KINGUNGE ADAIWA KUPINGA, ASEMA HAYALENGI KUBORESHA MFUMO WA CHAMA
SIKU
moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitisha mabadiliko ya Katiba
ya mwaka 1977 juu ya namna ya kuwapata wajumbe wa Halmashauri Kuu
(NEC), imeelezwa kuwa mabadiliko hayo yanatarajiwa kuwa kitanzi kwa
watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho tawala kuelekea Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2015.
Juzi, Nec ya CCM ilibariki mabadiliko muhimu ya
katiba ya chama hicho kuelekea uchaguzi wa ndani ambayo ni pamoja na
kuanzisha utaratibu ambao wajumbe wa NEC waliokuwa wanatoka mikoani,
sasa watakuwa wanachaguliwa kutoka wilayani na wabunge, wawakilishi na
madiwani sasa hawataruhusiwa kushika nyadhifa za chama.
Katika
marekebisho hayo, viongozi wakuu wastaafu wakiwamo Marais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Marais wa Zanzibar na makamu wenyeviti wa chama
hicho, wameundiwa Baraza la Ushauri na sasa hawatakuwa wajumbe wa NEC.
Hata
hivyo, uamuzi huo umepingwa vikali na baadhi ya wajumbe ambao walisema
marekebisho hayo hayana tija zaidi ya kutaka kudhoofisha upande mmoja
ambao uko kwenye harakati za urais mwaka 2015 na kuutaja kwamba, ni
genge la watuhumiwa wa ufisadi.
“Wamejaribu kuondoa wazee
wastaafu ili Kamati Kuu isiwe na watu ‘strong’, lakini yote hayo
yanalenga kwa mtu siyo mfumo. Chama kinatakiwa kufanya marekebisho yake
kwa mfumo siyo mtu... ngoja twende tutaona itakavyokuwa,” alisema mjumbe
mmoja wa NEC ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Mjumbe
mwingine ambaye pia hakutaja kutambushwa jina lake gazetini alisema
uamuzi huo wa kurejesha nafasi hizo wilayani, unalenga kuwazuia baadhi
ya watu wasiingie katika vikao hivyo vya uamuzi na kuwazuia watuhumiwa
wa ufisadi kuweka watu wao katika wilaya zote nchini hata kama wana
fedha.
Alisema hata kama watuhumiwa wa ufisadi wana fedha nyingi,
itakuwa vigumu kwao kuweza kupandikiza watu wao katika wilaya zote
nchini.
“Kwa hiyo sasa hivi angalau kutakuwa na mkakati wa
kuhakikisha mafisadi hawaweki watu wao wengi wilayani. Kwani itakuwa
vigumu kumudu kuweka wajumbe wa NEC wilaya zote nchini, lakini pia, wao
wenyewe itawawia vigumu kupenya.”
Mwishoni mwa mwaka jana, mpango
wa kujivua gamba ndani ya CCM uligonga ukuta katika kikao cha NEC hatua
ambayo ilimfanya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kutumia busara na
kurejesha utekelezaji wa mpango huo kwenye Kamati Kuu (CC) kwa
utekelezaji.
Kingunge apinga
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani
ya kikao hicho zilieleza kuwa, kada mkongwe wa chama hicho, Kingunge
Ngombale-Mwiru, ndiye mjumbe pekee aliyepinga marekebisho hayo, huku
akiituhumu sekretarieti kwa kukiuka katiba ya chama hicho.
Kingunge
anadaiwa kuwatuhumu Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama kwa kuvunja
katiba hiyo kutokana na Halmashauri Kuu kutokuwa na uwezo wa kupitisha
marekebisho hayo zaidi ya kupendekeza kwa Mkutano Mkuu ambao ndiyo wenye
mamlaka hayo.
"Mzee ametueleza wazi kabisa kwamba marekebisho
hayo hayana maudhui zaidi ya kumlenga mtu mmoja, aliuza sekretarieti
imepata wapi kwamba Halmashauri Kuu ina uwezo wa kufanya marekebisho
haya?,” alisema mtoa habari hayo.
Lakini, katika utetezi wake,
Sekretarieti ilisema kuna kifungu kinachotoa mamlaka hayo kwa NEC
kupitisha marekebisho hayo na kutoa taarifa kwa Mkutano Mkuu. Hata
hivyo, Kingunge hakukubaliana na hoja hiyo.
Ilielezwa pia kwamba
marekebisho hayo yaliyopitishwa kwa kupigiwa kura na wajumbe kwa kupata
theluthi tatu kutoka Tanzania Bara na nyingine tatu kutoka Visiwani,
wote walikubali isipokuwa Kingunge pekee.
“Ila tulichojifunza kwa
Mzee (Kingunge) ni kwamba lazima utetee unachokiamini hadi mwisho na
alimtaka Katibu Mkuu kuandika kuwa amepiga kura ya hapana ili iwe kwenye
kumbukumbu,” chanzo chetu kilieleza.
Hata hivyo, Kingunge
alipotafutwa jana kwa simu kufafanua msimamo wake hakutaka kuzungumza
chochote akisema kwamba alikuwa kikaoni...”Samahani niko kwenye kikao,
asante.”
Yapokea taarifa ya Katiba Mpya
Katika hatua
nyingine, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema Nec
imepokea taarifa ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Tanzania na
kuridhishwa na hatua iliyofikiwa lakini ikaitaka Serikali kuendelea
kutoa elimu kwa wananchi, huku akitaka wanachama wao kujitokeza kutoa
maoni pindi tume itakapoundwa.
Nape alisema mjadala ulikuwa iwapo
Tume ya Maadili iundwe au la lakini kutokana na katiba kuruhusu kuundwa
kwa tume mbalimbali wajumbe walikubaliana iundwe.
Aidha, alisema
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alitoa taarifa ya mgomo wa madaktari na
wajumbe waliitaka Serikali kuharakisha makubaliano yaliyofikiwa na iwe
inachukua hatua kabla ya migomo kusababisha madhara kama ilivyotokea.
Uchaguzi Mdogo Arumeru
Alisema
NEC imetoa ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea wa CCM kwenye uchaguzi
mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki na viti vinane vya udiwani
vilivyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kwa mujibu wa
ratiba hiyo, utaratibu utakaotumika katika nafasi ya ubunge ni ule wa
kura za maoni kwenye mkutano mkuu wa jimbo na kwamba Februari 13 hadi 18
wagombea watachukua na kurejesha fomu. Februari 20, mkutano mkuu wa
jimbo utapiga kura na kesho yake, kamati ya siasa ya Wilaya ya Arumeru
itajadili wagombea na kutoa mapendekezo kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa
ambayo itakutana Februari 24 na kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu ya CCM
ambayo itakutana Februari 27.
No comments:
Post a Comment