KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe,
amewashawishi wabunge wa upinzani kupitisha marekebisho ya mabadiliko ya
Katiba, huku akionya kuwa utamaduni unaojengwa bungeni sasa unabeba
sura ya ‘funika kombe mwanaharamu apite’.
Hatua hiyo, ilitokana
na mvutano kati ya wabunge wa CCM na wale wa upinzani, kuhusu upitishaji
kifungu cha 17 cha sheria hiyo baada ya kufanyiwa marekebisho na kuweka
wakuu wa wilaya na wakurugenzi kwamba wanaweza kutumiwa na Tume ya
Katiba kuitisha mikutano ya maoni.
Marekebisho ya kifungu hicho
juzi yalilazimika kurejeshwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, baada ya
kutokea mvutano mkali kati ya wabunge wa CCM ambao walikuwa wakitaka
kuwekwa mkuu wa wilaya, huku upinzani ukitaka mkurugenzi wa halmashauri
kama ilivyopendekezwa na Serikali.
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu
wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema, alipendekeza ili kuondoa kila
upande kuonekana mshindi kwa suala hilo, kifungu hicho kiruhusu mkuu wa
wilaya na mkurugenzi wanaweza kutumiwa na Tume ya Katiba, kuitisha
mkutano wa maoni ingawa yalipingwa na wabunge wa CCM.
Mvutano huo
ulimlazimisha Spika Makinda kurudisha kifungu hicho kwenye Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala ili kijadiliwe na kuona kinavyoweza
kutekelezwa kwa njia nzuri.
Akisoma maafikiano ya Kamati na pande
husika jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Angela Kairuki (CCM),
alisema wamekubaliana na marekebisho yaliyopendekezwa na AG, ya kuwekwa
kwa mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri.
Hata hivyo, Mbunge
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alisema marekebisho hayo ni
mkanganyiko mtupu na kwamba, wakurugenzi wa halmashauri wanatosha
kutumiwa na Tume ya Katiba, lakini kuingiza wakuu wa wilaya kunalenga
kulinda maslahi ya CCM.
Mbowe alilazimika kuingilia kati na kuomba wapinzani kupitisha marekebisho hayo kwa ajili ya mustakabali wa nchi.
“Wakurugenzi
wa halmashauri ni watendaji wa Serikali ya CCM, wanaosimamia shughuli
za maendeleo ya wananchi… inasikitisha kuona kwamba Serikali haiwaamini
watumishi wake,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Wabunge wa upinzani
tunalazimika kuweka record (kumbukumbu) kukubaliana na marekebisho ya
Mwanasheria Mkuu yapite…, lakini utamaduni huu tunaojenga humu ndani wa
‘kufunika kombe mwanaharamu apite utatu-cost (gharimu) baadaye.
“Wabunge
wenzangu wa upinzani tukubali jambo hili limalizike kwa sababu lazima
tufike sehemu tu-compromise (turidhie) twende tukatunge Katiba ambayo
itadumu zaidi ya miaka 100 bila kujali kuwapo kwa CCM au Chadema.”
Baada
ya Mbowe kumaliza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano),
Steven Wassira, alisimama na kumpongeza kwa kutumia hekima na busara
kushawishi wenzake.
Maoni ya Dk Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk Willibrod Slaa amewaasa Watanzania kutokubali kuburuzwa na watu
watakaotoa elimu ya upotoshwaji wakati wa mchakato wa kuandika Katiba
Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzingatia maslahi yao
binafsi.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana Dk
Slaa, alisema ikiwa itikadi zitaachwa zitawale mchakato huo ni hatari
kwa kuwa zinaweza kuliingia taifa kwenye migogoro huku ikiwezesha
kupatikana kwa Katiba isiyo na manufaa kwa wananchi.
“Suala
kuandika Katiba Mpya ni kubwa, linahitaji umakini na ushirikishwaji.
Ombi langu ni kwa wananchi, nawasihi kutokubali kuburuzwa na watu
wachache watakaotoa elimu kuhusu Katiba yenye mlengo wa itikadi za vyama
vyao vya siasa,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Mtu yeyote awe wa
CCM, Chadema au chama chochote ikigundulika anafanya kazi hiyo kwa
itikadi ya chama chake cha siasa, apuuzwe kwani Katiba ni chombo muhimu
cha kitaifa kinachopaswa kubeba maslahi ya Taifa la Tanzania kwa kipindi
kirefu kijacho.”
Alisema ikiwa wananchi wataruhusu hali hiyo
iliyojitokeza, mchakato wa kupata Katiba yenye maslahi ya kitaifa
hautafanikiwa, badala yake taifa linaweza kuingia katika kipindi cha
miaka hamsini mingine likiwa na Katiba isiyokidhi mahitaji ya
Watanzania.
“Nimelazimika kusema hayo kwa sababu ninazo nyaraka
za CCM zinazowahimiza wanachama wao kutumia kila njia kuhakikisha
wanaingiza mahitaji yao mengi katika katiba mpya. Nawasihi wananchi
wayakatae na wahakikishe kuwa kila kinachoingia kwenye Katiba Mpya
kinahusu maslahi ya taifa na si ya chama fulani; mwisho wa siku tusije
kuwa na Katiba yenye mlengo wa chama cha siasa,” alisema Dk Slaa.
Alielezea
dhamira ya chama chake kuwa ni kutetea maslahi ya taifa na kwamba hiyo
ndiyo sababu iliyowafanya waanzishe na kusimamia agenda ya kutaka
kuandikwa kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania muda mfupi
baada ya kumalizika kwa uchaguzi.
Akizungumzia mjadala bungeni
kuhusu Katiba Mpya, Dk Slaa alielezea kusikitishwa kwake na namna
wabunge walivyokuwa wakitetea itikadi za vyama vyao vya siasa badala ya
maslahi ya umma huku akiwapiga kijembe wabunge wa CCM kuwa waliacha hoja
na kujadili Chadema kumtambua Rais.
“Binafsi nilihuzunishwa na
namna wabunge walivyojadili mchakato wa Katiba Mpya, wengi waliweka
pembeni maslahi ya taifa na kujadili kwa kuzingatia misingi ya itikadi
za vyama vyao vya siasa , hata hivyo ninashukuru busara za mwenyekiti
wetu zilisaidia kufikia maridhiano,” alisema.
No comments:
Post a Comment