SERIKALI imesema mishahara ya walimu imekuwa ikipanda kwa kiasi kikubwa kuliko watumishi wengine nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Hawa
Ghasia alisema walimu wamekuwa wakipandishiwa mishahara kila mwaka na
kwamba kiwango cha upandishaji kinatofautiana na watumishi wa kada
nyingine.
Ghasia alisema katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2011, kiwango cha
upandaji wa mishahara kwa walimu kimekuwa kwa asilimia 12 na 12.4 kwa
mwaka, wakati kada nyingine mishahara iliongezeka kwa asilimia 5 hadi
12.6 kwa mwaka.
Majibu hayo yalitokana na swali la msingi la mbunge wa Kisarawe
Seleman Jafu (CCM) ambaye alitaka kujua mpango wa serikali kushughulikia
tatizo la mishahara kwa walimu ambayo imekuwa haipandi mara kwa mara na
kufanya walimu wawe na ugumu wa maisha.
Mbunge huyo alitaka kujua mikakati ya serikali katika kuwasaidia
walimu wanaoishi katika mazingira magumu ikiwa ni pamoja na kuwasaidia
vifaa vya usafiri.
Waziri alifafanua kuwa mwaka 2005, mwalimu wa daraja la tatu A’alianza
na mshahara wa Sh 74,570 ambapo kwa sasa mwalimu huyo anaanza na
mshahara wa sh 244,400 kwa mwezi.
Ghasia alisema walimu wa stashahada walianza na mshahara wa sh
108,800 na sasa wanaanza na sh 325,700 wakati walimu wa shahada walikuwa
wakianza na mshahara wa Sh 140,000 lakini kwa sasa wanaanza na mshahara
wa sh 449,200 kwa mwezi ambalo ni ongezeko la asimilia 235.14.
Kuhusu posho za walimu za kujikimu pamoja na usafiri kwa walimu
wanaokwenda katika mazingira magumu, alisema serikali imeboresha
mazingira yake ikiwa ni pamoja na kuwapatia mikopo kulingana na
mishahara yao.
No comments:
Post a Comment