KAMATI ya Siasa ya Wilaya ya Simanjiro kesho inatarajia kukutana na
kumjadili aliyekuwa Katibu wa UVCCM Wilaya ya Simanjiro, Alhaj Omar
Kariaki anayedaiwa kutokomea na fedha zilizochangwa kwenye harambee
maalumu ya kutunisha mfuko wa maendeleo ya vijana wilayani humo.
Hayo
yalisemwa jana na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer
ikiwa ni siku moja baada ya Kariaki kuibuka na kukiri kutokabidhi fedha
hizo.
Laizer alithibitisha jana kufanyika kwa kikao hicho
alichosema pia kitahudhuriwa na mkuu wa wilaya hiyo, Khalid Mandya
ambaye amevalia njuga upatikanaji wa fedha hizo zilizopatikana kwenye
harambee iliyoongozwa na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha.
Nahodha ambaye
sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Muungano, binafsi
alichangia Sh2 milioni katika harambee hiyo iliyofanyika katika ukumbi
wa hoteli ya kitalii ya Manyara Inn ulioko mji mdogo wa Mererani
wilayani Simanjiro.
“Kwanza nachukua fursa hii kukupongeza wewe
binafsi na gazeti lako la Mwananchi kwa jinsi mlivyofuatilia kwa karibu
suala hili hadi mtuhumiwa ambaye tumemtafuta kwa kipindi kirefu
kujitokeza hadharani na kukiri kuondoka na fedha zetu. Jumamosi
tunakutana kwenye kamati ya siasa wilaya kujadili hili,” alisema Laizer.
Akizungumza
kwa njia ya simu kutoka Simanjiro jana asubuhi, Mwenyekiti huyo wa
vijana alisema kila siku anamwomba Mungu suala hilo lipate ufumbuzi
kwani licha ya kuwapa picha mbaya mbele ya waliojitolea kuchanga fedha
zao kuinua hali ya maisha ya vijana kwa kuanzisha mradi wa mahari ya
kusafirisha abiria, yeye binafsi amekuwa akihusishwa na upotevu wa fedha
hizo.
Habari zaidi katika Mwananchi.
No comments:
Post a Comment