NJOMBE

NJOMBE

Friday, March 9, 2012

Mwalimu achapwa kwa tuhuma za ushirikina

MWALIMU wa Shule ya Msingi Juhudi, Ilemi jijini Mbeya, Eliud Kyando, amecharazwa bakora na wananchi kwa kile kilichodaiwa kuwa anajihusisha na vitendo vya ushirikina.
Tukio hilo lilitokea Februari 6, mwaka huu, shuleni hapo baada ya wananchi na baadhi ya walimu kumtuhumu mwalimu huyo kuwa amekithiri kwa kupaka kinyesi cha binadamu katika samani za mwalimu mkuu na vyombo vya kupikia chakula cha walimu wa shule hiyo.
Sakata hilo la aibu, baada ya kuvumiliwa kwa muda mrefu hatimaye viongozi wa kimila walibaini kuwa aliyekuwa akifanya hivyo ni Mwalimu Kyando ambaye alikuwa akiona wivu kuwa kwa nini alikuwa hateuliwi kushika nafasi ya ukuu wa shule hiyo wakati amekaa muda mrefu shuleni hapo. Ndipo ukaitishwa mkutano wa hadhara.
Katika mkutano huo, wananchi wakamuonya mhusika kutorudia vitendo hivyo lakini baada ya wiki mbili, vilijirudia na kuonekana kinyesi katika samani za ofisi ya mwalimu mkuu na ofisi za walimu huku milango ikiwa imefungwa.
Baada ya kuona hivyo wananchi waliamua kuitisha tena mkutano wa hadhara na kwenda kumuona ofisa elimu wa jiji la Mbeya na mkurugenzi ambapo majibu yalikuwa ni kuifunga shule hiyo mara moja.
Baada ya kuona hivyo, wazazi walikasirishwa kufungwa shule hiyo wakati mtuhumiwa yupo, na hapo ndipo vijana wakaamua kumsaka na hatimaye kumwadhibu mpaka pale alipookolewa na askari polisi.
Hata hivyo, wananchi hawakuishia hapo kwani waliifuata familia ya mwalimu huyo na kuiamuru iondoke na shule ikafunguliwa.
Taarifa za uhakika zimeeleza kuwa tukio hilo kwa mwalimu huyo ni la pili ambapo awali alifukuzwa Shule ya Msingi Itagano kwa tuhuma hizo hizo za ushirikina.
Baada ya sakata hilo walimu wa shule hiyo walitumia muda wa siku nzima kujadili kitendo cha kupigwa mwalimu mwenzao na kuweka mikakati ya vitendo hivyo visitokee tena, kwani hata mahudhurio ya wanafunzi hayakuwa mazuri darasani wakihofia vitendo vya kishirikina.
Habari zaidi na Mtanzania Daima

No comments:

Post a Comment