NJOMBE

NJOMBE

Thursday, October 4, 2012

Uchunguzi waakhirishwa Afrika Kusini

Tume inayochunguza mauaji ya Marikana
Tume ya kuchunguza mauaji ya wachimba migodi nchini Afrika Kusini, imetoa muda kwa mawakili kushauriana na jamaa za waliouawa
Wakili mmoja wa familia kadhaa za waathiriwa, alisema kuwa sio wachimba migodi wote waliouawa wamezikwa na kwa hivyo hakupata muda wa kuwasiliana na familia zao.
Makamishna wa tume hiyo, tayari wamezuru eneo la mauaji karibu na mgodi wa Marikana unaomilikiwa na kampuni ya Lonmin
Majasusi na wataalamu wa uchunguzi wa mauaji wanatarajiwa kutoa ushahidi wao.
Tume hiyo yenye makamishna watatu, pia itachunguza mauaji ya wachimba migodi wengine kumi akiwemo polisi mmoja aliyeuawa wakati wa vurugu katika mgodi huo.
Siku hiyo ya mauaji inasemekana kuwa mojawapo ya siku zilizosuhudia ghasia mbaya kuwahi kutokea tangu kumalizika kwa enzi ya utawala wa ubaguzi wa rangi ,mwaka 1994.
Ghasia hizo zilianza kufuatia vuta ni kuvute ya mishahara kati ya wachimba migodi na wamiliki wa migodi hiyo.
Tume hiyo ina vikao vyake katika ukumbi mmoja ulio karibu na eneo la mauaji Kaskazini Magharibi mwa Johannesburg.
Rais Jacob Zuma ndiye aliunda tume hiyo punde baada ya mauaji kutokea. Inaongozwa na jaji mstaafu wa mahakama ya rufaa, Ian Farlam.
Tume hiyo itachunguza namna ambavyo polisi, wamiliki wa mgodi, vyama vya wafanyakazi na serikali walivyohusika na mauaji hayo.
Tume hiyo inatarajiwa kutoa tathmini yake kuhusu mauaji hayo katika muda wa miezi minne, huku ripoti yake ya mwisho ikitolewa mwezi mmoja baadaye.
Takriban watu 46 waliuawa katika ghasia hizo ambazo zilifanyika wakati wa wiki moja ya vurugu kwenye mgodi wa Marikana.

No comments:

Post a Comment