NJOMBE

NJOMBE

Saturday, October 20, 2012

JESHI LAINGILIA KATI KUWADHIBITI WAANDAMANAJI, NI WAISLAMU WALIOKUWA WAKITAKA KWENDA IKULU ZANZIBAR BADO SI SHWARI, MWINGINE AFA KWA RISASI

 JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jana liliingilia kati kusaidia kurejesha amani, kutokana na vurugu zilizosababishwa na baadhi ya waumini wa Kiislamu, ambao jana walipanga kufanya maandamano kwenda Ikulu.
Magari ya JWTZ yalianza kuonekana mitaani mchana baada ya swala ya Ijumaa, yakitokea wilayani Temeke na kwenda katika maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam, hasa yale yaliyotajwa kuwa na vurugu.
Mabomu ya machozi yalitupwa katika maeneo mengi hasa Kariakoo na Magomeni, ambako waumini hao walikuwa wakijipanga kuanza maandamano baada ya swala ya mchana.
Mapema, Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na wale wa kawaida wakiwa mabomu ya machozi na gari lenye maji ya kuwasha, walionekana karibu na Misikiti ya Idrisa uliopo Kariakoo na Kichangani wa Magomeni.
Msikiti wa Kichangani mahali ambako huwa anaswali Katibu wa Jumuiya na Taasisi za  Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda anayetuhumiwa kuongoza harakati za kile kinachodaiwa kuwa haki za Waislamu nchini.
Ponda pamoja na wafuasi wake 49, juzi walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka kadhaa yakiwamo ya wizi na uchochezi.
 Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana kuwa hali ya usalama ilikuwa imedhibitiwa na kwamba hakuna polisi wala raia aliyekuwa ameripotiwa kujeruhiwa.
Kova alisema kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa wamekamatwa kutokana na vurugu hizo, wakiwamo 20 ambao ni wakazi wa Zanzibar ambao walikamatwa wilayani Temeke, baada ya kuhisiwa kuwa walikuwa na lengo la kushiriki katika vurugu.
“Tumewakamata na wanadai kwamba walikuja Dar es Salaam kwa ajili ya michezo, sasa tunaendelea kuwahoji na baada ya kukamilisha kazi hiyo tutafahamu kwamba kweli ni wanamichezo na walikuja hapa kwa mchezo upi, hatuwezi kuwahukumu sasa kwamba ni wana Uamsho,” alisema Kova.

