NJOMBE

NJOMBE

Sunday, February 5, 2012

Chadema:Kauli ya viongozi CCM kuhusu posho ni unafiki

 


Kauli ya CCM juu ya nyongeza ya posho za vikao kwa wabunge ni ya kinafiki, haionyeshi uongozi thabiti na inalenga chama tawala kujikosha kutokana na hasira ya umma dhidi ya viongozi waandamizi wa chama hicho na wabunge wake kutaka nyongeza ya posho za vikao kinyemela.
Aidha, kauli hiyo ni muendelezo wa kauli za CCM za kujikosha mbele ya umma baada ya wananchi kupinga maamuzi ya serikali inayoongozwa na chama hicho katika masuala ambayo chama hicho kilikuwa na taarifa nayo kabla lakini kikashindwa kutoa muongozo unaostahili kwa serikali kama ilivyokuwa kwenye suala la kupandisha kupindukia kwa ushuru wa mafuta ya taa na kuongeza bei na gharama za maisha kwa wananchi wa kipato cha chini au kuhusu malipo ya fidia kwa Dowans.
Kauli kwamba ‘CCM iliwaomba na kuwasihi wabunge na mamlaka zinazohusika na mchakato wa swala la nyongeza ya posho za vikao kuliangalia upya na kutumia busara, ikiwezekana kuachana nalo kwasasa’ inadhihirisha kwamba kimsingi chama hicho kimepoteza uwezo wa kuwa chama tawala.
Kauli kama hii ni kama agizo lililotolewa na Kamati Kuu ya CCM katika kikao chake cha tarehe 31 Agosti 2011 ya kutaka serikali ipunguze bei ya mafuta ya taa baada ya kuona wananchi wanaungana na msimamo wa CHADEMA uliotolewa bungeni na wabunge wake wakati wa kupitishwa kwenye muswada wa sheria ya fedha mwezi Juni 2011 na kujadiliwa kwa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini tarehe 15 Julai 2011.
Hata hivyo mpaka sasa agizo hilo ambalo limetokana na kikao kilichoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Rais Jakaya Kikwete halijatekelezwa hali ambayo inadhihirisha ulegelege wa CCM na serikali yake katika kusimamia masuala ya msingi ya taifa hali ambayo athari zake zinathibitika hivi sasa katika mjadala huu wa posho za vikao ambapo ombwe na uongozi linaonekana bayana katika chama hicho na serikali.
Kauli ya CCM ya kumpongeza Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho kwa kushindwa kuonyesha uongozi na badala yake kutupa mzigo wa wabunge kwenye suala ambalo kwa mujibu wa sheria Rais ndiyo mwenye mamlaka nalo ni ishara ya CCM kulea misingi ya kutowajibika miongoni mwa viongozi wakuu wa serikali na chama hicho.
Iwapo CCM ingekuwa na dhamira ya kweli ya kukataa posho za vikao ingefanya maamuzi ya kukataa kupitia vikao vya chama hicho vya kamati kuu na halmashauri kuu ambavyo viliongozwa na mwenyekiti wa chama hicho Rais Kikwete kwa nyakati mbalimbali wakati ambapo mjadala wa posho za vikao ukiwa tayari umekolea katika taifa baada ya CHADEMA kuibua suala husika ndani na nje ya bunge kuanzia wakati wa bunge la bajeti kupitia pia maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni.
CHADEMA inaitaka CCM kama kweli inajali maslahi ya wananchi kufanya maamuzi ndani ya vikao vya chama hicho na kuandaa mapendekezo kwa serikali ya kufuta posho zote za vikao kwenye mfumo wa utumishi wa umma kama ilivyoelezwa katika ilani ya CHADEMA ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na Mpango wa Taifa wa miaka mitano uliopitishwa na bunge mwaka 2011.
Aidha, badala ya kumpongeza Rais Kikwete kwa kauli iliyotolewa na ikulu ya kuhamisha lawama kuhusu suala hilo kwa wabunge, CCM itoe mwito kwa Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho kutoa kauli yake mwenyewe ya kufanya uamuzi wa kufuta posho za vikao katika mfumo wa utumishi wa umma na kutoa kauli ya wazi ya kukataa nyongeza ya posho za wabunge.
Pia, CCM badala ya kutaka tu wabunge kwa ujumla kutafakari ieleze inachukua hatua gani kwa viongozi wa serikali na bunge wanaotaka na chama hicho kunukuliwa na vyombo vya habari wakieleza kwamba Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho kuwa amebariki nyongeza ya posho hizo na hivyo kukosekana kwa uwajibikaji wa pamoja katika serikali na chama hicho.
Kushindwa kwa CCM kuchukua hatua za kichama dhidi ya viongozi hao ambao ni wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho kunadhihirisha kwamba pamoja na kuwa Rais Kikwete hajasaini masharti mapya ya kazi za wabunge ameshakubaliana nao kinyemela kuhusu kuanza kutoa nyongeza ya posho za vikao; kinyume na hapo kauli za CCM zitaendelea kudhihirika kuwa ni za kinafiki na za kujikosha.
