Abelina Kitochi Mgonjwa aliyekuwa amelazwa katika wodi ya Sewahaji
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam jana
akilia nje ya wodi hiyo baada ya kukosa huduma kwa siku kadhaa kufuatiwa
na mgomo wa Madaktari bingwa na Wauguzi wanaogoma kuishinikiza
serikali nyongeza ya mishahara.
WAKATI Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii ikianza kazi ya
kuzungumza na madaktari walio kwenye mgomo, madaktari bingwa katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na walio katika Taasisi ya Mifupa
(MOI) wamegoma. Mgomo huo wa jana ulihusisha vitengo vyote huku
wagonjwa waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo wakipewa taarifa za
kuondoka katika wodi walimolazwa.
Azimio la mgomo huo
lilifikiwa katika kikao cha dharura kilichoitishwa na jopo la madaktari
bingwa wakiongozwa na Dk James Rwehabura ambaye ni daktari bingwa wa
Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu.
Habari za ndani
kutoka katika kikao cha dharura cha wanataaluma hao, zilisema uamuzi
huo ulifikiwa kwenye kikao cha madaktari hao kilichoanza mapema asubuhi
jana na kumalizika saa 6:00 mchana. “Kwa pamoja tumekubaliana kuweka
vifaa chini, hii ni kutokana na ukweli kuwa hali ya utoaji huduma katika
hospitali hii ni mbaya huku taarifa za Serikali zikiwa siyo za kweli,”
alidokeza mmoja wa madaktari bingwa.
Daktari huyo aliyekataa
kutaja jina lake, alisema, “Tumekubaliana kugoma hadi hapo Serikali
itakapotoa majibu ya madai yote yaliyowasilishwa na jumuiya ya madaktari
inayoongozwa na Dk Stephen Ulimboka kwa Serikali.” Jumuiya hiyo
iliwasilisha madai mbalimbali likiwamo la kuitaka Serikali kupeleka
vifaa na dawa katika hospitali za Serikali ili madaktari hao waweze
kutoa huduma bora kwa jamii.
Pia, madaktari hao walitaka
kusitisha safari za vigogo kwenda kutibiwa nje kwa magonjwa yanayotibika
ndani kwa kile walichodai, hali hiyo inachangia wao kudharauliwa na pia
kuzorotesha jitihada za Serikali katika uboreshaji wa mazingira ya kazi
kwa madaktari hao.
Kwa nyakati tofauti, madaktari hao
walibainisha sababu ya mgomo wao na kudai kuwa, kikubwa ni mazingira
magumu ya kazi. Daktari mwingine ambaye hakupenda jina lake kuandikwa
gazetini alisema, licha ya mishahara na posho ndogo, lakini mazingira ya
kufanyia kazi yamekuwa magumu mno.
“Tumeshaamua , ‘tools
down’ hospitali haina kitu, hata ‘mask’ hakuna badala yake tunavaa gozi
tunapofanya upasuaji, acha hiyo, hata nyuzi za kushonea wakati wa
upasuaji hakuna,” alisema daktari huyo. Daktari huyo alisema, hawawezi
kufanya kazi katika mazingira hayo kwa sababu yatawasababisha kuwa na
utendaji mbovu na baadaye taifa kuwalalamikia.
Alisema hapa
nchini madaktari bingwa ni wachache, kwa hiyo kitendo cha wao kufanya
kazi peke yao bila wasaidizi, yaani madaktari wa mafunzo na wale
wanaomaliza, wanaelemewa na mzigo wa kazi. Dk Henry Mwakyoma, Mhadhiri
Mkuu wa Chuo cha Udaktari Muhimbili, (MUHAS) ambaye hakuwapo katika
kikao hicho cha dharura alidai kuwa, yeye kama mhadhiri hajagoma, lakini
alikiri kuwapo kwa mazingira magumu ya kazi.
“Mpaka sasa
hatujalipwa mishahara ya mwezi uliopita, halafu kazi yetu ndiyo kama hii
tunatakiwa tufanye utafiti, unategemea tutafanya kazi kwa umakini
kweli? Tutawafundisha madaktari kwa umakini?” alihoji Dk Mwakyoma.
Mwakyoma
alisema, Serikali haiwezi kudai kuwa haina fedha za kutosha wakati
imetumia mamilioni ya shilingi katika sherehe za miaka 50 ya Uhuru na
uchaguzi wa Igunga. Alisema ni vyema Serikali ikajipanga na kuamua
kushughulikia masuala ya madaktari kwa hekima kwani kukaa kimya bila
kutoa suluhu ni sawa na kufanya ushindani usio na maana.
Hata
hivyo, Ofisa Habari Mwandamizi wa MNH Aminael Aligaesha alisema jana
jambo hilo lilikuwa likishughulikiwa kwani vipo vikao vinavyoendelea.
Wagonjwa watimuliwa wodini
Wodi
mbalimbali hospitalini hapo zilitawaliwa na vilio kutokana na wagonjwa
na ndugu za wagonjwa kupewa taarifa za kuondoka katika eneo hilo mara
moja, kutokana na mgomo huo wa madaktari. Mmoja wa wagonjwa waliokuwa
wamelazwa katika wodi ya Sewahaji, Sadick Dimoso (35) mkazi wa Morogoro
alisema hali sasa MNH ni mbaya.
“Tumeambiwa tuondoke wodini
bila ya kuruhusiwa na daktari, hii ni hatari tena wanasema tuondoke
tukakae huku hadi wiki mbili ndio turudi kuangalia,” alisema Amina
Ramadhani, aliyekuwa akisubiri kufanyiwa upasuaji wa jicho. Alisema
hatua ya kutakiwa kuondoka hospitalini hapo imekatisha matarajio yao ya
kuendelea kuwa hai na kuitaka Serikali kufanyia kazi madai ya madaktari.
Wakati kundi la watu wengine wakililia huduma hosptalini hapo,
baadhi ya ndugu za wagonjwa waliingia katika mgogoro na walinzi wa wodi
hiyo ya Sewahaji wakitaka waandishi wa habari kuingia wodini.
Vikao
vya Kamati Wakati hayo yakijiri, vikao baina ya madaktari na Kamati ya
Kudumu ya Huduma za Bunge, viliendelea jana katika ofisi ndogo za Bunge
huku taarifa zake zikiwa ni siri.
No comments:
Post a Comment