JAJI Mkuu, Othman Chande amewataka Majaji Wafawidhi kupanga mikakati
mbalimbali ya kuboresha tija, kutathimini majukumu yao pamoja na
utendaji haki ulivyo sasa na wanakoelekea.
Alisema hayo juzi Bagamoyo mkoani Pwani wakati akifungua warsha ya
siku mbili kwa majaji wafawidhi ya kujadili mambo mbalimbali
wanayokabiliana nayo katika utendaji kazi wao wa kila siku ikiwamo
utendaji haki na uendeshaji mashauri.
Alisema katika ofisi nyingi tija imepungua na kuwataka nafasi hiyo
waliyopata waitumie kupanga mikakati ya kuongeza nguvu kuboresha tija,
kuweka malengo nani ana jukumu gani na nani atatoa taarifa za
utekelezaji wa majukumu.
“Lengo ni kuboresha utoaji wa haki … ni mara yetu ya kwanza kukutana
tangu uteuzi wangu na madhumuni ya kukutana ni kujua tunakokwenda na
mchango wa kila mmoja,” alisema Jaji Mkuu.
Alisema katika warsha hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Waziri wa
Katiba na Sheria, Celina Kombani wataweka vipaumbele vya Mahakama kwa
sababu fedha inayopatikana katika bajeti ya muhimili huo wa Dola
haitoshelezi.
Jaji Othmani alisema fungu pia lililopatikana kwa kesi za uchaguzi,
limechelewa kuwafikia hivyo wataangalia namna ya kuziendesha ziishe
kabla ya Mei mwaka huu muda ambao ndio wa kikomo wa kesi za uchaguzi
kisheria.
Imeandikwa na Regina Kumba habari leo
No comments:
Post a Comment