NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, October 16, 2012

Pombe,Sigara Na Ukahaba Marufuku Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepiga marufuku biashara ya ukahaba, matangazo yote ya pombe na uvutaji wa sigara katika mikusanyiko ya watu katika visiwa vya Unguja. Hayo yamebainika kufuatia marekebisho ya kifungu cha sheria cha 112, cha mswada wa sheria kuhusiana na hifadhi na usimamizi wa vihatarishi vya afya ya jamii na afya ya mazingira na mambo yanayohusiana na hayo iliyopitishwa ndani ya Baraza la Wawakilishi jana.Waziri wa Afya Zanzibar Juma Duni Haji aliwaambia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba kutokana na michango mingi ya wajumbe kutaka suala la matangazo ya pombe, uvutaji wa sigara, na biashara ya ukahaba vipigwe marufuku, serikali imekubaliana na maoni ya wajumbe hao. Waziri Duni amesema, kuanzia sasa kwa mujibu wa sheria hiyo itakuwa ni marufuku kutangaza au kushajiisha matangazo ya pombe kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo ufadhili au matamasha ya muziki na starehe katika visiwa hivyo. Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman alisema anakubaliana na maoni ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuondoa kabisa matangazo ya pombe na kwamba serikali imefanya vyema, kwani hivi sasa Shirika la Afya Duniani WHO, Umoja wa Ulaya EU na baadhi ya nchi ikiwemo Sweden tayari zimezuia matangazo ya pombe na Zanzibar kufuata sheria hiyo ni jambo la busara.

No comments:

Post a Comment