BARAZA la Mtihani la Taifa(Necta) limetangaza matokeo ya
mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa
asilimia 53.59 ya wanafunzi 426,314 waliofanya mtihani huo wamefaulu. Hata
hivyo, wakati asilimia hiyo ambayo ni sawa na wanafunzi 180,216
wakifurahia matokeo hayo, wenzao 3,301 wamefutiwa matokeo kutokana na
udanganyifu ikiwamo mfanano usio wa kawaida wa majibu. Akitangaza
matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk
Joyce Ndalichako alisema wasichana waliofaulu ni 90,885 sawa na asilimia
48.25 na wavulana ni 134,241 sawa na asilimia 57.51.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Marian Girls,
Roselye Tandau (16)
akishangilia jijini Dar es Salaaam
jana baada ya kutangazwa mshindi wa
pili katika mtihani
wa Kitaifa wa Kidato cha nne wa mwaka 2011.
“Mwaka
2010 watahiniwa waliofaulu walikuwa 223,085 sawa na asilimia 50.74,
hivyo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.63,” alifafanua Dk Ndalichako.
Wanafunzi 10 bora Dk Ndalichako aliwataja wanafunzi 10 bora kitaifa
kuwa ni Moses Andrew Swai kutoka shule ya Feza Boys, Rosalyn Tandau
kutoka Marian Girls, Mboni Mumba kutoka St Francis Girls na Sepiso
Mwamelo kutoka St Francis Girls. Wengine na shule zao kwenye mabano ni
Uwella Rubuga (Marian Girls), Hellen Mpanduji (St Mary’s Mazinde Juu),
Daniel Wallace Maugo (St Joseph Millennium), Benjamin Tilubuzya, (Thomas
More Machrina), Simon Mbangalukela (St. Joseph Millennium) na Nimrod
Rutatora (Feza Boys).
Wasichana 10 bora
Kwa upande wa
wasichana kumi bora, Dk Ndalichako aliwataja na shule walizotoka kwenye
mabano kuwa ni Rosalyn (Marian Girls), Mboni (St Francis Girls),
Sepiso Mwamelo (St Francis Girls), Uwella Rubuga (Marian Girls) na
Hellen Mpanduji (St Mary’s Mazinde Juu). Wengine ni Lisa Chille (St
Francis Girls Mbeya), Elizabeth Ng’imba (St Francis Girls Mbeya), Doris
Noah (Kandoto Sayansi Girls), Herieth Machunda (St Francis Girls
Mbeya) na Daisy Mugenyi (Kifungilo Girls Tanga).
Wavulana 10 bora
Wavulana
kumi waliofanya vizuri zaidi katika mtihani humo ni Moses Andrew Swai
(Feza Boys), Daniel Maugo (St Joseph Millennium), Benjamini Tilubuzya,
(Thomas More Machrina), Simon Mbangalukela (St. Joseph Millenium) na
Nimrod Rutatora (Feza Boys). Wengine ni Simon Mnyele (Feza Boys),
Paschal Madukwa (Nyegezi Seminary), Henry Stanlay (St Joseph Millenium),
Fransisco Kibasa (Mzumbe) na Tumain Charles (Iliboru).
Shule 10 bora
Matokeo
hayo yanaonyesha shule kumi bora zenye zaidi ya watahiniwa 40 kuwa ni
St. Francis Girls ya Mbeya, Feza Boys, St Joseph Millenium, Marian
Girls, Don Bosco Seminary, Kasima Seminary, St. Mary’s Mazinde Juu,
Canossa, Mzumbe na Kihaba.
Matokeo hayo yanaonyesha pia shule
10 bora zenye watahiniwa chini ya 40 kuwa ni Thomas More Machrina, Feza
Girls, Dungunyi Seminary, Maua Seminary, Rubya Seminary, St Joseph
Kilocha Seminary, Sengerema Seminary, Lumumba, Queen of Apostles-
Ushirombo na Bihawana Junior Seminary.
Shule 10 za mwisho
Shule kumi za mwisho zenye watahiniwa zaidi ya 40 ni Bwebwera, Pande
Daraja, Mufindi, Zirai, Kasokala, Tongoni, Mofu, Mziwa, Maneromango na
Kibuta. Na shule kumi za mwisho zenye watahiniwa chini ya 40 ni
Ndongosi, St Luke, Igingwa, Kining’inila, Ndaoya, Kilangali,
Kikulyungu, Usunga, Mto bubu day na Miguruwe. Waliofutiwa matokeo Dk
Ndalichako alifafanua zaidi kuwa watahiniwa 3,301 waliobainika kufanya
udanganyifu wamefutiwa matokeo na hawataruhusiwa kufanya mtihani wowote
wa Necta kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.
