Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya 2012 yaliyofanywa
na Bunge yamezua mtafaruku na sintofahamu, huku wafanyakazi wa sekta
mbalimbali wakiyapinga kwa maelezo kwamba ni kandamizi na yanalenga
kuwanyima haki ya fedha wanazokatwa kwa mujibu wa sheria kuchangia
mifuko hiyo.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
Tanzania (Tucta), Nicolaus Mgaya aliliambia gazeti hili jana kuwa,
watafungua kesi katika Mahakama ya Kazi nchini, kupinga hatua ya
Serikali kubadili Sheria ya muda wa lazima wa kuchukua mafao hayo ambao
ni kati ya miaka 55 na 60.
Tangu juzi watu kutoka sehemu
mbalimbali hasa jijini Dar es Salaam wamekuwa wakipiga simu katika
chumba cha habari cha Mwananchi kwa lengo la kupata ufafanuzi wa
mabadiliko hayo ya sheria yaliyopitishwa na mkutano wa saba wa Bunge,
Aprili 13 mwaka huu.
Kadhalika sheria hiyo inayozuia mwanachama
wa mfuko wowote wa hifadhi ya jamii kuchukua mafao kabla ya umri wa
kustaafu kwa mujibu wa sheria ambao ni miaka 55, lilichukua nafasi kubwa
katika mijadala ya mitandao ya kijamii ambako wengi wa wanaliochangia,
wameiponda sheria hiyo na kuiita kuwa ni ya ‘kinyonyaji’.
Hata
hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka alisema jana kuwa: “Hakuna haja ya
watu kuwa na wasiwasi, maana sheria hii itafuatiwa na kanuni na miogozo
mingine ambayo ninaamini kwamba itaondoa wasiwasi uliopo”.
Isaka
alisema miongoni mwa mambo yatakayozingatiwa katika miongozo hiyo ni
iwapo mwanachama atafukuzwa au kuachishwa kazi, wanachama ambao wako
kwenye kazi za mikataba na wale wanaopata ulemavu wa kudumu wakiwa
kazini.
“Kimsingi ni kwamba suala la mafao ya kuacha kazi kabla
ya umri wa kisheria wa kustaafu limefutwa kwa mifuko yote, isipokuwa
katika mazingira hayo niliyoyaeleza litawekewa miongozo, na hii ni kwa
faida ya wachangiaji,”alisema Isaka.
Alisema baada ya sheria hiyo
kuwa imepitishwa na Bunge, kisha kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete mwezi
Juni mwaka huu, SSRA ilianza mchakato wa kuweka miongozo na baada ya
hapo kinachofuatia ni kutoa elimu kwa umma na baadaye kuanza kutumika
kwake rasmi.
“Lakini sasa tumelazimika kuanza kutekeleza sheria
hiyo mapema kuliko tulivyopanga hasa baada ya kutokea kwa suala hili
kwenye public (umma) kabla ya muda tuliokuwa tumekusudia,”alisema
mkurugenzi huyo.
Isaka aliongeza kuwa chimbuko la sintofahamu
iliyojitokeza ni baadhi ya mifuko kuchezeana rafu kwa lengo la kupata
wanachama wapya kwenye migodi na kwamba wao kama wadhibiti tayari
wametoa onyo kwa mifuko iliyohusika.
“Kwanza hakuna mfuko wowote
ambao una mamlaka ya kutangaza kuanza kutumika kwa sheria, ni SSRA tu
wenye mamlaka hayo, kwa hiyo tumewapa onyo, kama wanajitangaza
wajitangaze kwa kueleza uzuri wa mfuko wao ni siyo kuchafuana au
kuchafua wengine,” alisisitiza.
Wasemavyo wafanyakazi
Mgaya
alisema sheria hiyo ni kandamizi kwani inamnyima fursa mfanyakazi
aliyestaafu au kufukuzwa kazi kupata malipo yake ambayo ni halali.
“Sheria
hii sisi hatuikubali na tunaipinga kwa nguvu zote na tutakwenda
Mahakama ya Kazi kufungua kesi ya kupinga kutumika,” alisema Mgaya na
kuongeza:
“Tutafanya mawasiliano na Kamati ya Bunge ya Huduma za
Jamii kuwaeleza kuhusu sheria hii ili watusaidie na ikishindikana azma
yetu ni kwenda mahakamani.”
Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba
haiwezekani mtu anafukuzwa kazi akiwa na miaka 45 na baadhi yao hawataki
tena kuajiriwa wanataka kufanyabiashara halafu unamnyima mafao yake
hadi afikishe miaka 55, kitu ambacho kitamfanya mtu huyo aishi maisha
magumu.
“Sheria hiyo ingekuwa na usawa ingetumika kwa wafanyakazi
wote wa Serikali na kutowabagua kama inavyojieleza kwamba, Mbunge
akimaliza miaka yake mitano anachukua mafao yake. Sasa kwa nini iwe
kwao tu na si kwetu pia?,” alihoji Mgaya.
Kwa upande wao Chama
cha Wafanyakazi wa Migodini (Tamico) Wilaya ya Geita, kimesema
kitapeleka maombi maalumu kwa Rais Kikwete kupinga marekebisho ya Sheria
ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Katibu wa Tamico Wilaya ya Geita,
Benjamin Dotto alisema wameamua kupiga kura ya maoni juu ya mabadiliko
ya sheria hiyo, ili wanachama wao waamue wenyewe kama wanaitaka au la.
”Tunamwomba
Rais aagize kupelekwa muswada wa marekebisho bungeni, kwa ajili ya
kipengele ambacho kimeleta mtafaruku,” alisema Dotto.
Alisema
kipengele cha kuzuia mfanyakazi kuchukua mafao yake hadi afikishe umri
wa miaka 55, kinakandamiza masilahi ya mfanyakazi mnyonge ambaye kwa
kiasi kikubwa amekuwa akichangia mapato ya nchi kupitia kodi anayokatwa.
Chimbuko la sheria
Mabadiliko
ya sheria hizo za mifuko ya hifadhi ya jamii yalifanywa na Bunge Aprili
13 mwaka huu, baada ya muswada husika kuwa umesomwa kwa mara ya kwanza
bungeni Februari 1, 2012.
Ibara ya 107 ya muswada huo ndiyo
ilipendekezwa kufutwa kwa Ibara za 37 na 44 za Sheria ya Mfuko wa
Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) ambavyo vilikuwa vikiruhusu mafao ya
kujitoa.
Meneja uhusiano wa SSRA Sara Mssika alisema jana kuwa
kufutwa kwa ibara hizo kulimaanisha kwamba hakuna mfuko wowote
unaoruhusiwa kutoa tena mafao ya aina hiyo hadi hapo miongozo mipya
itakapotolewa.
“Hakuna sheria ya mfuko mwingine iliyokuwa
ikiruhusu mafao ya kujitoa, na kama wapo waliokuwa wakifanya hivyo, basi
walikuwa wanafanya hivyo pengine kwa taratibu nyingine ambazo ni nje ya
sheria za kuanzishwa kwa mifuko yao,”alisema Mssika.
Waziri wa
Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka akiwasilisha maelezo ya muswada huo
bungeni alisema lengo la marekebisho katika Sheria za Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii ni kuiwezesha SSRA kufanya kazi yake kikamilifu na kusimamia na
kudhibiti Sekta ya Hifadhi ya Jamii.
Alisema muswada huo
uliandaliwa kwa kuwashirikisha wadau wote wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii,
wakiwamo wafanyakazi, waajiri na Serikali, pia
mifuko yenyewe kupitia vikao vya wadau na Baraza la Ushauri wa Masuala ya Kazi Jamii na Uchumi.
“Kimsingi,
wadau wote waliunga mkono mapendekezo yaliyomo katika muswada huu,”
alisema Kabaka na kuongeza kuwa mabadiliko hayo yatawezesha kupanuliwa
kwa wigo wa wanachama kwenye mfuko kwa kuruhusu wafanyakazi wanaoingia
kwenye ajira kwa mara ya kwanza ama kujiajiri wenyewe ili waweze
kujiunga.
Chanzo cha Habari ni Mwananchi
No comments:
Post a Comment