RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali itagharimia ujenzi wa makao makuu ya kudumu ya Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (ACHPR) mjini Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilisema, Rais Kikwete anaunga mkono mageuzi yanayokusudiwa kufanywa kwenye muundo wa mahakama hiyo.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa ujenzi huo unalenga kuiwezesha mahakama hiyo kuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuzitolewa uamuzi kesi za makosa ya jinai sawa na mamlaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) ya mjini The Hague, Uholanzi.
Ahadi hiyo ya Rais Kikwete aliitoa wakati akizungumza na ujumbe wa majaji wa mahakama hiyo, wakiongozwa na rais wake, Jaji Gerald Niyungeko, mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Katika taarifa hiyo ya Ikulu, Rais Kikwete aliwaambia majaji kufikiria kuwa na mchoro wa jengo zuri lenye hadhi la mahakama hiyo, kwani itakuwa ni mahakama ya bara zima na wala siyo ya Tanzania pekee.
Rais pia aliwaahidi kuwa serikali itaongeza kasi ya kutafuta ardhi kwa ajili ya ujenzi wa mahakama hiyo mjini Arusha, kutokana na mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa AU uliomalizika jana kukubaliana ujenzi mjini humo.
Jaji Niyungeko alimweleza Rais Kikwete kuhusu shughuli za mahakama hiyo, ambapo aliishukuru serikali kwa mchango wake mkubwa katika kuunga mkono shughuli za mahakama hiyo.
Jaji huyo alisema mahakama hiyo sasa imeanza kupokea kesi nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo mwanzo ambapo kwa kipindi cha mwaka jana ilipokea kesi 14, ikiwamo moja kutoka Tanzania, na maombi mawili ya kuitaka mahakama hiyo kutoa ushauri wa kisheria.
No comments:
Post a Comment