NJOMBE

NJOMBE

Wednesday, October 31, 2012

Njia za kujenga uwezo wa kujiamini



Ni vigumu kuelezea moja kwa moja kujiamini maana yake nini? Lakini mtazamo wa mwanadamu juu ya namna wenzake wanavyomchukulia inaweza kuwa kutafsiri ya neno kujiamini. Ikiwa utajilinganisha na wengine na hatimaye kuhisi aibu, ujue unakabiliwa na tatizo la kujiamini.
Kimsingi kuna mambo mengi yanayoweza kumfanya mtu asijiamini mbele ya wenzake, kiasi cha kujiona duni kwa hili na lile na wakati mwingine hali hiyo humfanya ashinde kufanya hata mambo ambayo anayajua na kwamba amekuwa akiyafanya kila siku
Kisaikolojia huu ni ugonjwa ambao unaweza kuathiri uwezo wa mtu kibaiolojia, nikimaanisha kwamba mtu anaweza kuwa si mlemavu wa miguu, lakini akatembea mbele za watu upande upande, anaweza kuwa na akili lakini akajikuta hawezi kuzitumia kwa sababu si mwenye kujiamini.
Kama ilivyo kwa magonjwa mengine, kuponywa kwa tiba, tatizo hili la kutokujiamini nalo linatakiwa litibiwa. Zipo njia nyingi ambazo mtu anaweza kuzitumia kujenga hali ya kujiamini, Kwangu mimi yako  mambo 10 ya msingi ambayo mtu akiyazingatia na kuyafanyia kazi anaweza kuondokana na hali ya kutokujiamini.
Kuchagua mavazi
Ingawa mavazi hayatafsiri moja kwa moja hali ya mtu, lakini katika lugha ya mawasiliano yasiyokuwa na sauti uvaaji wa mtu ni utambulisho wake. Hivyo kama mtu hazingatii uvaaji unaokubalika katika jamii anakuwa katika wakati mgumu wa kujiamini, hasa kama akilini mwaka yeye mweyewe atatambua kuwa amevaa vibaya.
Hii ina maana kwamba kama mtu anataka kujenga hali ya kujiamini, lazima achague mavazi yanayoendana na mazingira na yawe ni mavazi ambayo mwenyewe akiyafikiria yahatamfanya ajione ni wa tofauti kwa wenzake. Mavazi hujenga muonekano, ukionekana vizuri mbele za watu utajiamini, hivyo kuwa makini na uchaguzi wa mishono ya nguo unazovaa kila siku.
Kutembea haraka
Njia rahisi ambayo imethibitika kuweza kumuondolea mtu hali ya kutokujiamini ni kutembea kwa mwendo wa haraka. Haipendezi unapokuwa njiani kutembea kama mgonjwa, uliyechoka. Ukiwa hivyo ni rahisi sana kuwafanya watu wakukodolee macho ambayo yatakufanya wewe uhisi tofauti. Utemebeaji wa haraka una faida nyingi, lakini kubwa kabisa ni kuwafanya watu wengine wakuone wewe ni mtu wa kazi usiyetaka kupoteza muda wako, mtu makini na mwenye mipamgo. Kitaalamu mwendo unaoruhusiwa ni wa asilimia 25, usizidi sana kiasi cha kuonekana kama unakimbia.
Muonekano sahihi
Namna mtu mwenyewe anavyouweka mwili wake linaweza kuwa ni tatizo la kumfanya ashindwe kujiamni. Kwa mfano,mtu kama si mlemavu lakini akajikuta anatembea miguu upande, mabega juu, kichwa chini au juu sana au kutembea akiwa anadundika kama mpira, ni vibaya kwa vile kitalaamu huchangia kumuondolea mtu ujasiri mbele za watu.
Ushauri wangu ni kwamba mtu anatakiwa kuupa mwili wake umuhimu na kuuweka kama alivyoumbwa, haifai kuwa mtu wa kuinama na kuficha uso, kusimama tenge pale unapoitwa au kuwa mbele za watu. Si vema pia kung�ata kucha, kujipapasa mwilini au kutazama pembeni. Ni vizuri kila mtu kulinda muonekano wake wa asili mbele za wenzake.
 Kujizoeza kujiamini
Njia moja muhimu sana kisaikolojia ya kujenga hali ya kujiamini ni kupenda kusikiliza maneno ya kutia moyo nay a ujasiri kutoka kwa watu maarufu. Kwa mfano, viongozi wenye msimamo, watetezi wa haki za binadamu, wanasiasa wanaotetea maslahi ya nchi bila hofu na kadhalika. Hotuba na maneno yao yakipata sehemu kubwa katika akili ya mtu, lazima yatajenga hali ya kujiamini kama wale anaowasikiliza.
Kukubali matokeo
Ifahamike kuwa ukiwaza kwa kina sana juu ya mahitaji yako, zao litakalofuata hapo ni akili kukuletea sababu za kishindwa kufanikisha mambo unayoyataka. Sababu hizo ukizipa nguvu sana ya kuziwaza zitakupa jibu la haiwezekani. Unapokuwa na mawazo yenye mlango huo wa kutokufanikiwa, uwezo wako wa kujiamini hushuka na kujikuta unashindwa katika mambo uyafanyayo. Katika maisha lazima mtu akawa na wakati wa kuachia mawazo yake na kukubaliana na matokeo yaliyopo hasa pale hali ya kushindwa inapokuwa kubwa.
Kupingana na wengine
Mtu akijiona duni mwenyewe ni rahisi kwake kudhani kuwa watu wengine ndiyo wenye mambo ya kweli na hivyo kujikuta akifuata mkumbo na kupotoshwa katika ukweli. Ili mtu aweze kuwa sahihi katika mawazo ya vile ananvyoamini ni lazima awe na tabia ya kupingana na wenzake. Ni jambo baya kukubaliana na watu katika mawazo yao bila kupinga katika kile unachoamini, kufanya hivyo kunaweza kuyafanya maneno ya uongo ya wengine yakaaminika na kuuacha ukweli wa mtu asiyejiamini ukipuuzwa kwa sababu tu hakuwa na ujasiri wa kukabiliana na hoja za wenzake.
7. Pendelea kukaa mbele

