NJOMBE

NJOMBE

Sunday, February 5, 2012

Wabunge CCM wamgomea Rais

UHUSIANO kati ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete, unazidi kuzorota, kiasi cha kutishia nafasi ya kiongozi huyo mkuu wa nchi.
Baada ya juzi wabunge wa CCM kumshambulia na hata kutishia kupiga kura ya kutokuwa na imani naye kwa madai kuwa amewageuka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Spika, Anne Makinda, kuhusu posho mpya za wabunge, jana wabunge hao katika mkutano wao wa ndani waliazimia kukataa ombi la Rais Kikwete kukutana nao mjini Dodoma.
Mbali ya kukataa kukutana naye, wabunge hao pia wameazimia kugomea marekebisho ya sheria ya Katiba yaliyopendekezwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kushirikiana na ujumbe wa Rais Kikwete.
Maazimio hayo yalipitishwa jana katika kikao cha ndani cha wabunge wa CCM, kilichofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini hapa.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya kikao hicho, vilisema kuwa wabunge hao wa CCM wamekataa kukutana na Rais Kikwete kwa madai kuwa hawaoni jambo la kujadiliana naye kwa sasa.
“Kikao chetu cha jana kilikuwa kifupi sana. Tuliambiwa rais anataka kuja kutuona, lakini tumekataa,” kilisema chanzo cha habari.
Wabunge hao wa CCM wamefikia hatua hiyo kwani kile walichopigania kufa na kupona hadi kuzusha tafrani bungeni baada ya wenzao wa CHADEMA kususia na kutoka nje, ndicho wanatakiwa kufuta na badala yake kuridhia mapendekezo ya CHADEMA.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya kikao hicho, vimethibitisha pasipo shaka kuwa wabunge wa CCM wameweka msimamo wa kutoridhia mabadiliko yaliyofanywa na Rais Kikwete wakati tayari alishasaini muswada huo na kuwa sheria.
Baadhi ya wabunge waliochangia hoja hiyo ni Christopher ole Sendeka, Betty Machangu, Ally Kessy Mohammed, Josephat Kandege na wengine ambao kwa nyakati tofauti, tena bila kumung’unya maneno, walisema hawako tayari kuridhia mabadiliko hayo.
Kwa mujibu wa habari hizo, wabunge hao walisema baada ya CHADEMA kususia muswada huo na kuondoka bungeni, wabunge wa CCM waliwazomea na kuwaona wajinga, hivyo hawawezi tena kurudi kwenye mjadala kupitisha mabadiliko yaliyotokana na mapendekezo ya CHADEMA ambayo awali yalionekana hayakubaliki.
Baada ya kupitisha muswaada huo, CCM iliwatuma wabunge kwenda majimboni kuwaeleza wananchi uzuri wa muswada huo. Jana Kessy alilhoji: “Leo nitaenda kuwaambia nini wananchi wangu?”
Mbunge huyo wa Nkasi aliikumbusha serikali kurejea matukio mawili wiki iliyopita ya wabunge wa CCM kuungana na wa upinzani kukwamisha miswada miwili ya mabadiliko ya sheria.
Miswada iliyokwamishwa ni pamoja na ule wa mabadiliko ya sheria ya ushuru wa bidhaa za maji ya chupa ambapo Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, alipendekeza kupunguza ushuru wa bidhaa hizo kutoka sh 67 hadi sh 12 kwa chupa moja ya maji.
Hata hivyo wabunge wa CCM na wa kambi ya upinzani, walikwamisha muswada huo kwa madai kuwa umelenga kuwanufaisha wazalishaji wa bidhaa hiyo badala ya watu wa chini.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, naye alikwamishwa na muswada wake wa mabadiliko ya sheria mbalimbali, ukiwamo muswada wa marekebisho ya sheria ya Bodi ya Mikopo, ambao wabunge waliukataa kwa madai kuwa una ubaguzi.
