda sana kuropoka kauli za kudhalilisha jinsia ya kike.

“Mimi nakwambia sisi wanawake hatufai kabisa, kuzaliwa mwanamke ni jambo baya sana………ningekuwa naweza nimwombe Mungu anibadilishe niwe mwanaume …. Wanawake ni wajinga sana….” Kauli za aina hii zinaporudiwa mara mbili au tatu humfanya mtoto wa kike kuziamini na huanza kuwa na wasiwasi na jinsia yake. Hata watoto wa kiume nao huziamini kauli hizi na kuanza ‘ubabe’ wa kiume kuanzia hapo.

Mtoto wa kike anapozisikia kauli hizi kutoka kwa mama yake na kwa sababu mama yake ndiye ‘shujaa’ wake, huanza kujenga dhana kwamba, kama mama yake hapendi kuwa mwanamke, kwa sababu mwanamke ni mjinga na dhaifu, naye hana budi kuikimbia hali hiyo.

Anaikimbiaje?

Kuna njia nyingi za kukimbia hali hiyo, lakini kubwa na ya karibu ni kwa mtoto huyu kuanza kujibainisha na jinsia ya kiume. Kwa sababu akili ya mtoto haichuji, huanza kuhisi vibaya kuwa kwake mwanamke mbele ya wenzake, hasa wanaume. Kujibainisha na jinsia ya kiume ni pamoja na kufuatana na wanaume, kuvaa kiume, kuongea kiume, kutembea kiume na kufanya kazi za kiume.

Siyo lazima, lakini mtoto huyu anaposhindwa kupata mahali ambapo atadondosha dhana au imani hii, ni wazi atakuja kujibainisha kimapenzi, atajibainisha kama mwanaume. Matokeo ya jambo kama hili ni kuwa na mwanamke ambaye anataka kuwa mwanaume kwa wanawake wenzake kimapenzi.

Kama sio kauli za akina mama kujilaumu, kauli za akina baba kuwalaumu wanawake pia na akina mama kuzikubali kivitendo, zinaweza kuwaathiri watoto wa kike kimakuzi. Baba anapokuwa na tabia ya kutoa kauli kali na chafu dhidi ya mama, na mama kuonyesha kukubaliana na kauli hizo kwa vitendo ni hatari sana.

Hebu sikia kauli kama hii kutoka kwa baba: “Mwanamke gani anayezaa mitoto ya kike tu, ni afadhali kuoa mke mwingine…..” majibu ya mwanamke anayekashifiwa ni haya: “Kwani mimi nimetaka, si Mungu mwenyewe, kwani hata mimi si ninapenda watoto wa kiume……” Kwa mtoto wa kike majibu kama haya, huwa yanasikika masikioni mwake kama, “Hata mimi sitaki watoto wa kike kwa sababu hawana thamani, lakini sina uwezo wa kuwakataa..”

Akina mama, yawapasa kuelewa kwamba, kauli zao na kuzipa kauli za waume zao nguvu, huweza kuwaathiri sana watoto wao. Kila neno wanalotamka kwa watoto ni lazima walikague mara mbili. Waume zenu wanapotoa kauli zinazobagua watoto kijinsia mbele ya watoto hao ni lazima mzikanushe sawia na kuwaeleza watoto ukweli utakaowapa nguvu ya kufurahia jinsia waliyonayo.

No comments:

Post a Comment