UTAFTI mpya umebaini kuwa nusu ya wanaume nchini ni wagumba ukipingana
madai ya wengi kuwa tatizo hilo linawaathiri zaidi wanawake.Kwa mujibu
wa utafiti huo, uliofanywa na Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili kati ya
mwaka 2009 na Septemba 2010 unaonyesha, asilimia 47.05 ya wanaume
wanaokwenda kupima afya zao za uzazi, hawana uwezo wa kutungisha
mimba.Malengo ya utafiti huo uliosimamiwa na Dk Henry Mwakyoma, yalikuwa
ni kubaini ni kwa kiasi gani wanaume huweza kuathiriwa katika via vyao
vya uzazi na hatimaye kushindwa kutungisha mimba.
Utafiti huo
ulionyesha kati ya wanaume 221 waliopimwa, asilimia 30.03 walikuwa na
mbegu dhaifu na asilimia 17.02 walikuwa hawana kabisa mbegu zenye uwezo
wa kutungisha mimba, zaidi ya maji tu.
Akizungumza katika mahojiano
maalumu na Mwananchi, Dk Mwakyoma alisema, ugumba kwa wanaume limekuwa
tatizo sugu katika miaka ya hivi karibuni.
“Nasisitiza kuwa,
pengine mwanaume aliwahi kupata watoto hapo awali, lakini sasa hivi
hapati, bado atakuwa mgumba,” alisema Dk Mwakyoma.Alisema hapo awali
ilikuwa vigumu kupata idadi kamili ya wanaume wenye ugumba kwa sababu
walikuwa hawajitokezi kupima.“Angalau sasa hivi wanakuja na tunawapima,
ingawa ni kazi ngumu kuwapa majibu yao,” alisema Mwakyoma.
Sababu za ugumba
Mwakyoma alitaja sababu za ugumba kwa wanaume kuwa ni uambukizo katika tezi inayozalisha manii.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni kemikali zinazoingia katika miili yetu, mionzi na wakati mwingine ajali inapoathiri tezi hiyo.
Dk
Mwakyoma aliongeza kuwa, wanaoathirika zaidi ni wanaofanya kazi
migodini, jeshini au wanaozungukwa na kemikali kwa muda mrefu.“Sababu
nyingine ni joto kuzidi katika sehemu za siri za mwanaume, kubeba
laptop, unene kupita kiasi na mazingira,” alisema.
Dk Mwakyoma
akifafanua jinsi kitengo chake kinavyopima manii ili kujua kama zina
matatizo au zipo salama, alisema, " rangi ya mbegu pamoja na umbile
huangaliwa ili kutambua ubora wake. Hata kwa kuziangalia tu, mbegu zenye
rangi aidha kijivu au nyeupe si salama.”
Kwa upande wake, Dk
Innocent Mosha, ambaye ni daktari wa uchunguzi wa magonjwa katika
Hospitali ya Muhimbili alisema, wamefanikiwa kupata takwimu hizo
kutokana na wanandoa wengi kufika hospitalini hapo kwa ajili ya kujua
sababu ya kutokuwa na watoto katika ndoa yao."Mara nyingi matokeo
huonyesha tatizo liko kwa mwanaume. Lakini kuna tabu ya kuwaeleza
ukweli, wengi hawataki kukubali," alisema Dk Mosha.
Aliongeza,
“Kesi kama hizo huleta migogoro ya kifamilia, kwani huenda mwanamke huyo
amekwishamzalia mumewe watoto ambao kimantiki si wa kwake,” alisema Dk
Mosha.
Dk Mosha alisema, kuna ugumba wa aina mbili; wa kuzawa nao na ugumba unaopatikana ukubwani.
“Wapo wanaozaliwa na ugumba, yaani mbegu zao aidha ni dhaifu au hawana kabisa mbegu tangu kuzaliwa kwao,” alisema Dk Mosha.
Shirika
la Afya duniani (WHO) linathibitisha kuwa, ujazo wa manii anaopaswa
kuwa nao mwanaume ili aweze kutungisha mimba ni milligram moja na nusu
hadi nne na nusu na kuongeza, “Ujazo wa manii ukipungua au ukizidi
basi mbegu hizo zina matatizo” alisema Dk Mwakyoma.
Naye Dk
Joshua Noreh wa kituo cha upandikizaji cha jijini Nairobi (IVF centre)
alisema, tatizo la ugumba alianza kuliona tangu mwaka 2006 baada ya
kupokea wanandoa wengi kutoka Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania
waliofika kutafuta huduma ya upandikizaji wa mbegu ili kupata watoto.
Utafiti
uliofanywa na WHO mwaka 2009 duniani, ulibainisha kuwa, mwanaume mmoja
kati ya saba wanaofika kupima afya ya uzazi hugundulika na matatizo ya
ugumba.
No comments:
Post a Comment