Mauaji Zanzibar



Visiwani Zanzibar, vurugu ziliendelea, huku mtu mmoja akidaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia jana.
Habari zilizopatikana zinasema mtu huyo, Salum Hassan Muhoja (30), mkazi wa Regeza Mwendo nje kidogo ya Mji wa Zanzibar alipigwa risasi karibu na eneo la Amaan.
Inaaminika kuwa mtu huyo alipigwa risasi wakati akipita karibu na baa na nyumba ya kulala wageni, Mbawala Amaan ambayo ilivunjwa katika ghasia hizo.
Kijana huyo alitarajiwa kuzikwa jana jioni kijijini kwao Mwera, Regeza Mwendo, Wilaya ya Magharibi Unguja.
Kuuawa kwa kijana huyo kumetokea siku moja baada ya askari wa FFU, CPL Said Abdulrahman kuuawa kwa mapanga na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Kikundi cha Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki).
Wakati kukiwa na habari hizo za mauaji, jana vijana kadhaa waliingia barabarani eneo la Darajani na kupambana na askari wa doria ambao walikuwa wametanda katika eneo hilo.
Vijana walikuwa  wakiimba: “Tunamtaka amiri wetu, tunamtaka amiri wetu, tunamtaka amiri wetu,” huku wakiwarushia mawe polisi, kabla ya kutawanywa kwa mabomu ya machozi.
Polisi walitupa mabomu ya machozi na kufyatua risasi katika mitaa mbalimbali ya Zanzibar kila kulipokuwa na mikusanyiko, hivyo kuufanya mji huo kusikika milio ya risasi na mabomu. Barabara kadhaa zikifungwa kwa muda kutokana na hali hiyo.
Uwepo wa JWTZ
Kamanda Kova alipoulizwa kuhusu kuwapo kwa askari wa JWTZ katika operesheni za polisi, alisema wanajeshi hao walikuwa katika kazi zao nyingine.
“Hawa nao ni askari na wanahusika na ulinzi na usalama wa nchi, kwa hiyo sisi tulifanya kazi yetu, lakini askari hawa wa JWTZ hawakuwa sehemu ya operesheni yetu. Kimsingi kazi yote tumefanya sisi,” alisema.
Msemaji Mkuu wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe kwa upande wake, alisema hakuwa anafahamu chochote kuhusu kuwapo kwa askari wa jeshi hilo katika operesheni ya kudhibiti vurugu hizo.
“Kwa kawaida kama askari wanahitajika kusaidia operesheni zozote zile, basi mawasiliano huanzia kwa mawaziri na baadaye kushuka kwa viongozi wetu akiwamo Mkuu wa Majeshi kwa ajili ya utekelezaji,” alisema Kanali Mgawe na kuongeza: “Sasa niseme kwamba katika hili la sasa, mimi kweli sifahamu chochote.”
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya jeshi hilo zinasema kuwa kuwapo kwa askari hao kulitokana na ombi la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadik ambaye aliomba liwe tayari kusaidia endapo polisi wangezidiwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, viongozi wa jeshi hilo walikubaliana na ombi hilo hivyo kupeleka baadhi ya askari kutoka Vikosi vya 34 KJ cha Lugalo na 511KJ cha Gongo la Mboto ili kuongeza nguvu katika kudhibiti vurugu hizo.
Habari zaidi zinadai kuwa, wanajeshi hao waliwekwa tayari kwa lolote kwa wiki mbili kabla ya tukio hilo la jana.
Wanajeshi hao wa JWTZ, walionekana wakifanya doria hasa katika maeneo ambayo yalikuwa na ishara za vurugu, lakini hawakufanya chochote kwa maana ya kuwadhibiti watu.
Pamoja na kwamba hawakufanya chochote, wananchi waliokuwa katika makundi katikati ya jiji walikuwa wakitawanyika na kuondoka katika sehemu hizo, kila walipowaona.
Mbali na askari hao, pia polisi walitumia helikopta kukagua jinsi operesheni za udhibiti zilivyokuwa zikifanyika katika sehemu mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam.
Chanzo cha vurugu
Taarifa za kuwapo kwa maandamano na vurugu zilianza kusikika tangu juzi usiku na kusambaa zaidi jana asubuhi.
Kadhalika, kabla ya kuanza kwa swala ya Ijumaa kulisambazwa vipeperushi katika baadhi ya misikiti, vilivyokuwa vikiwahamasisha waumini hao kuandamana kwa amani kwenda Ikulu baada ya swala hiyo.
Vipeperushi hivyo vilikuwa na maandishi yanayoeleza sababu za maandamano hayo kuwa ni pamoja na kukamatwa kisha kufikishwa mahakamani Sheikh Ponda na kutojulikana aliko Kiongozi wa Kundi la Uamsho Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed.
Sheikh Farid anadaiwa kwamba alitekwa na polisi. Hata hivyo, jeshi hili limekanusha kufahamu aliko kiongozi huyo. Kadhalika, vipeperushi hivyo vilieleza kwamba maandamano hayo yalikuwa ni kwa ajili ya kupinga kitendo cha kukojolewa kwa Quran, kitendo kinachodaiwa kufanywa na mtoto mwenye umri wa miaka 14 mkazi wa Mbagala, ambaye alifikishwa mahakamani katikati ya wiki hii. Awali, tukio hilo lilisababisha vurugu na uhalifu wa uchomaji wa makanisa saba pamoja na wizi wa mali kadhaa katika makanisa hayo.
Watu 126 walikamatwa katika sakata hilo na kati yao 35 walifikishwa mahakamani.