Katika kujenga hali ya kujiamini ni vizuri zaidi unapokuwa shule, ofisini, kwenye mikutano, semina ukawa na tabia ya kuketi nafasi za mbele. Ni ukweli kuwa, watu wengi hawapendi kukaa sehemu za mbele kwa sababu ya hofu ya kuonekana kwa urahisi na pengine kuwa wa kwanza kuulizwa au kuchangia hoja, tabia hiyo huondoa hali ya mtu kujiamini. Ili kujenga ujasiri ni vema mtu akapendelea kuketi vitu vya mbele na mara nyingi kuwa wa kwanza katika kufanya mambo.
Zungumza bila aibu
Ukimya wa kupita kiasi nao ni tatizo, hasa pale linapokuja suala la kuogopa kuzungumza mbele za watu kwa hofu ya kuonekana hujui. Wapo wanafunzi na wasomo wengi wanapokutana katika vikundi vya mazungumzo maarufu kama Groups Discusions huwa hawapendi kuzungumza wakilenga kujificha na aibu itokanayo na udhaifu wao katika uelewa. Hata hivyo kutochangia mazungumzo na wengine hakuna faida zaidi ya hasara kwa mtu kutoweza kujiamini. Inashauriwa kwamba ili mtu aweze kujenga hali ya kujiamini ni vema akajenga mazoea ya kuongea mbele za watu bila aibu.
Kujenga afya
Kipengele cha kulinda afya ni muhimu sana kwa mtu anayetaka kujenga hali ya kujiamini. Kukonda au kunenepa sana umbo kunaweza kumfanya mtu akajiona wa tofauti na hivyo kupoteza hali ya kujiamini. Hivyo basi kama unakonda hakikisha kuwa unakula vyakula vyenye vitamini ili kuufanya mwili wako usiwe kituko kwa wengine, hali kadhalika kama unanenepa sana fanya mazoezi ili kuupunguza mwili wako. Tafuta afya ili uwe na nguvu za kufanya mambo kwa umakini.
Msaada kwa wengine
Baada ya kufanikiwa katika hatua zote ambazo tumeziangalia hapo juu, jambo jingine la muhimu katika kuhitimisha uwezo wa mtu kujiamini ni kupata msaada wa mawazo kutoka wa watu wengine ambao ni makini katika maisha yao. Kama kuna jambo ambalo linakuwa gumu katika mawazo yako na limekosa ufumbuzi kiasi cha kukufanya usijiamini, washirikishe wengine wakusaidie  na kukutia moyo wa kuendelea kukabiliana na hali yakutojiamini.

No comments:

Post a Comment