NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe anatarajia kuondoka nchini
wakati wowote kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu.
Dk
Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi ambayo Oktoba 9 mwaka
jana, alilazimika kupelekwa katika Hospitali ya Appolo nchini India kwa
matibabu zaidi.
Jana, vyanzo vya karibu na Dk Mwakyembe
vilidokeza gazeti hili kwamba naibu Waziri huyo na Mbunge wa Kyela
anatarajiwa kurudi Appolo, kwa ajili ya kuangalia kama matibabu
aliyopata yameweza kumsaidia kwa kiwango gani.
Vyanzo hivyo
vilivyo karibu na Dk Mwakyembe, vilifafanua kwamba anachokwenda kufanya
India ni "Uchunguzi tu wa kawaida kuona maendeleo ya matibabu."
"Atarudi
katika uangalizi wa kawaida, kwasababu amekuwa akipata matibabu hivyo
lazima achunguzwe kuona dawa alizokuwa akitumia zimemsaidia kwa kiwango
gani," alisema.
Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, hivi
karibuni alijitokeza na kutoa kauli nzito kuhusu chanzo cha maradhi
yanayomsibu, huku Serikali ikiendelea kukaa kimya hata baada ya
washirika wake wa karibu kusisitiza kwamba alipewa sumu.
Itakumbukwa
kwamba, mwaka jana, Dk Mwakyembe akiwa na hali mbaya alipelekwa katika
Hospitali ya Appolo, nchini India kwa matibabu baada ya kuugua maradhi
yaliyosababisha ngozi yake kuharibika. Tangu arejee mwanzoni mwa mwezi
uliopita alikuwa hajaonekana hadharani, mbali na kutoa tamko kwamba afya
yake ilikuwa inaendelea vizuri.
Hata hivyo, muda wote huo
aliokuwa nchini India na baada ya kurudi nchini, mazungumzo ya watu
maofisini, nyumbani, mitaani na vijiweni yalitawaliwa na utata wa suala
la afya ya Dk Mwakyembe, huku uvumi, tetesi na minong’ono kwamba maradhi
yake yalisababishwa na hujuma za kisiasa vikitawala hisia za wananchi.
Hisia
hizo zilikuzwa na kauli ya mmoja wa washirika wake kisiasa, Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta ambaye alimtembelea
hospitalini nchini India na baadaye kutoboa hadharani kwamba Dk
Mwakyembe alikuwa amelishwa sumu kutokana na msimamo wake dhidi ya
mafisadi.
No comments:
Post a Comment