Misikitini
Katika Msikiti wa Kichangani uliopo Magomeni, Imamu wa msikiti huo, Alhaji Wallid Alhad, alipigwa na baadhi ya waumini pale alipowataka kutofanya maandamano kwa maelezo kwamba hayakuwa na tija.
“Wekeni hasira zenu chini na mkitoka humu msiweke vikundi kwani Sheikh Ponda kakamatwa na yuko chini ya dola na jana (juzi), alifikishwa mahakamani ambako haki itatendeka,” alisema Alhaji Walid.
Alisema Sheikh Ponda yupo katika hali nzuri mikononi mwa Serikali na haki itatendeka.
Kutokana na kauli hiyo, waumini walimgeukia na kuanza kumwandama, hivyo kuzusha vurugu ndani ya msikiti huo... “Haiwezekani... huyo anatumika kuzuia maandamano, ametumwa na watu wasio utakia mema Uislamu acha tumpige,” ilisikika sauti ya mmoja wa waumini.
Hata hivyo, waumini hao waligawanyika na baadhi yao walimkingia kifua na walifanikiwa kumtoa nje na kumwondoa kwa nguvu katika eneo la msikiti huo kwa gari.
Katika Msikiti wa Mtambani, Kinondoni kabla ya swala ya Ijumaa, Imamu wa msikiti huo alisikika akiwahamasisha waumini wake kutoogopa polisi na kwamba anayepaswa kuogopwa ni Allah.
Baada ya swala hiyo, wakati wanajiandaa kufanya maandamano hayo, Polisi waliwadhibiti walipofika eneo la Kinondoni kwa Manyanya kwa kuwatawanya kwa baruti.
Katika Msikiti wa Idrissa, Kariakoo, Imam wa Msikiti huo baada ya swala ya Ijumaa alianza kuwahamasisha waumini wake kufanya maandamano kwenda Ikulu kwa kutumia Barabara ya Msimbazi karibu na Kituo cha Polisi Msimbazi.
Walipofika karibu na kituo hocho, walizuiwa na askari na kuanza kurusha mawe ambayo yalijibiwa kwa mabomu wa machozi. Hali hiyo ilidumu kwa takriban dakika 15.
Iliwalazimu polisi kuongeza nguvu kwani mbali na magari matano yaliyokuwa na polisi wa kutuliza ghasia, waliwasili wengine wapatao 16 wakiwa kwenye pikipiki nane.
Baada ya swala ya jioni kundi kubwa la waumini lilirejea tena barabarani na polisi waliamua kutumia maji ya kuwasha na kuwakamata baadhi ya watu waliokuwa katika kundi hilo.
Barabara, maduka vyafungwa

Baada ya kumalizika kwa swala hiyo ya Ijumaa, askari kanzu na polisi wakiwa na silaha pamoja na mabomu ya machozi, walifunga Barabara ya Morogoro eneo la Magomeni Mapipa ili kuwadhibiti waandamanaji.
Kadhalika, polisi waliamuru maduka yanayozunguka misikiti iliyokuwa ikiashiria vurugu yafungwe na watu waliokuwa katika makundi waliamriwa kutawanyika.
Kufungwa kwa barabara kulisababisha wafanyakazi na watu waliokuwa katikati ya Jiji la Dar es Salaam kukwama kurudi nyumbani.
Magari yaliyokuwa katikati ya jiji wakati barabara hizo zikifungwa hayakuweza kutoka na yale yaliyokuwa nje hayakuruhusiwa kuingia.
Hali kama hiyo pia iliyakumba maeneo ya Kariakoo ambako hadi saa 11:00 jioni hali ilikuwa tete kutokana na shughuli za uchumi kusimama na magari ya abiria yalishindwa kufanya kazi zake.
Timu ya Mwananchi iliyokuwa ikitembelea maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, ilishuhudia watu wakiwa wamejazana katika vituo vya daladala katika maeneo ya Fire, Kariakoo, Akiba, Mnazi Mmoja, Posta Mpya, Kivukoni na Posta ya zamani, huku wengine wakitembea kwa miguu kurejea nyumbani.

