NJOMBE

NJOMBE

Saturday, October 20, 2012

Magufuli agundua ufisadi unaofanyika kupitia magari ya Serikali


WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli, ameanzisha operesheni maalumu  ya kukamata magari ya umma yanayotumia namba za kiraia, baada ya kubaini kuwa yanatumika kufisidi fedha za Serikali.Waziri huyo pia ameahidi kuwachukulia hatua kali waliouziwa magari ya Serikali na bado wanatumia namba zile zinazoonyesha kuwa yanamilikiwa na Serikali.

Alitoa onyo hilo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huku akiahidi kuendesha operesheni kali ya kuhakikisha wote waliokiuka taratibu wanawatiwa mbaroni.

"Operesheni hii itahusisha  magari yote ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Wakala wa Serikali, Mashirika ya Umma na taasisi nyingine za umma," alisema Magufuli.

Alisema hivi karibuni Serikali ilibaini kuwapo kwa magari ya umma yaliyosajiliwa kwa namba za kiraia na yanatumia namba hizo kwa manufaa binafsi na hivyo kuisababishia Serikali hasara.

Dk Magufuli alisema kwa kuzingatia hali hiyo, atahakikisha kuwa utaratibu wa usajili wa magari ya umma  unafuatwa.

“Serikali  itafanya operesheni maluum ya kurejesha  usajili wa magari yote ya umma kwenye utaratibu,” alisisitiza waziri huyo maarufu katika kusimamia sheria zinazohusu wizara yake.

Alisema Serikali inatoa muda wa hadi kufikia Novemba 15 mwaka huu magari ya umma yenye  namba za kiraia, yarejeshwe kwenye namba stahiki za magari hayo.
"Baada ya hapo, tutatumia  vyombo vya ulinzi na usalama katika kukamata magari, pikipiki, bajaj na mitambo ya umma na tunawaomba wananchi watusaidie kwa kutoa taarifa,"alisema Dk Magufuli.

Dk Magufuli alisema Serikali iliweka utaratibu  unaozuia matumizi ya namba za kiraia kwenye magari, pikipiki, bajaj na mitambo yake na kwamba hata hivyo utaratibu huo sasa umekiukwa.
Alisema Sheria  ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973, inaipa mamlaka, Wizara ya Ujenzi kusajili na kutunza kumbukumbu za magari yote ya Serikali  ambayo yatapewa namba zitakazotanguliwa na JW, PT,ST, MT,CW na DFP.
Alisema  magari, pikipiki, bajaj na mitambo ya umma itakayokamatwa, itapelekwa katika maeneo ya vituo vya polisi ama karakana za Tamesa mikoani na maeneo ya idara za ujenzi wilayani.

Alisema wanaohusika kusimamia na kufanikisha zoezi hilo ni makatibu wakuu wa wizara zote, makatibu tawala wa mikoa yote, wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote, watendaji wakuu wote wa taasisi na idara za serikali na watanzania wote.

No comments:

Post a Comment