KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema hana mpango wa
kugombea ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki.Juzi, Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe alikaririwa akisema kama Dk Slaa ataamua kuwania
ubunge katika jimbo hilo, chama kitaheshimu uamuzi wake akisema: “Katika
suala la kugombea, utashi binafsi ni jambo la msingi... kama Dk Slaa
ataamua kugombea ubunge Arumeru Mashariki, tutaheshimu uamuzi wake.”
Mbowe
alisema Dk Slaa amekuwa akiombwa kugombea ubunge katika maeneo mengi
ikiwemo Igunga na chama hakikuwahi kumlazimisha kwani jambo la kwanza
ilibidi mwenyewe aonyeshe utashi binafsi wa kutaka kuwania kiti
hicho.“Dk Slaa aliwahi kuombwa akagombee Igunga lakini hakwenda. Hii ni
kwa sababu anakubalika karibu kote nchini, hivyo kama atakuwa na utashi
binafsi kwanza, nadhani taratibu za chama zitatumika tu kufikia uamuzi,”
alifafanua.
Lakini akizungumza katika mahojiano maalumu na Kituo
cha Televisheni cha Mlimani jana, Dk Slaa alisema hafikirii kuwania
ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa kuwa kazi yake ni kukijenga
chama kitaifa ili kiweze kupata wabunge wengi.
Alisema hawezi
kujifunga kwenye jimbo moja wakati alishasema kuwa kazi yake ni kutetea
wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwa kukijenga chama chake.“Siwezi
kujifungia kwenye jimbo moja, nilishasema kazi yangu ni kukijenga chama
ili kiweze kupata wabunge wengi,” alisema Dk Slaa.
Wakati Dk Slaa
akitoa msimamo wake huo, baadhi ya makada waliokwishajitokeza na
kuonyesha nia ya kugombea jimbo hilo wamesema kama ataamua wako tayari
kumpisha.
Mmoja wa makada hao ni aliyepeperusha bendera ya
Chadema katika uchaguzi wa mwaka 2010 jimboni humo, Joshua Nasari ambaye
alitoa upinzani mkali kwa mgombea wa CCM, marehemu Jeremiah Sumari.
Tangu
juzi kumekuwa na mjadala katika mitandao ya kijamii huku baadhi
wakimtaka Dk Slaa akagombee ubunge Arumeru Mashariki kuziba pengo la
marehemu Sumari lakini, wengine wanapinga na kumtaka aendelee kubaki na
nafasi yake ya katibu mkuu wa chama kwa lengo la kukijenga.
Joshua Nasari
Kwa
upande wake, Nasari (26) ambaye ana mtaji mkubwa wa kura alioupata
katika uchaguzi wa mwaka 2010, alisema yupo tayari kufanya mazungumzo na
viongozi wa juu ya chama chake juu ya kumpisha Dk Slaa kuwania ubunge
katika jimbo hilo kama akihitaji.
Nasari ambaye amerejea hivi
karibuni mjini Arusha akitokea Marekani, leo anatarajiwa kuchukua fomu
rasmi ili kuwania nafasi hiyo kupitia Chadema.“Nimesikia maoni kupitia
mitandao na wadau wakimuomba Dk Slaa kugombea, hili ni jambo jema kwetu
kwani wananchi wanajua jimbo hili tunashinda Chadema na kama Dk (Slaa)
akitaka kugombea demokrasia ya chama chetu itafanya kazi, kwani kikubwa
tunataka ushindi,” alisema Nasari.
CCM walalamika
Baadhi ya
wanachama wa CCM, wamelalamikia gharama kubwa za fomu za chama hicho
zinazotolewa kwa makada wake wanaotaka kuwania ubunge katika jimbo
hilo.Wanachama Julias Nangisa na Lameck Kanangira walisema jana kwamba
gharama ya Sh300,000 wanayotakiwa kulipa ni kubwa mno kwa mwanachama wa
masikini wa CCM.
“Gharama hizi kubwa zinaonyesha kama mtu huna
kipato cha kutosha huwezi kuwa kiongozi ndani ya CCM kwani fomu
tunatakiwa kulipa 100,000 na mchango wa chama 200,000 kabla ya
kukabidhiwa fomu,” alisema Nangisa na kuungwa mkono na mwenzake.
Alipoulizwa
kuhusu malalamiko hayo, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Arumeru, Edson
Lihweuli alisema: “Kwanza hao wanaolalamika walipaswa kuja kwangu na
siyo kwenye vyombo vya habari, gharama ya fomu ni Sh100,000 na mchango
ni Sh200,000 na malipo haya ni halali.”
Kwa upande wake Chadema kinatoa fomu zake kwa wagombea kwa Sh50,000 bila ya gharama nyingine za ziada.
Mwenyekiti
wa Baraza la Vijana wa Chadema Mkoa wa Arusha, Ephata Nanyaro alisema
japokuwa chama hicho ni kichanga na bado kinahitaji michango ya
wanachama, wameona gharama ya fomu ikiwa ni Sh50,000 inawafanya
wanachama wengi hasa wa hali ya chini kujitokeza kugombea.
Hadi
sasa wanachama tisa wa vyama vya CCM na Chadema wamejitokeza kuchukua
fomu kupitia vyama vyao hadi jana mchana. Wagombea wa CCM ni sita na
Chadema watatu.
Takukuru waweka CCM
Maofisa wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Arusha, wameweka kambi
katika Ofisi za CCM Wilaya ya Arumeru ili kuchunguza mwenendo wa utoaji
fomu na pia vitendo vya rushwa.
No comments:
Post a Comment