Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
Helen Kijo-Bisimba (Katikati) akizungumza baada ya kuandamana jana
jijini Dar es Salaam kuishinikiza serikali iumalize mgomo wa madaktari
unaoendelea..Picha na Venance Nestory
MGOMO wa madaktari nchini umeingia katika sura mpya baada ya
wanaharakati kutoka asasi 15 za kiraia kufanya maandamano ya amani jana,
wakitokea maeneo mbalimbali kuelekea Ikulu jijini Dar es Salaam, kwa
lengo la kuwasilisha kilio chao kwa Rais Jakaya Kikwete. Hata hivyo,
wanaharakati hao hawakufanikisha lengo lao baada ya kujikuta
wakidhibitiwa na kusambaratishwa na polisi waliokuwa na silaha .
Pamoja
na kukwamishwa mkakati wao huo, wameipa Serikali saa 24 kuchukua
hatua za haraka kumaliza mgomo wa madaktari na kutishia kwamba kinyume
na hapo, watawahamasisha wananchi kuingia barabarani, kufanya
maandamano makubwa ya kuishinikiza Serikali kujiuzulu.
Kwa muda
wa wiki mbili sasa nchi imekuwa ikitikiswa na mgomo wa kihistoria wa
madaktari, ambao umeathiri kwa kiasi kikubwa utoaji huduma za afya
kwenye hospitali za rufaa ikiwamo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na
Taasisi ya Mifupa (MOI), ambako huduma zimesitishwa.
Katika
maandamano ya jana, wanaharakati hao walifunga Barabara za Ali Hassan
Mwinyi na Ocean Road kwa muda wa saa moja na kusababisha foleni kubwa ya
magari.
Maandamano hayo ya kushtukiza yaliyoanza saa 8:00
mchana, yalishirikisha asasi za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na Chama cha Waandishi wa
Habari Wanawake Tanzania (Tamwa).
Awali, wanarahakati hao walianza
kujikusanya taratibu kati ya eneo la Hoteli ya Palm Beach na Kituo cha
Polisi cha Oysterbay kilichopo jirani na daraja la Salender, huku
wengine wakilala barabarani.
Wakiwa na mabango yenye ujumbe
mbalimbali, wanaharakati hao wametaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk Haji Mponda na Naibu wake, Lucy Nkya na Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo, Blandina Nyoni wajiuzulu kwa kuwa wanafanya mzaha kwasababu Rais
na viongozi wengine hawatibiwi nchini wakiugua. Katika maandamano
hayo, waanaharakati hao pia walimlaani Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa
kuzuia kujadiliwa kwa suala hilo la dharura na kuongeza kwamba, kwa kuwa
tatizo linajulikana hakukuwa na haja ya kuunda kamati kutafuta chanzo.
Akizungumza
jana Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Ananilea Nkya alisisitiza kuwa
maandamano hayo ni ya wananchi. Alieleza kuwa ujumbe wao walioutuma kwa
Serikali usipotekelezwa, watawaambia wananchi waingie mtaani kudai haki
yao ya kupata matibabu.
“Tunatoa saa 24 kwa hatua za haraka
kuchukuliwa kuhusu mgomo wa madaktari la sivyo, kesho (leo) tutawaeleza
wananchi jinsi ya kuingia barabarani ili kuishinikiza Serikali
ijiuzulu,”alisema Nkya.
Mratibu wa Mtandao wa Asasi na Mashirika
yasiyo ya Kiserikali mkoani Arusha (Angonet), John Bayo, alisema mgomo
wa madaktari unapaswa kusitishwa sasa, kwa pande hizo mbili yaani
Serikali na madaktari, kukaa na kukubaliana.
“Lazima wakae,
watu wanakufa kwa kukosa matibabu, hapa hatafutwi mshindi bali haki na
maisha ya watu,”alisema Bayo. Bayo alisema katika kikao hicho kwa kuwa
madai ya madaktari yanafanana na wafanyakazi wengine wa umma katika
sekta nyingine, lazima kuwapo mpango wa kumaliza matatizo ya muda mfupi,
wa kati na mrefu.
Alisema haiwezekani sasa maisha ya watu
yanapotea, huku Bunge likiendelea kulumbana na Serikali ambayo nayo
inatoa matamshi ya vitisho kwa madaktari jambo ambalo, si jema.
Polisi
Hata
hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alisema
watu hao walikuwa wamekusanyika eneo la Palm Beach na kwamba, mkusanyiko
huo ulilenga kuwashawishi madaktari kuendelea kutoa huduma kwa
wagonjwa. “Lilikuwa kundi la watu takribani 150 na walikuwa wakitaka
kufanya maandamano kushinikiza madaktari kurudi kazini…, tulichokifanya
Polisi ni kuwataka watawanyike na walitii amri hiyo,” alisema
Shilogile.
