Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
WAKATI
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akianza kugusa hisia za watu
wanaomtaka agombee ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, mwenyekiti
wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema iwapo mtendaji mkuu huyo wa chama
ataamua kuwania kiti hicho, wataheshimu uamuzi wake.
Wakati Mbowe
akitoa kauli hiyo, aliyepeperusha bendera ya Chadema katika uchaguzi wa
mwaka 2010, Joshua Nasari na kutoa upinzani mkali kwa mgombea wa CCM,
marehemu Jeremiah Sumari, naye amesema kama katibu mkuu wake ataamua
kuwania kiti hicho, hatakuwa na pingamizi ikiwa chama kitaamua kwani
lengo ni kutwaa jimbo hilo.
Akizungumza na Mwananchi jana baada
ya kuibuka mjadala kuhusu uwezekano wa Dk Slaa kuwania jimbo hilo, Mbowe
alisema, "Katika suala la kugombea, utashi binafsi ni jambo la
msingi...,kama Dk Slaa ataamua kugombea ubunge Arumeru Mashariki,
tutaheshimu uamuzi wake."
Mbowe alisema katika uteuzi wa chama,
kuna vigezo vinavyoangaliwa ikiwa ni pamoja na jinsi mtu anavyokubalika
kwa wananchi anakogombea, sifa zake na utashi wake binafsi na kuongeza,
"Hatuna uteule katika chama."
Hata hivyo, Mbowe alisema Chadema
hakiwezi kumlazimisha Dk Slaa akagombee jimbo hilo kama mwenyewe utashi
haumtumi kufanya hivyo, na kwamba hana shaka na kukubalika kwa katibu
mkuu huyo kutokana na imani aliyojijengea kwa umma wa Watanzania.
Mbowe
alisema Dk Slaa amekuwa akiombwa kugombea ubunge katika maeneo mengi
likiwamo Jimbo la Igunga, lakini chama kisingeweza kumlazimisha kwani
jambo la kwanza ilibidi mwenyewe aonyeshe utashi binafsi wa kutaka
kuwania kiti hicho.
"Dk Slaa aliwahi kuombwa akagombee Igunga,
lakini hakwenda. Hii ni kwasababu anakubalika nchini karibu kote, hivyo
kama atakuwa na utashi binafsi kwanza, nadhani taratibu za chama
zitatumika tu kufikia uamuzi," alifafanua.
Mwenyekiti huyo wa
Chadema pia alitoa angalizo kwamba, wakati mwingine uamuzi wa chama
kupata mgombea unaangalia jinsi mgombea alivyo na mtandao katika jimbo
analotaka kugombea ili hata kama akichaguliwa aonekane ni mbunge wa eneo
hilo.
"Ndiyo maana nasema kuna vigezo vingi tu, kwa mfano mtu
anaweza kuwa mbunge mzuri bungeni, lakini je, ana connectivity
(kinachomuunganisha) jimboni, kuangalia kama ana makazi na mtandao
mwingine kwani asije akawa mbunge mzuri bungeni, lakini jimboni akiwa
kama mgeni hivyo watu wakaona kama kimewapelekea pandikizi
tu,"alifafanua Mbowe.
Tangu juzi kumekuwa na mjadala katika
mitandao ya kijamii huku baadhi wakimtaka Dk Slaa akagombee ubunge
Arumeru Mashariki kuziba pengo la aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo,
Marehebu Sumari, lakini wengine wanapinga na kumtaka aendelee kubaki na
nafasi yake ya katibu mkuu wa chama kwa lengo la kukijenga.
Hata
hivyo, Dk Slaa ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 alishika nafasi
ya pili akiwa nyuma ya Rais ya Jakaya Kikwete, juzi alinukuliwa na
gazeti moja la kila siku (siyo Mwananchi) akisema, "Siwezi kulizungumzia
jambo hilo, maana nilikwisha kusema muda mrefu kuwa sitaki tena ubunge
na isitoshe mimi si mwenyeji wa Arumeru,"
Katibu Mkuu Chadema Dr.Willibrod Slaa
Joshua Nasari
Kwa
upande wake Nasari (26) ambaye ana mtaji mkubwa wa kura kufuatia matokeo
ya uchaguzi wa mwaka 2010 alitoa msimamo wake akisema yupo tayari
kufanya mazungumzo na viongozi wa juu ya chama chake juu ya kumpisha Dk
Slaa kuwania ubunge katika jimbo hilo kama akihitaji.
Nasari
ambaye amerejea hivi karibuni mjini Arusha akitokea nchini Marekani, leo
anatarajiwa kuchukua fomu rasmi ili kuwania nafasi hiyo kupitia
Chadema.
"Nimesikia maoni kupitia mitandao na wadau wakimuomba Dk
Slaa kugombea, hili ni jambo jema kwetu kwani wananchi wanajua jimbo
hili tunashinda Chadema na kama Dk (Slaa) akitaka kugombea dekomrasia ya
chama chetu itafanya kazi, kwani kikubwa tunataka ushindi,"alisema
Nasari.
Nasari aliyewahi kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) kati ya 2008 na 2009
alipohitimu shahada ya Sayansi ya Jamii katika masuala ya utengenezaji
Sera na Utawala, alisema ana imani Chadema kitashinda Arumeru.
