WILAYA ya Ileje mkoani Mbeya imetajwa kuwa miongoni mwa wilaya nchini
zinazotisha kwa wanawake wajawazito kutojifungulia hospitali na vituo vingine
vya afya licha ya kuhudhuria kliniki katika kipindi chote cha ujauzito.
Hali hiyo imebainishwa na Meneja Uwezeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya (NHIF) Dk. Mathias Sweya katika mkutano wa kupanua uelewa kwa viongozi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ileje juu ya mradi wa kuwasaidia wanawake wajawazito
wasio na uwezo kupata huduma za matibabu chini ya utaratibu wa NHIF na Mfuko wa
Afya ya Jamii (CHF).
Dk. Sweya alitolea mfano kwa Kituo cha Afya cha
Sange kilichopo wilayani hapa ambapo katika mwaka 2011 wanawake 137 walihudhuria
kliniki kituoni hapo, lakini kati yao ni 34 pekee waliojifungua hapo.
Alisema uchunguzi unaonesha kuwa gharama za vifaa vinavyopaswa
kununuliwa kwa mama mjamzito zinachangia kwa kiasi kikubwa wanawake
kutojifungulia kituoni hapo.
Hata hivyo, mmoja wa maofisa maendeleo
wilayani Ileje, Lucy Mwani akichangia hoja alisema yapo mambo mengi yanayopaswa
kuchunguzwa ili kupata sababu ya wajawazito kutohudhuria kliniki ukiachilia
mbali gharama akitaja baadhi kuwa ni pamoja na mila potofu.
Mwani
alishauri kurejeshwa kwa Mpango wa Uhai, Ulinzi na Maendeleo ya Mama na Mtoto
(CSPD) akisema uliwezesha kupatikana kwa taarifa za haraka juu ya mama mjamzito
na mwenendo wa maisha yake tangu dalili za mimba hadi kujifungua pamoja na
changamoto anazokumbana nazo.
No comments:
Post a Comment