Dk Ndalichako
alisema kati yao watahiniwa waliofanya mtihani huo walikuwa 426,314,
sawa na asilimia 94.67 ya watahiniwa wote waliosajiliwa. “Mwaka 2010
watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 458,114 hivyo, idadi ya watahiniwa
imepungua kwa watahiniwa 7,790 sawa na asilimia 1.70,” alisema Dk
Ndalichako. Alisema mwaka jana, watahiniwa wa shule waliosajiliwa
walikuwa 349,39 na watahiniwa huku wa kujitegemea wakiwa ni 100,934.
Akifafanua zaidi juu ya matokeo hayo, Mtendaji Mkuu huyo wa Necta
alisema watahiniwa 450,324 walisajiliwa kufanya mtihani huo ambao
wasichana ni 201,799, sawa na asilimia 44.81 na wavulana 248,525, sawa
na asilimia 55.19. Alisema jumla ya watahiniwa wa shule 180,216 sawa na
asilimia 53.59 ya waliofanya mtihani wa kidato cha nne wamefaulu, kati
yao wasichana wakiwa 69,913 na wavulana 110,303.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, waliofaulu ni 44,910 wasichana wakiwa 20,972 na wavulana 23,938.
Waliofutiwa mitihani
Dk
Ndalichako alisema Necta imefuta matokeo ya watahiniwa 3,03
waliobainika kufanya udanganyifu kati yao, watahiniwa wa shule ni 3,301
na wawili wakiwa wa maarifa (QT). Akifafanua zaidi juu ya udanganyifu
huo alisema , 182 walikamatwa na wasimamizi wakiwa na makaratasi (notes)
sita walikamatwa na simu, watatu walikuwa wakifanyiwa mtihani na watu
wengine, wanne walisajiliwa kufanya mtihani kwa majina ya watu wengine.
Dk
Ndalichako aliongeza kwamba, pia watahiniwa 2,896 karatasi zao za
majibu zilikuwa na mfanano usio wa kawaida, 155 karatasi zao za majibu
zilikuwa na miandiko zaidi ya mmoja, 14 kubadilishana karatasi katika
chumba cha mtihani, 18 kukamatwa na karatasi za majibu zaidi ya moja, 25
wakiwa na mfanano usio wa kawaida wa majibu , kuwa na vikaratasi ama
kubadilishana vikaratasi. “Mtu mmoja unakuta mitihani yake ya majibu
ina miandiko zaidi ya 10, na jeshi la polisi ndilo lililothibitisha kuwa
miandiko ya wanafunzi hawa ilikuwa inatofautiana. Alisema pia kuwa,
baraza hilo limefuta matokeo ya watahiniwa nane walioandika matusi ya
nguoni kwenye karatasi zao za majibu. “Kitendo cha kuandika matusi
kwenye karatasi za majibu kinaonyesha utovu wa nidhamu, hivyo pamoja na
kuwafutia matokeo ufuatiliaji zaidi unaendelea ili kuona hatua za
kuwachukulia,” alisema Dk Ndalichako.
Pia alitoa onyo kali kwa
vituo vilivyohusika na udanganyifu huo, huku akisema kwa vilivyobaika
vitaandikiwa barua ya kutaka vijieleze kwa nini visifutiwe matokeo. Dk
Ndalichako akielezea zaidi juu ya hali hiyo, alisema baadhi ya
watahiniwa waliandika nyimbo za kizazi kipya (Bongo fleva) kwenye
karatasi zao za majibu huku wengine wakichora michoro isiyo eleweka na
wachezaji wa mpira. “Mwingine aliandika bongo fleva, ngoja niwasomee
‘wasahihishaji msinisamehe..., acha utani na girl wangu, najukuja home
nakukuta.. nikifeli mtihani naendelea na fani ya muziki,” Dk Ndalichako
alisoma moja ya karatasi za majibu za watahiniwa hao huku akiruka baadhi
ya maeneo akisema ameandika matusi yasiyoweza kusomeka.
Ubora wa ufaulu kwa jinsi
Dk
Ndalichako alisema ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata
watahiniwa wa shule unaonyesha kuwa, jumla ya watahiniwa 33,577 sawa na
asilimia 9.98 wamefaulu katika daraja la kwanza mpaka la tatu.
“Wasichana
waliofaulu katika daraja la kwanza mpaka la tatu ni 10,313 sawa na
asilimia 7.13 na wavulana ni 23,267, sawa na asilimia 12.13,” alisema Dk
Ndalichako. Aliongeza kwamba, waliopata daraja la nne ni 146,639 sawa
na asilimia 43.60 ambao wavulana ni 87,039 sawa na asilimia 45.40 na
wasichana 59,600, sawa na asilimia 41.22. Dk Ndalichoka aliongeza
kwamba, waliofeli ni 0156,089 sawa na asilimia 46.41, kati yao
wavulana wakiwa 81,418 sawa na asilimia 42.47 na wasichana wakiwa
74,667, sawa na asilimia 51.64.
No comments:
Post a Comment