Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kwamba Uchaguzi mdogo wa
jimbo loa Arumeru Mashariki utafanyika Aprili Mosi mwaka huu na kuonya
kuwa hakutakuwepo na uandikishaji wa wapigakura wapya bali watatumika
wale ambao walijiorodhesha kwenye daftari kwenye uchaguzi mkuu 2010.
Uchaguzi
huo unafuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jeremia Sumari
kilichotokea Januari 19, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH) alikokuwa amelazwa kwa ajili ya matibabu.
“Baada ya Tume
kupokea taarifa hiyo ya kuwepo nafasi wazi kwa Jimbo la Arumeru
Mashariki, Tume imepanga kufanya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo
hilo kwa mujibu wa sheria,” alisema Mwenyekiti wa NEC, Damian Lubuva
kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.
Alisema kwamba tayari
wametoa ratiba ya uchaguzi huo pamoja na wa kata nane ili kujaza nafasi
za madiwani zilizowazi na kuonya: “Ifahamike kwamba, hakutakuwa na
kuandikisha Wapiga Kura kwa ajili ya Chaguzi hizo. Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura lililotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, ndilo
litakalotumika.”
Vile vile alisema vituo vya kupigia kura kwenye
uchaguzi huo ni vile vilivyotumika kwenye chaguzi mkuu uliopita na
kwamba watabandika orodha ya wapiga kura kwa siku saba kabla ya
uchaguzi.
“Wananchi wote wa Jimbo la Arumeru Mashariki na Kata zote
ambazo Chaguzi Ndogo zitafanyika mnaombwa kwenda katika vituo vyenu vya
Kupiga Kura na kukagua majina yenu ili kujua Vituo mtakavyo pigia Kura,”
alisema Lubuva.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo alisema uteuzi wa
wagombea utafanyika Machi 8 na kampeni zitaanza siku inayofuata na
kumalizika mwishoni mwa mwezi huo.
Katika hatua nyingine, Lubuva
alisema wamepanga kufanya chaguzi za kujaza nafasi zilizo wazi katika
kata nane, Vijibweni Halmashauri ya Temeke, Kiwangwa halmashauri ya
Bagamoyo, Kirumba (Mwanza), Lugangabilili (Bariadi), Chang’ombe
(Dodoma), Kiwira (Rungwe), Lizaboni (Songea) na Msambweni (Tanga).
No comments:
Post a Comment