Alisema kazi ya Jeshi hilo sio kutatua tatizo la
mgomo wa madaktari bali ni kuhakikisha usalama wa raia na kwamba, watu
hao wanatakiwa kuwasilisha madai yao sehemu husika.
Bungeni
Mgomo
huo jana ulirindima tena bungeni baada ya kipindi cha maswali na
majibu, kufuatia Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), akiwa ni
mbunge wa sita kutaka kujadiliwa hoja hiyo, aliomba kwa kutumia kanuni
ya 47, Bunge kujadili jambo hilo la dharura. “Naibu Spika, nchi yetu
inalo jambo la dharura sana. Hii ni karibu wiki ya pili Watanzania
wenzetu wanakufa mahospitalini. Hili limekuwa linaombwa hapa, naona tena
leo niombe Bunge lako lijadili suala la mgomo wa madaktari pamoja na
yote yanayoendelea. Wako watu wanaosema ni kuingilia mihimili mingine,
hapana, wanaokufa ni Watanzania ambao leo tuko hapa kuwawakilisha,”
alisema Serukamba na kuongeza:
“Litakuwa Bunge la ajabu sana na
tutaingia kwenye historia, Watanzania wanakufa tunasema hatuwezi
kuingilia mhimili mwingine. Ninaomba leo wabunge mniunge mkono ili
Spika uamue sasa tuanze kujadili suala hili gumu ambalo Watanzania
wanapoteza maisha yao.” Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) na kukubaliwa na wabunge wote. Lakini,
akitoa mwongozo wake, Naibu Spika Job Ndugai, alisema kwa mujibu wa
Ibara 63 ya Katiba ya Nchi, inatambua Bunge kama chombo kikuu cha
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambacho kitakuwa na madaraka ya niaba ya
wananchi kusimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote.
“Sasa
huwezi kusimamia jambo au huwezi kuwa mshauri mzuri kama hujapata
ukweli au hujapata kidogo undani wa mambo na ndiyo maana jambo hili
mliposimama mara ya kwanza, tena mkasimama tukashauri kwamba ni vizuri
liende katika Kamati yetu ili tutakapoishauri Serikali, tukiwashauri
hawa watumishi wa Serikali tuwe tunatoa ushauri ambao unatokana na watu
ambao wako informed,(wanauelewa)” alisema Ndugai. Madaktari Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari inayosimamia madai yao
Dk Stephen Ulimboka, alisema lawama zinazotokana na wagonjwa kwa kukosa
tiba zinapaswa kuelekezwa serikalini.
Dk Ulimboka alitoa kauli
hiyo jana alipotakiwa kuelezea hataua walizofikia kati yao na Serikali
kuhusu mgomo unaoendelea hivi sasa. “Tangu madaktari wagome leo (jana)
ni siku ya 16, Kamati iliyoundwa na Serikali kushughulikia suala hilo
haijawahi kutoa taarifa yoyote wala kukutana nasi, sisi tulishasema na
leo tunarudia, milango iko wazi kwa ajili ya majadiliano na
Serikali,”alifafanua Dk Ulimboka.
Alisema kimsingi, wao
wanaumizwa na hatua hizo, lakini, akadai msimamo wao unadai haki zao
sababu wamelenga kusaidia haki zao na za wananchi ambao wanakosa tiba
bora kutokana na Serikali kutozingatia umuhimu wa huduma za afya hapa
nchini.
Dk Ulimboka alisema kamati yake imeendelea na vikao
kujadili mambo mbalimbali huku ikisubiri tamko litakaloonyesha nia ya
Serikali ya kushughulikia madai yao.
Viongozi wa dini
Katibu
wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) Wilaya ya Arusha, Abbas
Mkindi maarufu kama Darwesh, alisema baraza hilo linapinga mgomo,
lakini pia linataka Serikali kukaa na madaktari.
“Lazima
Serika imalize mgogoro huu na pia ichunguze chanzo chake na hizi kauli
za watendaji wake, kwani hapa tunahisi kuna hujuma dhidi ya Serikali ya
Rais Kikwete, ”alisema Mkindi. Kwa upande wa Mchungaji Anicet Maganya
wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Arusha, alisema kubwa
katika madai ya madaktari ni maslahi, lakini wameonekana kukerwa na
majibu ya watendaji wa Serikali na vitisho. Mchungaji Maganya ambaye
ni Mkuu wa Idara Utetezi ya Kanisa hilo , alisema ingawa haungi mkono
mgomo unaoendelea anaamini kauli za viongozi wa Serikali akiwemo Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda kuwatisha madaktari ndio umefikisha hapa.
No comments:
Post a Comment