NJOMBE

NJOMBE

Thursday, October 25, 2012

SHAMUHUNA – HUKUSHIBA KWAKO, UTASHIBA KWA JIRANI?

ShamhunaHadithi hadithi! Hapo zamani za kale paliondokea kitumbili. Kitumbili majaliwa. Kitumbili huyu alikuwa na rafiki yake ambae ni jirani wa nyumba ya pili tu kutoka kwao. Sasa wakati wa kula kitumbili akila kwao bila kumuita rafiki yake. Lakini wakati wa kula kwa rafiki yake Kitumbili majaliwa alikuwa ndie wa kwanza kudaka tonge. Na kwa maana hii dadithi yangu imekomea hapa.
Hadithi hii ya kale imepata kuimbwa sana. Na kwa wenye kumbukumbu nzuri wanakumbuka kuwa Bi Shakila kule Tanga enzi zile, aliimba ‘Kitumbili majaliwa, wala kwenu nala kwetu, na kwetu wajajaliza’. Taswira hii ya kisanaa inajitokeza tena machoni mwetu mara tu Waziri wa Elimu wa Zanzibar Mh. Shamuhuna anapotangaza kuleta Walimu wa Sayansi kutoka Nigeria.
Tamko la Waziri Shamuhuna linanipa mashaka mengi . Shaka ya kwanza ni kuwa sioni haja ya mwiba uliochomea mguuni kutolewa ulimini. Na hivi ndivyo anavyofanya Shamuhuna sasa. Kabla hajsema mwiba ulipochomea anautafuta kwenye ulimi autoe ilhali akijuwa kuwa huko siko ulikochomea.
Tukubaliane kuwa taifa letu hili dogo, Zanzibar, lina uhaba wa Walimu. Nani asiejuwa. Lakini kwanza hili la uhaba wa walimu linashuhulikiwaje kabla ya kuomba kwa jirani tena kwa gharama gharika? Kuna haja ya kujiuliza kuwa jee ni kweli walimu ni haba au kuna jengine? Maana nionavyo, walimu wapo lakini kutokana na sera duni na mishahara vibutu, ukikorogea na siasa potofu, walimu hao wengi hukimbilia nchi jirani au ughaibuni kusomesha. Hili halijapatiwa ufumbuzi tunatafuta gharama nyengine zisizo na sababu wala adabu.
Wahitimu wa shahada na diploma pale SUZA na Chukwani, ukiachilia walio na vyeti vya ualimu kule Mkapa, Chuo Cha kiislamu Mazizini, na Kule Pemba Kiuyu, wangetosha tangu kuanzishwa vyuo hivyo vikuuu mapema miaka ya 2000 hapa nchini. Lakini kinachojitokeza hapa ni kuwa wahitimu kadhaa waliondoka kwenda bara na huku Serikali ikijua lakini ikanyamza kimya. Jirani (Bara) kajaza kijungu kwa makopa yatokayo nyumbani kwetu. Hii ndio ajizi ya viongozi vitumbili majaliwa. Tuliache la walimu wetu wanaokimbia kwetu kwenda kwa jirani.
La kusikitisha zaidi hapo katikati tulikuja kufanya mchezo mmoja mchafu wa kijinga wa kuajiri walimu kiudalali. Walimu kadhaa hasa wa shule za msingi hapa Zanzibar ambao ni wapya kidogo wengi wao wameajiriwa kwa mlango wa nyuma bila kuwa na sifa, kwa makubaliano na maafisa wa juu wa Wizara ya elimu wa kugawana mshahara kwa miezi sita na kisha mwalimu huyo ‘pyoro’ anaendelea kusomesha kama mwalimu halali. Hivi kuajiri wasiokuwa walimu huwa tunamdanganya nani na tunategemea nini? Hivi ndio tutapata walimu wa sayansi kwa kuajiri ndugu zetu walitoroka chuoni na skuli wakiwa darasa la sita? Hili mbona halijashuhulikiwa tunatafuta walimu kwengine wakati tumewaajiri wengi kama hawa?