“Mkulo alikuja na muswada wake, tukaukataa, Mwanasheria Mkuu naye alikuja na muswada wake, tukaukataa, huu wa marekebisho ya sheria ya katiba ya mwaka 2011, tuliokwisha upitisha na Rais kuusaini, tutaukataa,” alisema Kessy huku wabunge wengi wa CCM wakimshangilia.
Kessy alienda mbali kwa kusema kuwa hata Rais Kikwete akija Dodoma na kutaka kuzungumza na wabunge, hawatakuwa tayari kufanya hivyo, kwani hawaoni kama kuna jambo zaidi la kujadiliana naye kuhusiana na mabadiliko ya Katiba.
Kupelekwa kwa mabadiliko hayo bungeni miezi miwili baada ya sheria kupitishwa na kabla ya kuanza kutumika, kumetokana na hoja nzito zilizowasilishwa na ujumbe wa CHADEMA kwenye mkutano wake na Rais Kikwete, Ikulu.
Mkutano kati ya Rais Kikwete na viongozi hao wa CHADEMA, ulitokana na hatua ya wabunge wa chama hicho kutoka bungeni Novemba 14 mwaka jana kupinga kile walichokiita kuburuzwa na serikali katika mchakato wa kupata katiba mpya.
CHADEMA ilisema hatua ya rais kuteua wajumbe wa tume hiyo, kutasababisha kupatikana kwa katiba isiyokidhi matakwa ya wengi kwa kuwa wajumbe wake watawajibika moja kwa moja kwa rais.
Katika mabadiliko ya sasa yaliyopewa jina la Sheria ya Mabadilko ya Katiba ya mwaka 2011 Na. 8 ya mwaka 2012, serikali imeridhia vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyama vya kitaaluma, asasi za kidini, kuteua wajumbe wa kuingia kwenye Tume ya Katiba.
Serikali imekubali kufanya mabadiliko katika kifungu cha 6 (1) cha sheria hiyo kwa kuondoa mamlaka ya uteuzi moja kwa moja kwa rais.
Kifungu cha 6 (1) cha sheria, sasa kinasema rais atateua wajumbe kutoka miongoni mwa majina atakayopelekewa na vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za kidini na vyama vya kitaaluma kuwa wajumbe wa Tume ya Katiba.
Aidha, serikali imeridhia matakwa ya CHADEMA ya kuongeza kifungu cha 17 (10), kinachoruhusu watu binafsi, taasisi za kidini na vyama vya hiari kutoa elimu ya uraia. Asasi hizo sasa zitakuwa zinaripoti kwa mkurugenzi wa halmashauri badala ya mkuu wa wilaya.
Vile vile serikali imeridhia kufutwa kwa kifungu ch 6 (5) (c) kilichokuwa kina waondolea sifa wajumbe wa tume, watu waliowahi kuhukumiwa kwa kutenda kosa au mtuhumiwa katika shauri lililoko mahakamani linalohusu shitaka la kukosa uaminifu au maadili.
Ibara nyingine ambayo imefanyiwa marekebisho kwa mujibu wa makubaliano kati ya Rais Kikwete na CHADEMA ni 6 (5) (a) ambako madiwani au viongozi wa vyama vya siasa wa ngazi zote waliokuwa wamezuiliwa kuwa wajumbe wa tume, sasa wameruhusiwa.
Jingine ambalo CHADEMA walipendekeza na serikali kuridhia ni kuhusu kamati ya nidhamu ya Tume ya Katiba.
Awali sheria hiyo ilikuwa kimya kuhusu kamati ya nidhamu, lakini sasa kimeongezwa na kitakuwa kinaongozwa na mtu mwenye hadhi ya ujaji wa Mahakama ya Rufaa, akishirikiana na wajumbe wa nne kutoka Tume ya Haki za Binadamu, Utawala Bora, Tume ya Maadili ya Umma, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS).

No comments:

Post a Comment