CHADEMA inaendelea kusisitiza kauli yake kwamba ongezeko la posho ya vikao lilofanyika linapaswa kusitishwa kwa kuwa limefanyika kinyume na taratibu na pia halina uhalali wowote kimantiki na halijazingatia uhalisia wa maisha ya wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla; nyongeza hiyo ya posho ya vikao ni haramu (Illegitimate).
Aidha, kauli iliyotolewa kwamba nyongeza hiyo ya posho za vikao ni kwa sababu ya kupanda kwa gharama za maisha mkoani Dodoma haina ukweli, wala mantiki na ina mwelekeo wa upendeleo.
Nyongeza hiyo ya posho ya vikao ni matumizi mabaya ya madaraka na ni dharau kwa walipa kodi wanaohangaika na kupanda kwa gharama za maisha na athari za ubadhirifu wa fedha za umma. Ni udhaifu kufikiri kwamba suluhisho la kupanda kwa gharama za maisha ni kuongeza posho za kikao; tatizo la kupanda kwa gharama za maisha linapaswa kushughulikiwa kwa kuchukua hatua dhidi ya matatizo ya kiuchumi katika nchi ili kuweza kuwa na tija kwa wananchi wengi ambao ni waathirika zaidi wa kupanda kwa gharama za maisha kuliko wabunge.
CHADEMA inarejea kuukumbusha umma kwamba Sheria ya Utawala wa Bunge (National Assembly Administration Act) ya mwaka 2008 kifungu cha 19 kinataja aina ya posho ambazo zinaweza kutolewa kwa wabunge kama ambavyo Rais ataeleza kwa maandishi. Katika kipengele (d) sheria imetaja orodha (i) mpaka (iii) ya posho ambazo wabunge wanastahili kulipwa za usafiri, kujikimu na wasaidizi. Katika orodha hiyo hakuna Posho ya Kikao (Sitting Allowance) ambayo inalipwa hivi sasa kwa kuwekwa kwenye akaunti za wabunge moja kwa moja ambayo kamati ya wabunge wa CHADEMA tunataka ifutwe mara moja kama sehemu ya mchakato wa kubadili mfumo mzima wa malipo ya posho kwa watumishi wa umma.
Kifungu 19 (d) (iv) kimempa mamlaka Rais ya kutoa posho zingine kwa wabunge kwa kadiri atakavyoelekeza; kifungu hiki kimetoa mwanya wa kutolewa kwa waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais wa tarehe 25 Oktoba 2010 wenye kumbukumbu na. CAB111/338/01/83 masharti ya kazi ya mbunge ambao umeeleza viwango vya posho mbalimbali ikiwemo kutoa posho ya vikao (Sitting Allowance).
Hivyo, badala ya Rais Kikwete kukwepa wajibu huo wa kisheria na kuhamisha mzigo kwa wabunge anapaswa yeye mwenyewe kufanya uamuzi wa kukataa nyongeza ya posho za vikao na kufuta posho za vikao katika mfumo mzima wa utumishi wa umma kama ilivyopendekezwa na CHADEMA pamoja na kambi rasmi ya upinzani bungeni.
Izingatiwe kwamba uchumi wa nchi hivi sasa unasuasua, serikali ina hali mbaya ya fedha kutokana na kupungua kwa kiwango cha fedha kinachopatikana katika kodi na washirika wa kimaendeleo ukilinganisha na mahitaji ya bajeti; na hivyo kukopa kibiashara kwa ajili ya kuziba nakisi iliyopo.
Kupungua kwa uzalishaji, kiwango cha fedha pamoja na kuongezeka kwa ubadhirifu katika matumizi ya rasilimali za umma kunachangia katika mfumuko wa bei hali inayohitaji mpango wa dharura wa kunusuru uchumi wetu ukaohusisha pamoja na mambo mengine kubana matumizi ya serikali.
CHADEMA kwa kurejea tamko la mwanzo wa mwaka 2012 lililotolewa na Katibu Mkuu Dr Wilbroad Slaa ambalo limetaka kipaumbele kiwe ni kunusuru uchumi wa nchi na kupanda wa gharama za maisha kwa wananchi, tulitarajia kwamba CCM na serikali yake watoe kwa umma mpango wa kukabiliana na hali hiyo badala ya kurushiana mpira kuhusu nyongeza ya posho za vikao huku mwelekeo wa uchumi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ukiwa kwenye hali tete na nchi ikiwa kwenye migogoro ya kijamii kuhusu maslahi ya madaktari, wanafunzi na makundi mengine katika jamii.
CHADEMA inasisitiza msimamo wake kwamba posho za vikao zifutwe kwa kuzingatia kuwa Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 imeeleza kwamba lengo la msingi ni kuondoa posho za vikao (sitting allowance ) hatua ambayo itaambatana na nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma kuendana na ujuzi, nafasi, wajibu ili wafanyakazi walipwe kwa haki kwa kile wanachofanya kwa haki; uamuzi ambao utawezesha pia kuelekeza fedha zaidi katika miradi ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment