UTAFITI
wa hivi karibuni uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Johns
Hopkins nchini Marekani, umegundua kuwa matumizi ya dawa za kurefusha
maisha (ARV) yanaweza kuwafanya waathirika wa Virusi vya Ukimwi (VVU)
kukutana kimwili na wapenzi wao bila kondomu, pasi kuwapa maambukizi.
Wakati
wataalamu hao wakifikia hatua hiyo muhimu katika kupata jibu la janga
hilo lililoitesa dunia kwa miongo kadhaa sasa, kuna taarifa njema pia za
kugunduliwa kwa chanjo mpya ya Ukimwi.
Kwa upande wa utafiti wa
ARV walioufanyiwa majaribio kwenye sehemu mbalimbali za dunia, umebaini
kuwa mtu ambaye anatumia dawa za kurefusha maisha, anaweza kufanya tendo
la ndoa bila ya kutumia kondomu na mtu ambaye hana Ukimwi na
asimwambukize kwa asilimia 95.
Mkuu wa Mtandao wa Maabara za
Kuchunguza VVU katika chuo hicho, Profesa Susan Eshleman, alisema kwenye
ripoti ya ugunduzi huo, wamebaini dawa za kurefusha maisha kwa
waathirika wa HIV, sasa zinaweza kutumika kama sehemu ya kuzuia
maambukizi.
Profesa Eshleman alisema kwamba muathirika wa VVU
anayetumia ARV kikamilifu anaweza kujamiiana na mtu ambaye hana virusi
bila kondomu na asimwambukize.
“Huu ni ugunduzi wa kustajabisha,”
alisema Profesa Eshleman akifafanua: “Matokea haya yameleta mapambazuko
mapya katika sayansi ya kuzuia maambukizi na inawaweka watafiti kwenye
mazingira mazuri zaidi ya kupata suluhisho la kukabiliana na maradhi
haya.”
Walivyogundua njia
Profesa Eshleman
anasema utafiti huo walioupa jina la HPTN 052 walifanya kupitia maeneo
mbalimbali ya dunia hasa yenye kasi kubwa ya maambukizi kama vile
Afrika, Brazili, India na Thailand.
Kwenye ripoti hiyo ambayo pia
ilichapishwa kwenye jarida maarufu la kisayansi linaloitwa Science,
watafiti hao wanasema kwamba mtu anapotumia ARV, hufikia wakati fulani
wingi wa virusi mwilini hupotea kiasi kwamba anakuwa karibu sawa na yule
ambaye hajaambukizwa.
“Jambo la msingi katika utafiti huu ni
kwamba dawa hizi za kurefusha maisha zinapotumiwa kikamilifu, hupunguza
mzigo wa virusi mwilini kwa zaidi ya mara 200. Ni sawa na kusema
inapunguza hadi kufikia karibu na sifuri,” inaeleza ripoti hiyo.
Ni
katika mazingira hayo, ripoti hiyo inasema kuwa damu ya muathirika
inakuwa haina virusi na hivyo uwezekano wa kumuambukiza mpenzi wake
unakuwa haupo.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa ARV inafanya kazi mbili,
kwanza kurefusha maisha ya muathirika kwa kupunguza virusi mwilini na
pili ni kumkinga asiambukize wengine.
Sifa nyingine ya ARV,
anasema ni kwamba inapunguza uwezekano wa waathirika kupata ugonjwa wa
Kifua Kikuu (TB) kutokana na kiwango cha kinga za mwili kupanda.
Onyo la utafiti
Pamoja
na kwamba njia hii imeonekana kuwa ni nzuri kwa ajili ya kuzuia
maambukizi, wataalamu hao wanasema ni hatari pale itakapotumika vibaya.
Hatari
wanayoizungumzia ni kwa muathirika iwapo atatembea na mpenzi ambaye ni
muathirika, lakini akawa hajatumia ARV au ametumia, lakini siyo kwa
kiwango ambacho VVU vimepunguzwa hadi kufikia karibu na sifuri.
Watalaamu
hao wanasema iwapo muathirika atapata maambukizo mapya, atajiweka
katika hatari ya kupata usugu kwa aina ya ARV anayotumia.
Ili
kuwaweka katika mazingira salama, wataalamu hao wamewashauri waathirika
wanaotumia ARV kutobweteka na badala yake kuendelea kutegemea kondomu
kama moja ya njia za kuzuia maambukizo mapya na kuimarika kiafya.
Wataalamu wazungumzia utafiti huo
Wataalamu
na watafiti mbalimbali wameelezea utafiti huo kuwa ni mafanikio mazuri
katika kurahisisha njia ya chanjo katika kutoa kinga kwa waathirika na
wale ambao hawajaambukizwa.
Kwa sasa zipo aina nane za chanjo za
Ukimwi duniani ambazo wataalamu wapo kwenye hatua mbalimbali za
majaribio na wamekuwa wakizielezea kuwa zina matumaini.
Mkuu wa
Mambo ya Afya wa Serikali ya Marekani, Profesa Anthony Fauci ambaye pia
ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio
(NIAID), aliuelezea ugunduzi huo kuwa ni wakushangaza.
Wataalamu
wengine pia wakauelezea kuwa mtu anaweza kuuchukulia kama ni utani,
lakini ni jambo ambalo litaleta mapinduzi makubwa ya kukabiliana na VVU.
Profesa
Eshleman alisema utafiti wao utafungua urahisi wa njia ya wanasayansi
wanaoendelea na tafiti nyingine kuwa katika mazingira mazuri ya kutatua
tatizo hilo.
Profesa Eshleman anasema mkakati walio nao kwa sasa ni
kufanya uchunguzi zaidi wa njia hiyo katika ngazi ya kijamii na
kimataifa.
Alisema anaamini kwamba njia hiyo itakuwa na matokeo mazuri katika ngazi hiyo kabla haijathibitishwa rasmi kutumika kimataifa.
A.Kusini waiwekea mkakati
Serikali
ya Afrika Kusini tayari imeweka mkakati wa kutumia njia hiyo kuliokoa
taifa hilo lenye kasi kubwa ya maambukizo kuliko mengine duniani.
Mmoja
wa wataalamu wa afya wa nchi hiyo, Dk Brian Williams, anasema tayari
wamefanya tathmini na kuona baada ya miaka mitano watakuwa wamefanikiwa
kuyakabili maradhi hayo.Dk Willams, anasema Afrika Kusini ina waathirika
milioni sita na kwamba ni asilimia 30 tu wanaopatiwa tiba ya ARV.
“Ili
kuwagharimia waathirika hao itabidi tutumia Dola za Marekani kati ya
milioni mbili hadi tatu (Sh 3.2 trilioni hadi 4.8 trilioni) kununua dawa
za ARV kwa mwaka,” alisema Dk Williams.
Kutokana na uzoefu wake,
Williams alisema utafiti huo utasaidia waathirika kuwa katika mazingira
mazuri ya kupatiwa chanjo ambayo ipo mbioni kupatikana.
Tanzania ipo pazuri
Tanzania
ni moja ya nchi ambazo matumizi ya ARV kwa waathirika ni makubwa
kutokana na mpango wa Serikali wa kuwapatia dawa hizo bure kote nchini.
Tangu
Rais Jakaya Kikwete atangaze mpango wa kupima kwa hiari miaka michache
baada ya kuingia madarakani, aliwahakikishia wale wote watakaojikuta
wameambukizwa, watapatiwa dawa za kurefusha maisha bure.
Mwananchi
Jumapili lilipowasiliana kwa njia ya simu na Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, Dk Hadji Mponda, alisema asingeweza kulizungumzia suala hilo
kwa kuwa hakuwa ofisini na asingependa kuzungumza kwa njia ya simu.
Mkuu
wa Utawala wa Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Binadamu Hospitali ya KCMC
(KCRI), Lucy Shara alilimbia gazeti hili kwamba suala la matumizi ya ARV
nchini imekuwa ikifanyika ipasavyo kwa wale wanaojitokeza kwa hiari.
Shara
alikiri kuwa wataalamu nchini wamekuwa kwenye tafiti mbalimbali za VVU
na kwamba hata suala la ufanisi wa dawa za ARV wamekuwa wakiujadili mara
kwa mara kupitia vikao na semina mbalimbali.
Lakini akasema suala la utafiti huo wa Marekani lilijadiliwa kwenye mkutano uliofanyika Jijini Dar es Salaam karibuni.
“Juzi
tulikuwa kwenye semina hapo Dar es Salaam. Wasiliana na wataalamu wetu
wa pale Muhimbili (Hospitali ya Taifa) wanaweza wakakueleza jambo hili
kwa uzuri zaidi,” alisema Shara.
Juhudi za kuwapata wataalamu wa
Utafiti wa Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Muhimbili (MUHAS) kulieleza
suala hili hazikufanikiwa kutokana na tatizo la kimawasiliano.
Chanjo mpya yagundulika
Utafiti
wa chanjo Ukimwi uliosimamiwa na Chuo Kikuu cha Tiba cha Harvard nchini
Marekani na kusimamiwa na Profesa Dan Barouch wa chuo unaelezewa kuwa
na mafanikio makubwa katika kukabiliana na ugonjwa wa Ukimwi ambao mpaka
sasa hauna chanjo wala tiba ambayo imetambuliwa rasmi kimataifa.
