Remija Mtema Regia Mtema
PACHAwa Mbunge wa Viti Maalum Chadema, Regia Mtema (32) aliyefariki juzi kwa
ajali ya gari eneo la Ruvu mkoani Pwani, Remija Mtema (32) ameeleza
alivyonusurika baada ya kushuka kwenye gari muda mfupi kabla ya ajali.
Akizungumza na gazeti hili jana, Remija ambaye ni kurwa, alisema Regia
kabla ya ajali iliyosababisha kifo chake, alikuwa akitoa kauli za kutia moyo na
za kutarajia kuonana tena.
“Tulitoka nyumbani kwake Mbezi-Makabe, Dar es
Salaam kwenye saa tatu asubuhi, mimi nilikuwa nakwenda Iringa na tuliondoka na
gari lake hilo lililopata ajali nyumbani hapo, wakanishusha Mbezi stendi
nisubiri basi la Iringa .
“Wakati tunatoka nyumbani alikuwa anaongea kwa
uchangamfu sana, kwanza juzi (Ijumaa)
tulizungumza na kupanga kwamba mimi
niende Iringa kuomba ruhusa kazini, maana kuna wakati nikiwa huru namsaidia kazi
kama Katibu wake, tulipanga nikipewa ruhusa nirudi nimsaidie kwenye Kamati na
Bungeni,” alisema Remija.
Kwa mujibu wa Remija, walikubaliana hivyo na
baada ya kupanga mambo yao usiku huo wa
Ijumaa, walicheza sana karata.
“Ni karata za kuagana maana mimi ndio nilikuwa nasafiri kesho yake
kwenda Iringa, asubuhi ndio tukaondoka huku tunacheka, mimi nikashukia Mbezi,
alikuwa ni zaidi ya pacha wangu, alikuwa rafiki yangu,” alisema Remija.
Remija ambaye ni Ofisa Tarafa wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa,
alisema aliposhuka Mbezi
kusubiri gari, walikaa nae na watu wengine kwenye
gari kwa karibu saa moja wakimsubiri mama yao, Bernadeta aliyekuwa akitokea
Tabata-Chang’ombe nyumbani kwao.
“Mama alipofika aliingia garini na
wakaondoka, pacha akasisitiza nikipata usafiri niwaambie, ni
kama alitamani
niendelee nao lakini haikuwa hivyo, baada ya muda wa nusu saa mama alipiga simu
kuniuliza kama nimepata basi maana waliona basi la Upendo limewapita, nikamjibu
bado, baada ya muda mfupi nikapata basi la Budget,”
“Nilipoingia kwenye
basi saa tano asubuhi hivi, nikamtumia ujumbe Regia kuwa nimepata basi, lakini
ujumbe haukujibiwa, nikajua labda kwa kuwa alikuwa anaendesha gari, nikaendelea
kusoma gazeti na tulipofika Ruvu niliona watu lakini sikutilia maanani
nikaendelea kusoma gazeti,” alisema Remija.
Alisema kabla hajafika
Chalinze, alipigiwa simu na mama yake kuwa wamepata ajali na
wapo Hospitali
ya Tumbi na kumuomba dereva ashuke kwa kuwa ndugu zake wamepata ajali
Ruvu.
“Dereva na kondakta waliniuliza aina ya gari, nikawaambia wakathibitisha
waliiona. akasimamisha gari nikashuka na kuanza safari ya kurudi hadi Hospitali
ya Tumbi, nikakuta kweli Regia amefariki,” alisema Remija.
Alisema pacha
wake alikuwa jasiri ambaye akiamua jambo lake ni lazima alifanye, alikuwa na
huruma asiyependa mtu aonewe na alimuamini Mungu kwa kila jambo kutokana na
malezi ya kiimani waliyopata kwa baba na mama yao mlezi.
Kwa mujibu wa
Remija, yeye na pacha mwenzake walizaliwa Hospitali ya Ocean Road, jijini Dar
es Salaam Aprili 21 mwaka 1980, alikuwa mpenzi na shabiki wa timu ya mpira
wa miguu ya Simba kwa hapa nchini na kwa nje alikuwa akipenda kufuatilia
Barcelona ilipocheza zaidi ya timu nyingine.
Baba wa marehemu, Estelatus
Mtema aliliambia gazeti hili jana kuwa anamshukuru Mungu kwa
kila jambo na
kuomba majeruhi akiwemo mkewe waliolazwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili
walikohamishiwa wakitokea Tumbi juzi jioni, wapone mapema.
Utaratibu wa
maziko
Mtema alisema misa itafanyika leo saa tisa alasiri katika Kanisa
Katoliki la Segerea pamoja na heshima za mwisho na kesho kutakuwa na heshima za
mwisho katika ukumbi wa Karimjee.
Alisema bada ya hapo safari ya kulekea
Ifarakara itaanza na maziko yatakuwa Jumatano huko
Ifarakara mjini nyumbani
kwa wazazi wa marehemu.
Majeruhi Muhimbili
Mtoto wa binamu wa mama
wa marehemu, Theresia Simon, ambaye ilidaiwa kuwa amefariki
kutokana na
kujeruhiwa vibaya kichwani, anaendelea vizuri alikolazwa wodi namba 10 Kibasila.
Theresia katika mahojiano, alisema anamshukuru Mungu hali yake
inaendelea vizuri na maumivu yamepungua.
Baadhi ya vyombo vya habari
jana, viliripoti kuwa Theresia aliyejeruhiwa kichwani, alikufa hivyo kufanya
idadi ya walioaga dunia kuwa wawili akiwemo Mbunge Mtema.
Shangazi yake,
Consolata Mwandenga alisema pia kuwa alimpa uji jana na kula vizuri asubuhi na
mchana hivyo hali yake ni njema. Pia mama wa marehemu, Bernadeta na watu wengine
wawili, wanaendelea vizuri na wote wamelazwa katika wodi hiyo.
Vikao
vya dharura Chadema
Wakati huo huo Sekretarieti ya Chadema jana ilifanya
kikao cha dharura chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa kupanga
utaratibu wa chama na viongozi wake wakuu, kushiriki kikamilifu kwenye
maombolezo, heshima za mwisho na hatimaye maziko yaliyopangwa kufanyika Ifakara.
Shughuli hizo za mazishi ya heshima kwa Mbunge huyo, kwa mujibu wa
taarifa za Chadema, zitaongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman
Mbowe.
Mbali na Sekretarieti, pia Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa
Chadema, ilifanya kikao cha
dharura, kwa kuzingatia uzito wa msiba uliotokea
na kupitisha azimio kwamba wabunge wote wa Chadema washiriki kutoa heshima ya
mwisho.
Kwa mujibu wa azimio hilo, wabunge wote wa chama hicho
watasindikiza mwili wa Regia
hadi Ifakara na kushiriki maziko.
No comments:
Post a Comment