Benki zafungwa
Huduma katika benki mbalimbali katikati ya jiji pia zilisitishwa kwa muda kuhofia ghasia hizo.
Baadhi ya matawi ya benki zilizosimamisha kwa muda shughuli zake pamoja na  CRDB, Standard Charted, Benki ya Posta, Benki ya Wanawake, NMB na Barclays.
Hata hivyo, huduma za ATM za bemki hizo zilikuwa zikiendelea kama kawaida.
Ulinzi uliimarishwa katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi zilizopo Barabara ya Ohio, Wizara ya Fedha na Ofisi za Bunge zilizopo Barabara ya Shaaban Robert.
Pia ulinzi kama huo uliwekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Dar es Salaam kwa hofu kwamba kingeweza kuvamiwa.
Askari wa FFU na kanzu walionekana wakirandaranda nje ya majengo ya taasisi hizo baadhi yao wakiwa wamebeba silaha.
Watu waliokuwa wakitaka kuingia katika maeneo hayo hasa Mambo ya Ndani, walizuiwa. Hiyo ilitokana na tetesi kwamba kuna Kundi la Waislamu ambalo lilipanga kuandamana hadi hapo kushinikiza wenzao waliokamatwa na kufunguliwa kesi kuachiwa.
Katika kuimarisha ulinzi maeneo hayo, wafanyabiashara ambao kwa kawaida hufanya shughuli zao pembezoni mwa majengo hayo waliamriwa kuondoka.
Katika lindo hilo, watu watatu wanaosadikiwa kuwa miongoni mwa waandamanaji walikamatwa karibu na Jengo la Wizara ya Fedha wakidaiwa kuelekea Ikulu.
Hofu yatanda
Hofu ilitanda kutwa nzima ya jana kutokana na mabomu na risasi zilizokuwa zikisikika katika maeneo ambayo watu walikataa kutii amri ya polisi.
Habari ambazo hata hivyo hazikuthibitishwa zilizopatikana jana jioni zinadai kuwa katika vurugu zilizotokea kwenye Msikiti wa Kichangani, Magomeni mtoto mmoja alipoteza maisha.
Hata hivyo, Kamanda Kova alisema hakuwa amepata taarifa hizo hadi jana jioni... “Inawezekana tukio likawapo, lakini hadi sasa sijapata taarifa hizo kwa sababu kama unavyofahamu, mambo ni mengi na mkoa huu ni mkubwa.”

Sheikh wa Mkoa akemea

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema maandamano hayo yalitaka kuharibu sura ya Uislamu.Alisema Uislamu ni dini ya amani na utulivu na kwamba hata Mtume Muhammad (SAW), alihimiza watu kuvumiliana na kuishi na watu wengine kwa amani.
Alisema anaamini watu wanaoujua Uislamu hawawezi kufanya vitendo vinavyoharibu sifa njema ya Uislamu.
Sheikh Salum aliwataka Waislamu kote nchini kuwa wavumilivu akisema ndiyo njia pekee itakayotoa haki kwa wale wote wanaoshikiliwa akiwamo Sheikh Ponda.
“Nawasihi Waislamu wenzangu, jambo hili la kukamatwa kwa watuhumiwa hawa limetendwa na vyombo vya usalama, tukiendelea na vurugu kunaweza kuwanyima haki watuhumiwa hao na hata wakafanyiwa vitu vibaya, tuwe wavumilivu na tusubiri haki itendeke,” alisema alipohojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika Habari la Uingereza (BBC).
Hata hivyo, Sheikh Salum alisema tayari viongozi wa Dini ya Kiislamu wakiwamo Kamati ya Amani ya Maimamu imekutana jana kuona jinsi ya kumaliza vurugu hizo kwa njia za amani.

