NJOMBE

NJOMBE

Wednesday, October 17, 2012

Jeshi lapambana na Boko Haram Nigeria


Luteni Kanali Sagir Musa anasema kuwa washukiwa wanne wa Boko Haram walikamatwa katika msako uliofanywa usiku kucha.

Jeshi nchini Nigeria limesema limewaua washukiwa 24 wa kundi haramu la Boko Haram mjini Maiduguri Kaskazini mwa Nigeria.
Wanajeshi waliziba barabara kuu mjini humo baada ya kutokea msururu wa milipuko na milio ya risasi usiku kucha.
Kwa mujibu wa Jeshi, Boko Haram walishambulia kambi za jeshi.
Mwalimu wa shule ya msingi aliuawa huku mnara wa kupeperushia matangazo ya redio ukichomwa.
Mapema mwezi huu, walioshuhudia makabiliano kati ya jeshi na washukiwa wa Boko Haram, walisema kuwa wanajeshi waliwapiga risasi raia 30 baada ya shambulizi la bomu dhidi ya kambi ya jeshi mjini Maiduguri.
Katika tukio la hivi karibuni, ripoti zinasema kuwa wanajeshi walifunga karibu kila barabara mjini wakati mashambulizi yalipoanza Jumatatu adhuhuri na kuendelea hadi masaa ya usiku.
Walioshuhudia tukio hilo wanasema kuwa mapema Jumatatu mtu aliyekuwa amejihami alishambulia kwa risasi polisi aliyekuwa anashika doria mjini humo karibu na kizuizi barabarani.
Mapema mwezi huu, wanajeshi mjini Maiduguri, waliwashambulia watu baada ya kutokea shambuli la bomu na kumuua mwanajeshi mmoja.
Walichoma maduka ya watu pamoja na nyumba.
Jeshi lilikana mauaji hayo ingawa waandishi wa habari wanasema kuwa lilitoa maelezo ya kina kuhusu kilichotokea
Mashambulizi Kaskazni mwa Nigeria ambayo yamefanywa na Boko Haram yamesababisha vifo vya watu 1,400 tangu mwaka 2010.
Maiduguri ndiyo ngome kuu ya Boko Haram ambao wanapigania kile wanachosema ni sheria za kiisilamu kutumika nchini humo.

No comments:

Post a Comment