KUFUATIA mgomo wa madaktari unaoendelea nchini, Baraza la Mawaziri
limependekeza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na
Katibu mkuu wake, Blandina Nyoni, kuwajibishwa ili kurejesha imani ya
madaktari kurudi kwenye meza ya mazungumzo.
Katika kikao cha kazi
kilichofanyika juzi chini ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, inadaiwa
mawaziri hao walimweleza kuwa kutokana na hali ya mgomo wa madaktari
kuchafuka kupindukia, hakuna budi Waziri, naibu wake na katibu mkuu
wakawajibishwa.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, zilidai kuwa
suala la mgomo lilipofikia haliwezi likashughulikiwa kimyakimya, lazima
Serikali ikakubali kukaa na madaktari hao na kusikiliza malalamiko yao.
“Tumemweleza
Waziri Mkuu (Pinda) kwamba madaktari wanasema hawana imani na watu hawa
(waziri na katibu mkuu), hivyo hakuna njia ya kuwarejesha meza ya
mazungumzo hadi viongozi hawa wawe wameondolewa,” kilieleza chanzo chetu
cha uhakika.
Tayari, pendekezo hilo lilishatolewa na Kamati ya
Wabunge wa CCM, ambao walitaka Dk Mponda, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, Dk Lucy Nkya na Nyoni wajiuzulu au wakikataa wawajibishwe.
Pia,
mawaziri hao walikubaliana kusaidia kushawishi wabunge kupitisha
muswada wa mabadiliko ya katiba, ambao unapingwa na wabunge wa CCM, huku
wengine wakitaka wabunge wasidhibitiwe kutoa dukuduku lao.
Suala
la mgomo wa madaktari ambalo hivi sasa linashughulikiwa na Kamati ya
Bunge ya Huduma ya Jamii, halijapata ufumbuzi zaidi ya kuzidi kupanuka
kila siku na kuathiri huduma za afya.
Hata hivyo, wakati
akikabidhi suala la mgomo huo wiki iliyopita kwa Kamati ya Bunge ya
Huduma za Jamii, Naibu Spika, Job Ndugai, alionyesha wasiwasi na kauli
ya Serikali iliyotolewa na Dk Mponda bungeni, ambayo haikujumuisha
baadhi ya malalamiko ya madaktari.
“Lakini pia, katika submission
ya Mheshimiwa Waziri ya Kauli, ya madai yale yaliyodaiwa na Madaktari,
hata Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye tunamshukuru sana alipolishughulikia
suala hili alipoenda kule kukutana nao na wao hawakujitokeza, lilikuwepo
dai moja ambalo sijalisikia likizungumzwa hapa na ni vigumu
kuzungumziwa!” alisema Ndugai na kuongeza:
“Nalo ni kwamba, hawa
mabwana wanadai kwamba katika Wizara ya Afya kuna baadhi ya watendaji
wakuu wenye uwezo mdogo wa utendaji na wa kiuongozi, wasiowajibika
ipasavyo."
Na hawa watendaji wana kauli za kashfa na dharau kwa
Madaktari. Kwa kutegemea timu ile iliyoundwa na Serikali itakayoripoti
kulekule, itakuwa ni vigumu vilevile kupata ukweli wa upande huu wa
pili.”
No comments:
Post a Comment