WAKAZI watano wa jijini Dar es Salaam akiwamo mganga wa jadi
wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku baadhi yao
wakiwa wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi, wakishitakiwa kwa kukutwa na
bunduki na risasi bila kibali.
Kati ya watuhumiwa hao watano, wanne walikuwa wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili huku nguo zao zikiwa na damu.
Baadhi yao walionekana wamefungwa plasta za jasi na miguuni kuwekewa vyuma vya kurekebisha mifupa na kushindwa kutembea.
Watuhumiwa hao walisomewa mashitaka nje ya mahabusu ya Mahakama.
Washitakiwa hao ni Yusuf Matimango (35), Athuman Kibambe (44), Ally
Ngingame (42), Said Mangala (40) na mganga wa jadi Asha Ungando (45).
Wakili wa Serikali, Frida Mwela alimuomba Hakimu Bingi Mashabala
kuwafuata washitakiwa mahabusu kuwasomea mashitaka kwa sababu hawezi
kutembea kutokana na majeraha waliyonayo pamoja na maumivu makali.
Hakimu huyo alikubaliana na ombi hilo na kwenda mahabusu ambapo
alisimama nje ya jengo la mahabusu na washitakiwa hao walitolewa nje na
kuanza kusomewa mashitaka yao ambayo walikana yote.
Katika mashitaka yao walidaiwa Februari 10 mwaka huu katika mtaa wa
Tandika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam walikutwa na Bunduki aina
ya Shot Gun na kukutwa na risasi katika tarehe hiyo hiyo na eneo hilo
hilo.
Baada ya kukana mashitaka, walidai kuwa walikamatwa na kupigwa na
askari wa kituo cha Polisi Sitakishari na wengine kupigwa risasi miguuni
bila kufahamu makosa yao.
“Mheshimiwa hakimu sisi tumekamatwa bila kidhibiti chochote na
tulipofika Polisi tulipigwa sana tukalazimishwa kusaini maelezo ambayo
hatuyajui na waliokaa wakapigwa risasi na mmoja wetu ameuawa,” alidai
Matimango.
Mganga Asha Ungado akiwa chini ya Ulinzi
Mshitakiwa mwingine alidai kuwa waliwekwa kituoni wiki nzima ndipo
walipelekwa Hospitali. Hata hivyo walifungwa majeraha tu bila kupewa
dawa yoyote huku mwingine akilalamika kuwa alisikia polisi wakiwaeleza
madaktari akatwe mguu tu.
Hakimu Mwashabala alitoa masharti ya dhamana yaliyowataka kuwa na
wadhamini wawili wa kuaminika pamoja na kusaini hati ya dhamana ya Sh
milioni mmoja kila mmoja.
Imeandaliwa na Habari leo
No comments:
Post a Comment