TUME ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeanza mchakato wa kuhakiki mali
za viongozi wa umma nchi nzima ambapo kwa awamu ya kwanza itaanza na
vigogo 60 akiwamo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel
Sitta na Waziri Samia Suluhu Hassan wa Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano). Wengine ni wakuu wa mikoa na wilaya, Meya wa majiji,
madiwani, wabunge na wakurugenzi wa taasisi mbalimbali za Serikali.
Zoezi
la uhakiki wa mali za viongozi hao litaanza Februari 20 hadi Machi mosi
mwaka huu ambapo linafanyika baada ya kukamilika kwa zoezi la
urejeshaji wa fomu za utajaji mali na madeni kutoka kwa watumishi
mbalimbali wa Serikali. Mbali na Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo
Mashariki, wabunge wengine watakahakikiwa mali zao katika awamu hiyo ni
John Mnyika(Ubungo), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Jerome Bwanansi
(Lulindi), Faith Mitambo (Liwale) na Stella Manyanya (Viti Maalum).
Katika
orodha hiyo yumo pia Meya wa Jiji la Mbeya Athanas Kapunga, Mkuu wa
Mkoa wa Lindi Ludovock Mwananzila, Meya wa Jiji la Dar es Salaam Didas
Masaburi na Meya wa Jiji la Tanga, Guledi Mohamed. Wengine ni Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Charles Nyamrunda, Mkurugenzi Mkuu
Shirika la Nyumba la Taifa(NHC), Nehemia Mchechu, Naibu Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Placidus Luoga na Mkuu wa Mkoa wa
Manyara Elaston Mbwilo.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana Kamishna wa Tume ya Maadili, Jaji Mstaafu
Salome Kaganda alisema kuwa uhakiki huo ni nguzo bora ya kuijenga jamii
ya Watanzania, hasa viongozi wa umma katika kuishi kwa kufuata misingi
ya uadilifu, iliyowekwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Alisema kwa kuwa idadi ya viongozi ni kubwa na kwamba tume hiyo itaanza
na uhakiki wa viongozi 60 wenye nyadhifa mbalimbali.
“Sisi
tunachokiomba kutoka kwao ni kutoa ushirikiano wa kutosha kwa maofisa
wetu wakati wa zoezi zima la uhakiki wa mali zao,” alisema Kaganda.
Alisema wananchi wanatakiwa kushirikiana na tume hiyo kutoa taarifa
zitakazowasaidia kugundua mali zilizofichwa, ambazo zinadhaniwa kuwa ni
za viongozi wa umma wanaoguswa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa
Umma. Aliwataka viongozi wanaohakikiwa kutokuwa na hofu kwa kuwa zoezi
hilo ni la kawaida.
“Hawa hawana tuhuma zozote ni utaratibu wa
kawaida tu,”alisema. Jaji mstaafu Kaganda aliliambia gazeti hili kuwa
si kosa kwa kiongozi yoyote wa Serikali kuwa na mali na kwamba kosa ni
mali hizo kupatikana kinyume na sheria. “Mbunge akiwa mfanyabiashara na
biashara yenyewe inafuata sheria hilo sio tatizo ila tukigundua mali
hizo au biashara inafanyika kinyume na sheria tunaweza kuwaeleza
Takukuru" alisema Kaganda.
Alisema kuwa kwa sasa uadilifu kwa
viongozi wa umma umeshuka hivyo zoezi kama hilo kwa kiasi kikubwa
linaweza kurudisha uadilifu huo. Katika hatua nyingine, Jaji Kaganda
alisema anafanya utafiti wa sheria ya kutenganisha biashara na uongozi.
“Nafanya utafiti kuhusu sheria hii ila kwa sasa ni mapema mno kueleza
nilipofikia,” alisema Kaganda.
No comments:
Post a Comment