Taarifa
iliyotolewa NIAID kwa gazeti hili wiki iliyopita, inaeleza kuwa utafiti
huo uliofanywa Profesa Nelson Michael wa Jeshi la Marekani,
akishirikiana na Profesa Jaap Goudsmit, Dk Vanessa Hirsch na Ilnour
Ourmanov, una sema mafanikio ya utafiti huo yanawapa matumaini ya kupata
chanjo madhubuti.
Walisema kwenye ripoti hiyo kuwa katika
majaribio kadhaa waliyofanya, chanjo hiyo iliweza kumsaidia Nyani kuwa
na chembechembe kinga ambazo zina uwezo wa kumkinga asiweze kuambukizwa
VVU.
Utafiti huo uliotangazwa Januri 4, mwaka huu unaeleza kuwa
kinachofanyika kwa sasa ni kuendelea na utafiti huo katika hatua ya
majaribio kwa binadamu.Kwa sasa chanjo hiyo walisema ipo kwenye hatua ya
awali ya majaribio ya usalama wa dawa kabla ya kuingia kwenye majaribio
ya uwezo wa dawa kwenye mwili wa bianadamu.
Utafiti ulivyofanyika
Walisema
walimpa nyani chanjo hiyo na baada ya muda alitengeneza chembechembe
kinga za aina ya protini na walipojaribu kumuambukiza VVU, virusi
walidhibitiwa na kushindwa kushambulia seli nyeupe za binadamu ama kwa
jina la kitaalamu CD4, ambazo ni kinga muhimu dhidi ya maradhi mengine.
Kwa
kawaida VVU hushambulia seli hizi nyeupe na kuzifanya makoloni ya
kuwawezesha kuzaliana na kuongezeka mara dufu mwilini hivyo kujenga
mazingira ya mtu kuugua Ukimwi.
Matokeo ya utafiti huo
yanafikisha idadi ya aina nane za chanjo dhidi ya VVU ambazo zimo kwenye
majaribio katika hatua mbalimbali duniani.
Mojawapo ya chanjo
hizo amabazo zipo kwenye hatua mbalimbali za majaribio, ipo ile ambayo
mafanikio makubwa yalichangiwa na wanasayansi wa hapa nchini waliokuwa
wanafanya kazi katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, mkoani Kilimanjaro.
Wanasayansi
wa Tanzania waligundua kwamba baadhi ya watu walioathirika na Virusi
vya Ukimwi (VVU), kwa muda fulani wanajijengea wenyewe kinga inayoweza
kudhibiti virusi hivyo na kuwa na afya njema bila kuwa na haja ya
kutumia dawa za ARV.
Wataalamu hao wa KCMC mjini Moshi
walifanikisha utafiti huo wa mwaka 2006 na 2010 na mwishoni mwa mwaka
jana wakaliambia Mwananchi Jumapili kuhusu ugunduzi huo.
Kiongozi
wa Ushirikiano wa kiutafiti kati ya KCMC na Chuo Kikuu cha Afya cha
Duke cha nchini Marekani, Dk Elizabeth Reddy aliliambia gazeti hili kuwa
matokeo hayo yatawezesha kutengeneza chanjo itakayowezesha watu wote
kuwa na kinga hizo, hivyo kutoathirika na VVU.
Alisema jambo la
msingi katika utafiti huo ni kugundulika kwa VVU kuwa wana gamba lenye
protini iliyochanganyika na sukari, ambayo huvifanya kushindwa
kutambuliwa na kinga za kawaida za mwili wa binadamu.
Lakini,
Dk Reddy alisema kuwa katika ugunduzi wao, wamebaini aina ya kinga za
mwili ambazo hutambua virusi kupitia aina hiyo ya sukari kwenye gamba la
nje la VVU na kuvishambulia hadi kuviua.
Alisema kuwa utafiti
huo ulifanyika katika maabara ya KCMC kwa ushirikiano wa timu ya
wataalamu wa afya wa Tanzania pamoja na wa Marekani.
Alibainisha
kuwa utafiti huo ulihusisha Watanzania kadhaa walioambukizwa VVU hapa
nchini, lakini wamekuwa wakiishi bila kuathirika. Dk Reddy alisema kuwa
utafiti huo umefanyika maeneo mengi duniani, lakini kituo cha KCMC
ndicho kilichotoa mwanga mkubwa zaidi ambao hatua zake za mwisho
zilithibitishwa na wataalamu waliobobea nchini Marekani.
Kiongozi
huyo wa utafiti, alisema kuwa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa
inayosimamiwa na Mfuko wa Good Samaritani (GSF) ambao ndio pia
unaosimamia taasisi nyingine kama vile Chuo Kikuu cha Afya cha Tumaini
na Hospitali ya KCMC, ndiyo inayopaswa kupewa shukurani kwa matokeo
hayo.
Dk Reddy anaamini kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo, chanjo kadhaa zitakuwa zimethibitishwa.
No comments:
Post a Comment