Mapadri mafichoni
Hofu hiyo pia ilisababisha mapadri na watumishi wengine wa Kanisa Katoliki Parokia na vituo vilivyopo Mbagala, Dar es Salaam waliondolewa haraka jana asubuhi, kukwepa vurugu ambazo zingeweza kutokea.
Habari zilizopatakana zilisema kuwa viongozi hao wametakiwa kuondoka katika maeneo ya kanisa ili kuepuka lolote ambalo lingetokea.
Akizungumza katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mbagala, mmoja wa watumishi wa kanisa hilo alisema nako wahusika wameamriwa kuondoka na baadhi ya mali zilihamishwa kuhofia kuchomwa.
Mbali na hayo, habari zilizopatikana jana zilidai kuwa, usiku wa kuamkia jana, polisi walizuia jaribio la kuchoma kanisa moja maeneo ya Mtoni Kijichi na inadaiwa wahusika na jaribio hilo wanatafutwa na polisi.
Visiwani Zanzibar, Kiongozi wa Kanisa la Anglikana  Zanzibar, Askofu Michael Hafidhi alidaiwa kukimbilia mafichoni kuhofia usalama wake.
Akizungumza na BBC jana, Askofu Hafidhi anayeongoza makanisa sita visiwani humo alisema alifikia uamuzi huo baada ya kupata ujumbe wa vitisho kutoka kwa wafuasi Jumuiya ya Uamsho.
“Jana nilitumiwa ujumbe wa vitisho kutoka Uamsho, nikaamua kuondoka kuja mafichoni. Muda mfupi tu baada ya kuondoka walifika nyumbani kwangu Mkunazini na kufanya vurugu,” alisema.
Askofu huyo alisema watu hao pia wameanza kumtishia Askofu wa Kanisa Katoliki, Agustino Shayo ambaye ameandikiwa ujumbe wa baruapepe ya kitisho.
Mapema jana asubuhi, zilienea taarifa kuwa Kundi la Uamsho kutoka Zanzibar lilikuwa njiani kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kuongeza nguvu katika maandamano.
Hali hiyo ilifanya FFU kupiga kambi bandarini eneo linalotumiwa na boti kwa ajili ya kupakia na kuteremsha abiria wanaokwenda na kutoka Zanzibar. Hata hivyo, hadi mchana hakukuwapo na taarifa zilizothibitisha kuingia kwa kundi hilo.
Visiwani Zanzibar
Hali ilianza kuchafuka jana saa 8:00 mchana wakati kikundi cha vijana kilichokuwa kimejikusanya eneo la Uwanja wa Malindi kuingia barabarani, huku wakipiga kelele za kutaka Amiri wao, Farid Hadi Ahmed ambaye alitoweka tangu Jumanne iliyopita atolewe ‘mafichoni’.
“Kupotea” kwa sheikh huyo ndiko kulikozua ghasia Zanzibar hapa tangu Jumatano na kufanya mji usikalike, huku biashara zote zikifungwa na askari mmoja kuchinjwa Jumatano usiku na kijana mwingine kupigwa risasi jana.
Wafuasi wa Sheikh huyo wanaamini kwamba kiongozi wao amekamatwa na Serikali. Hivyo, walitaka kushinikiza aachiwe huru. Barabara za mjini zilikuwa zimejaa takataka za kila aina kuanzia vifusi, mawe makubwa, matairi yaliyochomwa moto, matofali na vifuu vya madafu.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Said Juma Hamis alisema hana taarifa za kuuawa kijana huyo zaidi ya zile za kuuawa kwa askari wao Bububu.
Kamanda Hamis alisema kuwa hadi jana, watuhumiwa waliokuwa wamekamatwa kutokana na vurugu hizo walikuwa 39 na wanane kati yao, walifikishwa mahakamani jana na wengine wanaendelea kuhojiwa na polisi.
Kaimu kamanda huyo pia alisema jeshi hilo linaendelea na juhudi zake za kumtafuta kiongozi huyo wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu, Sheikh Farid ambaye anadaiwa kutekwa.
Alisema katika kufanikisha juhudi hizo jana kulifanyika kikao cha wapelelezi kilichoongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi Zanzibar, ACP Yussuf Ilembo kujadili suala hilo.

