MSAFARA wa Rais Jakaya Kikwete uliokuwa ukielekea Bagamoyo jana
ulilazimika kusimama kwa muda baada ya kuzuka kwa vurugu kubwa za
kurushiwa mawe katika eneo la Namanga Tegeta Manispaa ya Kinondoni jiji
la Dar es salaam.
Wakazi wa eneo hilo walifunga barabara kwa muda, na hivyo kuzuia
msafara wa Rais Kikwete kwa kile walichodai aweze kuona namna matajiri
wanavyotumia uwezo wao wa kifedha kuwanyanyasa raia wanyonge.
Vurugu hizo zilisababisha mabaunsa wawili kujeruhiwa vibaya na
wananchi na wamelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu
zaidi.
Vurugu hizo zilizodumu kwa zaidi ya saa mbili, zilitokana na kitendo
cha watu (mabaunsa) wanaoaminika kukodiwa na mmiliki wa kituo cha mafuta
cha GAPCO aliyetajwa kwa jina Hemed Salum, kuvunja nyumba zao na
mfanyabiashara huyo.
Hata hivyo, msafara huo wa Rais uliweza kuendelea baada ya askari
wengi kumwagwa na kuanza kuwatawanya wananchi waliokuwa na hasira.
Wakiongea kwa hasira, wananchi hao walidai kuchoka na vitendo wanavyotendewa na baadhi ya wawekezaji.
“Watu wenye pesa wanafanya kila wanaloliona kuwa linawafaa bila hata
kujali sheria za nchi, sasa sisi wananchi tulifanya makusudi ili Rais
aone mambo tunayofanyiwa na hawa wawekezaji atusaidie, lakini kinyume
chake tunapewa bakora,” alisema mwananchi mmoja ambaye hakupenda kutajwa
jina lake.
Watu waliobomolewa nyumba zao wamesema kuwa wamesikitishwa na kitendo
cha mmiliki wa kituo hicho kuwavunjia nyumba zao akidai kuwa wamejenga
kwenye eneo lake.
“Hili eneo ni letu tunalimiki kihalali, kwani tuliachiwa urithi na
baba yetu na sisi tuko watoto kumi, kila mmoja alipewa eneo lake
tukajenga, na eneo la barabarani halikuwa letu hivyo aliuziwa yeye
(Salum) na mtu mwingine akajenga kituo cha mafuta.
“Kinyume chake ametafuta nyaraka za kugushi na kuanza kudai kuwa sisi
tunaishi katika eneo lake tuondoke tumwachie, lakini hakuna mtu yeyote
asiyejua kwamba eneo hili ni letu na tumeachiwa urithi na baba yetu,”
alisema Fikiri Saidi mmoja wa waliobomolewa nyumba huku akitokwa na
machozi.
Fikiri aliongeza kwamba kabla ya tukio hilo siku mbili zilizopita,
mmiliki huyo aliwafuata nyumbani kwao kwa lengo la kutaka wamuuzie eneo
hilo kwa shilingi milioni 100 ili wagawane lakini walikataa, ndipo
akatoa vitisho akiwambia kuwa, kwa kuwa wamekataa pesa hizo atawapa
wanaozihitaji ili wabomoe na hawataambulia kitu chochote.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela alisema polisi
wanamshikilia mmiliki huyo kwa kosa la kujichukulia hatua mkononi na
kuwavunjia wakazi hao nyumba na kusababisha upotevu wa mali.
Hata hivyo, Kenyela alisema polisi watafanya msako wa watu waliohusika
kupopoa mawe msafara huo, huku akiwataka wakazi hao kuwa watulivu
wakati serikali ikiangalia namna ya kuwatafutia hifadhi ya muda.
Watu walioathirika na tukio hilo ni Fikiri Saidi, Rashid Said, Farida
Said na Ally Mkwandu, wengine ni Shabani Said, Kassim Said, Sijali Said
Rajab Said na Waziri Rashid, ambapo inakadiriwa kuwa thamani ya nyumba
na mali zilizoharibiwa inafikia zaidi ya sh milioni 300.
Chanzo cha Habari Tanzania daima
|
No comments:
Post a Comment