NJOMBE

NJOMBE

Sunday, October 7, 2012

Chadli Bendjedid aaga dunia


 
Chadli Bendjedid
Chadli Bendjedid
Aliyekuwa rais wa Algeria kwa miaka mingi, Chadli Bendjedid, ambaye anasifika kwa kuanzisha mfumo wa utawala wa kidemokrasia katika taasisi za kiserikali nchini humo, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 83.
Ripoti zinasema Bendjadid, aliaga dunia kutokana na maradhi ya saratani baada ya kulazwa katika hospitali ya kijeshi ya Ain Naajda mjini Algiers tangu wiki iliyopita.
Januari mwaka huu, Bendjadid, alipelekwa nchini Ufaransa kwa matibabu ya saratani na tangu wakati huo amezuru hospitali mara kadhaa.
Bendjadid ameandika vitabu kadhaa vya kumbukumbu ambayo vinatarajiwa kuchapishwa tarehe Mosi mwezi ujao, siku ambayo raia wa nchi hiyo wanaadhimisha kumbukumbu ya kuanza kwa vita vya uhuru wa taifa hilo.
Alihudumu kama rais wa Algeria, tangu mwaka 1979 hadi mwaka wa 1992 na kuandikisha historia ya kuwa rais wa nchi hiyo aliyehudumu kwa kipindi kirefu zaidi.
Bendjadid aliondolewa madarakani wakati jeshi la nchi hiyo lilipoingilia kati kuzuia ushindi wa wapiganaji wa Kiislamu, katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini humo.
Kufuatia uamuzi huo wa jeshi wa kuingilia kati masuala ya kisiasa, vita vikali vilizuka nchini humo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu laki mbili.
Bendjedid alikuwa miongoni wa wapiganaji wa uhuru wa taifa hilo kutoka kwa utawala wa kikoloni kati ya mwaka wa 1954 na mwaka wa 1962 na aliteuliwa kuwa kamanda wa jimbo la Oran Magharibi mwa nchi hiyo kwa miaka 14.
Alijiunga na vugu vugu la mapinduzi, lililoundwa Juni mwaka wa 1965, kumuondoa madarakani rais wa kwanza wa nchin hiyo Ahmed Ben Bella.
Huku akiungwa na jeshi la nchi hiyo, Bendjedid, alichaguliwa kuwa rais wa mwaka wa 1979 na mwaka wa 1989 alichaguliwa tena kwa muhula mwingine, miezi miwili tu baada ya ghasia na machafuko za kulalamikia kuongezeka kwa bei ya bidhaa muhimu na pia kuitisha kuanzishwa kwa utawala wa kidemokrasia.
Bendjedid anasifika kwa kuanzisha utawala wa kidemokrasia nchini humo pale alipoidhinisha mabadiliko ya kikatiba Februari mwaka wa 1989.
Lakini baada ya kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, rais huyo wa zamani alihukumiwa kifungo cha nyumbani katika eneo lake la Oran, mwaka wa 1992.
Hukumu hiyo ilifutiliwa mbali wakati rais Abdelaziz Bouteflika alipochaguliwa rais mwaka wa 1999.
Bendjedid alizaliwa Aprilo 14, 1929 katika eneo la Bouteldja, Mashariki mwa Algeria karibu na mpaka wa Tunisian.

No comments:

Post a Comment