"Nilikuwa
Marekani kikazi na sasa nimerejea kama ulivyoshuhudia watu wengi
wananiunga mkono na tayari wamenichangia Sh 11milioni za kampeni na
magari manane," alisema Nasari.
Mgombea huyo ambaye tayari
ametangaza kuacha kazi katika shirika la Kimarekani la Foundation For
Tomorrow ili kujikita kwenye uchaguzi huo, alisema wakazi wa Arumeru
Mashariki wanahitaji mwakilishi sahihi ambaye anaweza kuwatetea katika
kuinua uchumi wao.
Hata hivyo, alisema tayari amepata taarifa za
Dk Slaa kutoa tamko kuwa hawezi kushiriki katika uchaguzi huo, kwa
kuzingatia kuwa sio mkazi wa Meru na pia hana nia ya kugombea kiti
hicho.
"Nategemea Dk Slaa na viongozi wengine wa kitaifa,
wakiwapo wabunge, marafiki zangu wa vyuo vikuu na wengine wengi tutakuwa
nao Arumeru kuhakikisha Chadema inashinda,"alisema Nasari.
Hadi
kufikia jana, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema
Mkoa wa Arusha (Bavicha), Ephata Nanyaro, wanachama waliokuwa
wamechukua fomu ni Yohane Kimuto, Samweli Chami na Rebecca Mwingisha na
leo Nasari atakuwa mwanachama wa tatu.
"Tunatarajia wanachadema
wengi zaidi watajitokeza katika siku hizi zilizobaki ili kuchukuwa fomu
na kurejesha mapema,"alisema Nanyaro.
Mgombea CCM alalamikia rushwa
Katika
hatua nyingine, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM katika Wilaya ya
Nyamagana mkoani Mwanza, Elirehema Kaaya ambaye pia ni afisa wa mifugo
mkoani Mwanza, amekitaka chama hicho kukemea kampeni za fedha ndani ya
chama katika uchaguzi huo.
Kaaya ambaye pia aligombea jimbo hilo
katika uchaguzi uliopita na kushindwa katika kura za maoni ndani ya
CCM, alisema wakazi wa Arumeru hawahitaji mgombea wa CCM ambaye anapata
nafasi hiyo kwa kutumia fedha.
"Arumeru wanataka mtu wa
kuwasemea matatizo yao mjengoni (bungeni) na sio mtu anayetumia fedha
kupata ubunge na mimi naomba chama kikemee na kukomesha matumizi ya
fedha,"alisema Kaaya.
Akizungumzia maombi hayo, Katibu wa CCM
Wilaya ya Arumeru Edson Lihweuli alionya mgombea yoyote ambaye
atabainika kujihusisha na vitendo vya rushwa au kukiuka taratibu
atachukuliwa hatua.
Lihweuli alisema wagombea wote ambao
wamechukua fomu, wamekuwa wakipewa taratibu hizo ili kuhakikisha
uchaguzi ndani ya chama hicho unakwenda vizuri.
Wakati
huohuo, Mkuu wa shule ya Sekondari ya Leguruki inayomilikiwa na Jumuiya
ya Wazazi ya CCM, Mwalimu Athony Msami jana alijitokeza kuchukua fomu
na kufanya wagombea wa chama hicho wanaomba ridhaa ya chama kufikia
sita.Wengine waliokuwa wamechukuwa fomu ni Sioi Sumari, mtoto wa
aliyekuwa mbunge Jeremiah Sumari, William Ndeoya Sarakikya, Elipokea
Urio, Elishiria Kaaya na Elirehema Kaaya.
Wakati kada huyo wa
CCM akichukua fomu, juzi jioni Mkurugenzi wa kituo cha Mikutano cha
Arusha(AICC), Elishiria Kaaya alirejesha fomu na kueleza kuwa anagombea
ili kutekeleza ilani kwa kushughulikia matatizo ya wananchi wa Meru.
Kaaya
ambaye pia aligombea uchaguzi uliopita na kuangushwa katika kura za
maoni na Marehemu Sumari, alisema miongoni mwa mambo ambayo atayasimamia
ni kuhakikisha anashirikiana na wananchi kukabiliana na matatizo ya
upatikanaji maji, barabara, huduma za afya na masuala ya elimu.
Takukuru yaanza kazi
Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Arusha imekutana na
wagombea waliojitokeza kuchukua fomu katika uchaguzi huo na kuwaonya
kutojihusisha na rushwa pia kuwataka waheshimu sheria za gharama za
uchaguzi.
Takukuru pia imetamka kwamba tayari imeshashaanza
kupokea malalamiko mbalimbali ya makada wa vyama tofauti vya siasa
wilayani humo, kujihusisha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa na
kwamba madai hayo yameanza kufanyiwa kazi.
Taarifa iliyotolewa na
Kamanda wa Takukuru mkoani Arusha, Mbengwa Kasumambuto imesema katika
kujipanga kukabiliana na rushwa katika uchaguzi huo taasisi hiyo
imekutana na wagombea wote wa vyama hivyo kwa lengo la kuwatahadharisha.
“Katika
kujipanga na uchaguzi wa Arumeru kwanza tumewaita wagombea ambao
wameshajitokeza hadi sasa pamoja na viongozi wa vyama vyao, lengo ni
kuwatahadharisha na kuwataka waheshimu sheria ya uchaguzi,”alisema
Kasumambuto.