KATIBU
WA SHIRIKA HILO BI DORO EZEKEL NTUMBO AKIWA KATIKA MAHOJIANO NA
MWANDISHI WA HABARI HIZI KATIKA OFISI YAO ILIYOPO KATIKA JENGO LA READ
CROSS
SHIRIKA la Unite Tanzania linalojihusisha na afya ya mtoto na sanaa,
limeandaa warsha kwa watendaji na wananchi katika kata ya Usagara
Jijijini Tanga yenye lengo la kuijengea uwezo jamii kuhusu masuala
yanayohusu haki mbalimbali za watoto ili waweze kuzitekeleza katika
familia.
Sanjari na hilo, shirika hilo litaendesha kampeni kwa kufanya shughuli
mbalimbali ikiwemo mabonanza ya watoto kwa kipindi cha miezi sita lengo
likiwa kuhakikisha inapambana na vitendo vinavyowakosesha raha na haki
watoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Bi Irene Mhando, akizungumza na
waandishi wa habari mjini hapa jana, alisema kuwa lengo la mradi huo
uliofadhiliwa na mtandao wa mashirika ya kiraia ya Foundation For Civil
Society, alisema kwa kipindi cha miezi sita watajikita katika kata
hiyo kuzungumzia kwa undani haki anazostahili kupata mtoto na vile vile
kutambua vipaji vyao.
Alitaja makundi ambayo watakutana nayo katika kipindi hicho kuwa ni
pamoja na watendaji wa mitaa, madiwani, polisi na wananchi wa kawaida
katika mitaa mbalimbali ya kata hiyo ambapo wanatarajia kwamba
itawajengea uwezo wa kutambua kwa nini jamii inapaswa kuwalea watoto
kwa mtizamo mpana.
"Shirika litaendesha mradi wa kampeni ya haki ya mtoto katika kata ya
usagara, kwa kipindi cha miezi sita watazungumza na wananchi,
watendaji, polisi na makundi mengine ya jamii ili kuhakikisha malengo
ya kuijengea uwezo jamii yanatimia ipasavyo na watoto wanaishi kama
watu wengine," alisema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake, Katibu wa shirika hilo, Bi Doro Ntumbo, akijibu suala
la kwanini wamechagua kata ya Usagara na siyo kata nyingine za Jiji
hilo, alisema kuwa kata hiyo imekuwa na matukio mengi ya unyanyasaji wa
mtoto hivyo kuendesha kampeni katika kipindi hicho kutasaidia kuongeza
uelewa kwa jamii na matukio hayo mwisho wa siku kupungua.
"Ukitazama malengo ya mradi huu, kuwaongezea uelewa jamii kuhusu sera
ya mtoto ya mwaka 2008, kubadilisha tabia za watu kuhusu namna
wanavyotakiwa kuwapa haki watoto...Sasa kata ya Usagara tumeonelea
tuanze nayo kwa vile masuala ya unyanyasaji yamekuwa yakikithiri hivyo
kufika kwetu tutasaidia maana pia tutaunda mabaraza ya watoto, hii
itasaidia kupunguza matukio ya ukiukwaji wa sheria za haki za mtoto,"
alisema Bi Ntumbo.
|
No comments:
Post a Comment