Kwa upande mwengine,si vibaya hata kidogo kuleta walimu wa kigeni hapa nchini lakini shaka yangu nyengine iko hapa. Kwanini tuagizie walimu wa Sayansi badala ya kutayarisha wetu wenyewe na kuwajengea mazingira mazuri badala ya kutumia gharama nyingi kuleta wageni kwa mambo ambayo sisi wenyewe tunaweza kuyafanya kwa gharama nafuu na hata kwa kujitolea? Pili, ikibidi lazima tulete walimu wa Sayansi, kwanini lazima iwe Nigeria? Kunani Lagos na Abuja? Nanusa harufu ya kivundo fulani hivi Wizara ya Elimu kwa hili.
Tunaelewa fika kuwa Nigeria wenyewe yao yanawashinda na dunia nzima inawatambua kama ni watu wasio na radhi wala kubadhi, na isitoshe hawasarifiki kama ngozi ya futi. Juu ya hayo, sioni kama ni mabingwa wa sayansi wa kiasi cha Shamuhuna kuona lazima wawe wao tu na awaajiri kwa magharama na karama. Kuna kitu kimejificha hapa. Kipapo hatukiona lakini tuendelee kunukiliza harufu itatoka tu.
Kwa upande mwengine, naamini kuna masomo yanahitaji walimu kutoka nje. Kwa mfano, masomo ya lugha ya kiingereza na zile lugha za kigeni ingekuwa vyema tukifunga mikataba na balozi zilizopo nchini wakawa wanatuletea wataalamu wa kufundisha lugha kama ilivyokuwa zamani. Tuliweza na tukapata vijana wazuri wasiofanana na Mulugo kwa kujua lugha. Hili Shamuhuna hakuliona au tuseme halitaki.
Kwa sasa suala liko wazi, kuita walimu hao wa kigeni ambao sijui kama watatosha kwa skuli zote hizi za hapa kwetu, na hata wakitosha bado ni gharama kubwa kwa taifa ambalo linahangaika kutafuta suluhisho la tatizo kwa mbinu zisizohusiana na tatizo lenyewe. Kama tunaona kuna uhaba wa walimu wa Sayansi, jee hili tumeanza kuliona lini? Hakuna mpango wa elimu wa muda mrefu huko Wizarani? Na kama hauko jee hata tathimini ya miaka kumi hadi ishirini iliyopita haikutoa bishara ya kuwepo kwa uwezekano huu wa kujitokeza tatizo hili? Ukweli ni kwamba hakuna lolote linalofanywa na ndio sasa tunashika hili na lile, mambo yameshaharibika.
Kwa uoni wangu, mie sioni haja ya kuleta wataalmu hao kutoka Nigeria kwani bado tunahitaji muda wa kutathimni na kuangalia undani na chanzo cha tatizo hili. Tunahitaji kuandaa mipango bora ya utatuzi wa matatizo kama haya na pia kuhakikisha kuwa tunabuni mkakati na pembejeo za kuwafanya walimu wetu wa hapa ndani na walio nchi jirani kuvutika kuja kusomesha kwetu kwa hiari zao na sio kuletwa hapa kama wataalamu wasio kuwa na taaluma chochote. Naamini cha thamani au kizuri hakupi jirani yako. Na mtaalamu wa kweli wa Sayansi hakai tu kule Kaduna, Umuofia, Lagos, au Kano Nigeria akisubiri Shamuhuna aje amuajiri.
Wataalamu wa nchi zote duniani hasa hasa waNigeria, ni ngumu kuwapata kirahisi kama anavyofikiri yeye Shamuhuna. Na hili wenzetu wa ulaya wanalijua vyema na ndio ukaona kila mtaalamu huchukuliwa hapa Afrika akatumikie Ulaya na Marekani. Sasa leo unaposema unaenda Kaduna, Abuja, Kano ukamchukuwe mwalimu wa Sayansi mtaalamu umlete Zanzibar, ambapo mwalimu hulipwa chini ya dola 100 kwa mwezi, sipati picha. Na isitoshe Muheshimiwa Shamuhuna kama hujashiba kwako, na kwa jirani hushibi. Tuachie kwa hili, kuna mengi ya kufanya sema tukusaidie.

No comments:

Post a Comment