NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, March 20, 2012

Wanajeshi waua raia watano kwa risasi

Watu watano wameuawa kwa kupigwa risasi na wengine wanne kujeruhiwa baada ya kuzuka tafrani baina ya wananchi na wanajeshi waliokuwa wakishirikiana na mgambo kuendesha operesheni maalum ya kuwaondoa waliovamia eneo la hifadhi katika kijiji cha Maguba, kata ya Igawa, tarafa ya Malinyi wilayani Ulanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Adolphina Chialo, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo saa Jumamosi iliyopita saa 8:00 mchana.
Waliouawa ni Sanyiwa Ndaya (34), Lutaya Ndala (48), Nchambi Bujiku (28), Kulwa Luhende (48) na Shija Msheshiwa (35), ambaye alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Ulanga. Wote wakazi wa Kijiji cha Mguba, kata ya Igawa.
Waliojeruhiwa na kulazwa  Hospitali ya Wilaya ya Ulanga ni Nkama Jisonge (35), Zina Msheshiwa (30), Msheshiwa Taiya (60) na MT 70328 Koplo Paulo Lawrent ambao hali zao zimeelezwa kuendelea vizuri.
Akifafanua kuhusiana na tukio hilo, Kamanda Chialo alisema kuwa siku ya tukio askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Job Edward (54) Ofisa Mteule wa daraja la pili, ambaye ni mshauri wa mgambo wilaya ya Mahenge akiongoza timu ya watu 15 akiwemo askari mwingine wa jeshi hilo, MT 70328 Koplo Paulo Lawrent na mgambo, walikwenda katika eneo hilo kwa ajili ya operesheni maalum ya kuwaondoa watu waliovamia hifadhi hiyo.
Kwa mujibu wa Kamanda Chialo, watu hao baada ya kufika walivamiwa na wananchi waliokuwa na silaha za kijadi na walipojaribu kujitetea, Koplo Lawrent aliyekuwa na bunduki aina ya SMG alifyatua risasi hewani ili kuwatawanya wananchi hao ambao waliendelea kupambana nao.
“Na yeye huenda katika kunusuru silaha ile isiporwe na wananchi, alirusha risasi hewani zilizopoteza maisha ya wananchi wanne pale pale katika eneo la tukio, huku mwananchi mmoja akifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mahenge,” alisema Kamanda Chialo.
Kufuatia tukio hilo, Chialo alisema watu wanane wamekamatwa na wanahojiwa na polisi ili hatua zaidi za kisheria dhidi yao zikuchukuliwe na kuongeza kuwa Polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Awali, ilidaiwa kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Morogoro ilikwenda katika eneo hilo na kuwazuia wananchi kuendelea na shughuli za kilimo na uharibifu wa mazingira katika eneo hilo la hifadhi, lakini walikataa kwa madai kuwa hawafahamu mipaka kati ya eneo lao na eneo la hifadhi.
Inadaiwa kuwa mipaka hiyo iliwekwa na Serikali na wananchi hao kutakiwa kutii mamlaka ya Serikali kwa kuacha kufanya uharibifu ndani ya hifadhi bila mafanikio, hadi ilipofanyika operesheni hiyo katika eneo hilo ambalo ni hifadhi ya wanyamapori linalomilikiwa na wizara ya Maliasili na Utalii.
Habari kamili na Nipashe

No comments:

Post a Comment