Vipindi vya Uamsho marufuku
Katika hatua nyingine, Tume ya Utangazaji ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepiga marufuku vipindi vyote kwenye redio na televisheni vya Kikundi cha Uamsho.
Barua iliyotumwa jana kwa wakurugenzi wa vituo vya redio na televisheni Zanzibar ilisema kwamba hatua hiyo imetokana na ghasia zinazoendelea ambazo zinasadikiwa kuwa zinachochewa na kikundi hicho.
Barua hiyo ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji, iliyosainiwa na Mtumwa Mzee kwa niaba yakeilisema itawachukulia hatua wale wote watakaokaidi agizo hilo.

Waandishi hatarini
Waandishi wa habari waliopo mjini Zanzibar kwa lengo la kufuatilia ghasia zinazoendelea hapa, wamekuwa kwenye hatari kwa kutishiwa maisha yao na vijana wanaofanya vurugu.
Makundi yanayofanya vurugu yako ya aina tatu Ubayaubaya, Kimyakimya na Mbwamwitu ambayo hufanya vurugu na kupora watu mali zao ikiwamo kwenye vyombo vya usafiri na kuvamia baa.
Waandishi wa habari wakiwamo wa kimataifa walivamiwa na moja ya kundi la vijana hao na kuwekwa chini ya ulinzi eneo la Mbuyuni na kutaka kuwanyang’anya vifaa vyao vya kazi, lakini waliokolewa na walinzi waliokuwa jirani.

Vipeperushi Zanzibar
Vipeperushi vinavyotishia uhai wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar vimesambazwa mjini Unguja.Kipeperushi kimojawapo kinahimiza kuvunjwa kwa ushirikiano huo baina ya CCM na CUF, huku vingine vikiwatuhumu baadhi ya mawaziri kutoka CUF kwamba ni chanzo cha fujo na vurugu zinazoendelea.

Baraza la Wawakilishi
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CCM jana waliendelea kugoma kuingia katika baraza hilo, ili kuishinikiza Serikali kuchukua hatua za haraka za kumaliza machafuko na kurejesha hali ya usalama Zanzibar.
Wajumbe wa baraza hilo ambao hawana nyadhifa serikalini kutoka kambi ya CCM walianza mgomo wao juzi jioni na kususia vikao vinavyoendelea na kumlazimisha Spika Pandu Ameir Kificho kuahirisha kikao kwa muda wa dakika tano ili kutoa fursa ya majadiliano jana asubuhi.
Kwa mujibu wa Mnadhimu wa CCM ndani ya Baraza la Wawakilishi, Salmin Awadh Salmin wajumbe kutoka chama hicho wamefikia uamuzi huo wa kugomea vikao kutokana na vurugu zinazoendelea na kutaka Spika akubaliane na hoja binafsi ya kujadili hali ya kisiasa Zanzibar jambo ambalo Spika alikataa.
Hata hivyo, baada ya ushauriano kati ya viongozi wa Serikali, Spika na wajumbe hao wa CCM, walikubali kurudi na kuendelea na vikao. Wajumbe hao walikuwa 45 ambao waliishutumu Serikali ya Zanzibar wakidai kuwa imeonyesha udhaifu mkubwa katika kuwahakikishia wananchi wake usalama.
Waliwataka Mkuu wa Jeshi ya Polisi nchini IGP, Said Mwema pamoja na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa kuwajibika kwa madai kwamba wameshindwa kutekeleza wajibu wao na kuacha hali tete ya usalama ikiendelea.
Chanzo cha habari na Mwananchi picha na Makali Machechi

No comments:

Post a Comment