Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni
JESHI la Polisi Wilaya ya Kinondoni limesema halitambui maridhiano ya
madaktari na Serikali ya kuwaachia huru wanaharakati walioandamana
kushinikiza Serikali kutatua madai ya madaktari.
Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Kinondoni,
Charles Kenyera alisema wanaharakati hao watafikishwa mahakamani kama
watuhumiwa wengine.
Alisema Jeshi la Polisi ni Taasisi inayojitegemea na haiwezi kufanya kazi kwa shinikizo la madaktari.
Kenyera
alisema wanaharakati 16 waliokamatwa na Jeshi hilo
watafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa iwapo mwanasheria wa
Serikali ataona kuna umuhimu wa kupelekwa mahakamani.
“Ninachoweza
kusema hapa, upelelezi umekamilika na tumeshapeleka kwa Mwendesha
Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) ndiye mwenye uamuzi wa kuwafikisha
mahakamani,” alisema. Jana jeshi hilo lilishindwa ama kuwaachia au
kuwafikisha mahakamani wanaharakati 16 waolitiwa mbaroni Alhamisi
iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wakidaiwa kutaka
kuandamana kuishinikiza Serikali kumaliza haraka mgogoro wake na
madaktari.
Pia wanaharakati hao wanadaiwa kukutwa na mabango 30
yenye ujumbe tofauti wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda akizungumza na
madaktari ambao walikuwa katika mgomo na kudaiwa kufunga baadhi ya
barabara za jjiji la Dar es Salaam siku moja kabla ya kukamatwa kwao.
Wanaharakati
hao waliachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti Kituo cha Polisi
Oysterbay jijini Dar es Salaam jana (Jumanne) lakini walipofika kituoni
hapo walielekezwa kuonana na Ofisa Upelelezi Makosa ya Jinai Wilaya ya
Ilala (RCO), Kituo Kikuu cha Polisi Kati kwa ajili ya maelekezo zaidi.
"Wametutaka
turipoti kwa RCO Ilala, wanasema kwa kuwa tulikamatwa Muhimbili suala
letu linatakiwa kwenda Ilala na hapa Oysterbay limeletwa kimakosa,"
alisema Mkurugenzi Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen
Kijo-Bisimba.
Akizungumza na wanaharakati hao ofisini kwake,
Ofisa Upelelezi Ilala, Duwali Dila aliwaambia kuwa suala lao lipo katika
ngazi nyingine linashughulikiwa na warudi tena kituoni hapo Jumatatu
wiki ijayo ambapo atakuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kujua
kinachoendelea.
"Nafikiri tuonane Jumatatu, labda tukubaliane
muda kwani suala hili kulingana na taratibu zetu siku hizi za jeshi la
polisi lazima lipitie ofisi ya DPP kabla ya kufika kwetu," alisema na
kuongeza kuwa sio wao polisi ambao wanatakiwa kuandaa mashtaka.
Alisema
ofisi hiyo ndio ambayo inapaswa kuandaa shtaka kama lipo baada ya
kupitia vielelezo vyote na kujiridhisha kuwa kuna tuhuma ambazo
zinapaswa kupelekwa mahakamani au vingine kisha kuwasilisha polisi.
Dila
aliwahakikishia kuwa Jumatatu ndio itakuwa siku ya mwisho kwani
mchakato utakuwa umekamilika, hoja ambayo ilikubaliwa na wanaharakati
hao ambao waliondoka ofisini hapo na kuendelea na shughuli zao zingine.
Wanaharakati
hao walikamatwa wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokuwa na mkutano
na madaktari waliokuwa katika mgomo na walipopekuliwa katika magari yao,
ambapo walikutwa na mabango 30 yenye jumbe mbalimbali ambayo yalikuwa
yanaishinikiza serikali kumaliza mgogoro wake na madaktari.
Pia
siku moja kabla wanaharakati hao walifanya maandamano ya kutaka kwenda
Ikulu ambayo yalisababisha kufungwa kwa barabara ya Ocean na Ali Hassan
Mwinyi eneo la Palm Beach, jijini Dar es Salaam kabla hawajaamriwa
kutawanyika na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasi (FFU).
No comments:
Post a Comment