NJOMBE

NJOMBE

Wednesday, October 24, 2012

JK aingia woga na rushwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi


•  Amtumia Mwandosya kujisafisha

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dr Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia

HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kueleza mshangao wake kuhusu vitendo vya rushwa kupenya katika chaguzi zinazohusisha wanawake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imepokewa kwa hisia tofauti na makada wa chama hicho na wadadisi wa masuala ya siasa, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Kikubwa kinachoonekana kuwashtua wafuatiliaji wa siasa ndani ya CCM ni hatua ya Rais Kikwete kutoa kauli ya mshangao pasipo kuonekana akichukua hatua zozote za kukabiliana na vitendo vya rushwa ambavyo yeye mwenyewe anakiri kwamba vinahatarisha uhai wa chama hicho.
Mmoja wa makada wa muda mrefu serikalini na ofisa wa juu mstaafu wa moja ya taasisi nyeti za dola, amelieleza Tanzania Daima Jumatano kwamba, kauli ya Kikwete imeonyesha namna kiongozi huyo anavyojitanabahisha kwa namna tofauti na ilivyopata kufanywa na watangulizi wake watatu.
Ofisa huyo ambaye kama walivyo wengine wanne waliozungumza na waandishi wa gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa kwa majina yao, alisema Rais Kikwete ambaye ndiye mwenyekiti wa taifa wa CCM alipaswa kutoa kauli ya kukemea, karipio na yenye mamlaka dhidi ya wagombea wanaotoa rushwa katika chaguzi zinazoendelea ndani ya chama hicho.
Kwa mujibu wa ofisa mwingine mstaafu, kitendo cha rais kutoa kauli zinazobadilika badilika kuhusu rushwa huku akiwa na mamlaka ya kuwachukulia hatua watuhumiwa wa vitendo hivyo hususan ndani ya serikali na katika vikao vya chama anavyoviongoza, ni dalili za woga wa kuchukua maamuzi sahihi.
“Rais wangu ni mtu wa kushangaza na mwoga. Amepata kusema anawafahamu wala rushwa kwa majina. Ni huyu huyu aliyewahi kutamka kuwa siku za wala rushwa zinahesabiwa na leo anasema eti anashangaa kusikia hata wanawake wanajihusisha na rushwa katika uchaguzi,” alisema kada mwingine mwandamizi ndani ya CCM.

Duru za siasa kutoka ndani na nje ya chama hicho tawala, zinasema kuwa kwa hali ilivyo sasa, CCM inaweza kufa kama isipofanya mabadiliko makubwa yatakayosaidia kudhibiti hali hiyo.
Tangu kuanza kwa uchaguzi huo wa chama hicho ngazi ya shina hadi taifa, kumekuwa na malalamiko kila kona ya kukithiri kwa vitendo vya rushwa, huku watuhumiwa hao wakipitishwa na vikao vya juu na kuibuka na ushindi.
Tayari baadhi ya vigogo walioanguka katika uchaguzi wa ndani ya CCM katika ngazi tofauti, wamekuwa wakizungumza chini kwa chini kwamba kuongezeka kwa kasi ya vitendo vya rushwa ndani ya chama imetokana na udhaifu wa Rais Kikwete kushindwa kuchukua hatua kudhibiti hali hiyo.
Akihutubia Mkutano Mkuu wa Nane wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) wa CCM juzi, Rais Kikwete aliishia kuonya juu ya vitendo vya rushwa vinavyozidi kushamiri ndani ya chama hicho, akisema kuwa visipochukuliwa hatua mapema, kuna hatari ya kukifikisha chama katika hatua mbaya.
Hakuishia hapo, alikwenda mbele zaidi na kusema, imekuwa ni hulka sasa hasa baada ya kumalizika chaguzi kwa wanachama kuendeleza na kuwekeana uhasama kama uliokuwepo wakati wa kampeni na wengine kuwaadhibu ambao hawakuwachagua hali ambayo ni mbaya sana kwa mustakabali wa chama.
Rais Kikwete aliwaasa wagombea wa nafasi mbalimbali wa UWT walioshindwa kutoweka visasi na walioshinda kutowapiga vijembe walioshindwa kwani kazi iliyo mbele ni kubwa kutokana na CCM hivi sasa kukabiliwa na hali ngumu ya ushindani wa kisiasa.
“Kweli tusipokemea vitendo hivi na kuviacha vikiendelea, tutakipeleka chama mahali pabaya, ninasikitika sana kusikia hata wanawake sasa wanajihusisha na utoaji rushwa ili kununua nafasi za uongozi kitu ambacho ni hatari sana,” alisema Kikwete.
Alifafanua kuwa chama kinapoelekea si kuzuri ni lazima zifanyike jitihada za mabadiliko.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete ameonyesha kutishwa na nguvu na kasi kubwa ya vyama vya upinzani.
Alisema wakati CCM ikichafuka kwa rushwa, vyama vya upinzani vimekuwa vikijiimarisha kisiasa hali ambayo inakifanya chama chao kiwe katika wakati mgumu.
Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete alizihimiza jumuiya za chama hicho kuongeza juhudi na kujipanga kupambana na hali hiyo kwa lengo la kuiwezesha CCM kushinda uchaguzi wa mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment