MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imeshindwa kumsomea
maelezo ya awali aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, anayekabiliwa na kesi ya kukutwa
na simu kwenye gereza la Ukonga, kutokana na wakili wake anayemtetea
Majura Magafu kutokuwapo mahakamani.
Wakili Mwandamizi wa
Serikali, Elizabeth Kaganda, jana alidai mbele ya Hakimu Mkazi Stuart
Sanga, kuwa kesi imekuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya
awali yanayohusiana na mashtaka yanayomkabili.
Baada ya kutoa
maelezo hayo, Liyumba aliieleza mahakama kuwa wakili wake hayupo
amekwenda mkoani Arusha kuhudhuria mkutano.Hivyo, Hakimu Sanga
aliiahirisha kesi hiyo hadi Machi 15, mwaka huu itakapopelekwa tena kwa
ajili ya Liyumba kusomewa maelezo ya awali.
Hatua hiyo ilikuja
baada ya Mahakama ya Kisutu kulitupilia mbali ombi la Liyumba kutaka
afutiwe kesi hiyo kwa sababu, haina mamlaka ya kuisikiliza.
Liyumba
kupitia kwa Wakili Magufu aliwasilisha pingamizi hilo la awali akidai
mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza, kwa sababu taratibu za awali
za sheria ya Magereza ya mwaka 2002 hazikufuatwa.
Wakili Magafu
alidai kwa mujibu wa Sheria ya Magereza ya mwaka 2002, inataka mshtakiwa
anayeishi mahabusu kabla hajaletwa mahakamani asomewe mashtaka na ofisa
wa magereza gerezani, iwapo atapatikana na hatia atapewa adhabu.
Alidai
kuwa iwapo mshtakiwa huyo ataonekana amekuwa mtendaji sugu wa makosa
akiwa gerezani, italazimika afunguliwe mashtaka katika mahakama za
uraiani.
Akipangua hoja za upande wa utetezi, Wakili wa Serikali
Eliezabeth Kaganda, alidai kuwa kesi ya aina hiyo inayomkabili Liyumba
siyo ya kwanza kufunguliwa mahakama nchini.
Kaganda alitaja kesi
ya jinai Na. 472/2009 iliyokuwa ikimkabili Juma Matonya katika Mahakama
ya Wilaya ya Temeke na Hakimu Mzava alimhukumu kifungo cha miezi sita
jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukutwa na simu gerezani.Kesi
nyingine mbili za aina hiyohiyo, ambazo washtakiwa walitiwa hatiani moja
akitakiwa kulipa faini ya Sh20,000 na nyingine kwenda jela miezi sita.
Wakili
Kaganda alieleza kuwa kabla hawajamfikisha Liyumba mahakamani hapo
Jeshi la Magereza lilikuwa na mamlaka ya kushughulikia tuhuma zilizokuwa
zikimkabili mshtakiwa na kwamba, mkurugenzi wa mashtaka na maofisa wa
magereza walikuwa wameishaamua kuifungua kesi hiyo mahakamani hapo.
Lakini
kwa sababu hiyo haikuwa mara ya kwanza kukutwa na simu gerezani na
alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu, hivyo haikuwa
rahisi kumpa adhabu akiwa gerezani.
Awali, Septemba 8, mwaka jana
Liyumba alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza akikabiliwa na
shtaka la kukutwa na kitu kilichokatazwa gerezani chini ya kifungu cha
86 (1,2) cha sheria ya Magereza kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka
2002.
Liyumba ambaye wakati huo alikuwa mfungwa mwenye
Na.303/2010, Julai mwaka jana, aliyokuwa akitumia kufanyia mawasiliano
binafsi wakati ni kinyume cha sheria.
No comments:
Post a Comment