Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
Ikulu, Dar es Salaam . Picha na Emmanuel Herman
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amezungumzia mambo muhimu kumi na moja yanayogusa
nchi kwa sasa yakiwemo ya kiuchumi na kisiasa huku akiwashangaa wanaotumia nguvu
nyingi kuwania nafasi ya urais akisema hawajui mzigo mkubwa wa kuongoza taasisi
hiyo.
Katika mkutano wake na wahariri na wawakilishi wao uliofanyika
ofisini kwake Dar es Salaam jana, Pinda alisema: “Kwa dhati sifikirii kugombea
nafasi hiyo ya juu kwani ni mzigo mkubwa.”
Alisema kuna watu wanautaka
urais kwa nguvu na kuhoji kama wanajua mzigo mkubwa uliopo katika taasisi hiyo
au wanafurahia mazingira yake ili wakanufaike kiuchumi na
kibiashara.
“Kuna watu wanautaka kweli urais... wanautaka kwelikweli,
lakini kuutaka na kuupata ni vitu tofauti. Sijui kama wanautaka ili wawatumikie
Watanzania au kwa sababu tu ya mazingira mazuri yaliyopo pale ili waweze kufanya
biashara au wanufaike kiuchumi.”
Alisema mtu anayejua mzigo mkubwa uliopo
Ikulu kamwe hawezi kuutaka kama baadhi wanavyofanya: “Wakati mwingine huwa
nikienda Ikulu namwambia ndugu yangu Rais pole. Ikulu ni mzigo
mkubwa.”
“Sasa hawa wanaoutaka kwa nguvu, ni kweli wanataka kwenda kubeba
mzigo huo mzito ? Mimi siko tayari. Sasa wanaoutaka urais kwa nguvu labda wawe
wanakwenda pale kufurahia mazingira ya Ikulu kama kufanya biashara lakini si
kutumikia Watanzania.”
Alisema Watanzania wanahitaji Rais ambaye atawatumikia
kwa dhati na anayejua matatizo yao na huyo ndiye ambaye wenyewe watamchagua
mwaka 2015 wakati wa uchaguzi.
Alisema anajivunia muda mwingi
alioutumikia umma tangu Ikulu na hadi nafasi ya Waziri Mkuu na kuongeza: "Sasa
hivi ni Waziri Mkuu. Hapa ni shule tosha najivunia kutumikia umma hadi hapa
nilipo. Panatosha nasema hili kwa dhati.”
Wakuu wa Wilaya
Waziri Mkuu
alikiri kuwepo wilaya ambazo zinakaimiwa na wakuu wa wilaya na kuongeza kwamba
mchakato wa kukamilisha uteuzi wao umeshakamilika na kinachosubiriwa ni
kutangazwa na Rais.
Alisema kuchelewa kukamilika kwa mchakato huo
kulitokana na matatizo ya kisheria katika baadhi ya maeneo, kwani kulikuwa na
mchakato wa kupokea maoni ya wapi kuwe makao makuu lakini, hilo na mengine
yamekamilika na anayesubiriwa sasa ni mkuu huyo wa
nchi.
Katiba
Akizungumzia mchakato wa Katiba, Pinda alisema Serikali
ina dhamira ya dhati kuhakikisha nchi inapata Katiba bora ambayo itagusa maslahi
ya makundi tofauti ya kijamii.
Alisema hivi sasa imeundwa timu ndogo ya
wataalamu ambayo itaangalia namna ya kufanya maandalizi ya kufanikisha utendaji
kazi wa tume ya kuratibu mchakato huo punde itakapoundwa.
Alifafanua
kwamba timu hiyo haina uhusiano wala haitafanya chochote kuhusu mapendekezo ya
uteuzi wala kuingilia mchakato wa kisheria wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa
mwaka 2011, bali itaangalia namna ofisi ya tume itakavyopatikana, maslahi kama
mishahara, vitendea kazi, magari na miundombinu ya mawasiliano katika
utendaji.
Pinda alisema timu hiyo ambayo imeundwa na Katibu Mkuu
Kiongozi, itafanya kazi hiyo kwa umakini ili kuhakikisha tume itakapoundwa na
kuanza kazi, maandalizi yote ya msingi yanakuwa yamekamilika.
Kuhusu
mapendekezo ambayo Rais amekuwa akiyapokea katika kipindi hiki ambacho tayari
sheria imekwishapitishwa na Bunge, alisema anasubiri maelekezo kutoka kwa mkuu
huyo wa nchi kuona kama kuna mapendekezo ambayo yanaweza kupelekwa bungeni na
sheria hiyo kufanyiwa marekebisho madogo ili kuhakikisha inakidhi matakwa ya
wadau wote.
Alisema dhamira ya Serikali na Rais ni kuhakikisha kwamba
Katiba inayopatikana inakuwa yenye matakwa ya pande zote husika, huku akitoa
mfano kwamba kama Chadema inataka Serikali tatu za katika muundo wa muungano
hilo litajulikana katika kura za maoni na kama CCM wanataka Serikali mbili pia
litajulikana katika kura za maoni.
Posho za wabunge
Akizungumzia posho
za wabunge, Pinda alisema tatizo kubwa lilijitokeza tangu mwanzo ni ukosefu wa
taarifa sahihi kwa umma hali iliyoibua mjadala na mgongano wa lugha kati ya
Spika wa Bunge, Anne Makinda na Katibu wake, Dk Thomas
Kashillilah.
Alisema wakati mjadala ulivyoibuka, ni kweli Spika
alimwandikia barua Rais kuomba nyongeza hiyo ya posho lakini mkuu huyo wa nchi
alikuwa bado hajaidhinisha posho hizo.
“Kwa hiyo, kwa lugha rahisi ingekuwa
ni kusema hivi... ni kweli tumeomba nyongeza ya posho kwa mheshimiwa Rais lakini
hadi sasa hajaidhinisha, atakapoidhinisha au vinginevyo tutasema. Lakini,
ikatokea huyu anasema hivi na yule hivi.”
Hata hivyo, alisema tayari Rais
Kikwete amekwisharejesha suala hilo kwake (Pinda) ili kuendelea na taratibu
nyingine zaidi ambazo atatoa maelekezo bungeni kuona namna ya kulimaliza suala
hilo bila mvutano.
Pinda alisema ingawa kumekuwa na malalamiko, lakini
wabunge wana matatizo ya msingi ambayo yanatokana na makato makubwa ya mikopo,
kusaidia wapiga kura majimboni na mengine mengi.
Alisema serikalini
kiwango cha posho ya vikao kwa siku kwa watumishi wa ngazi za juu ni Sh200,000
kwa ngazi ya kati Sh150,000 na nyingine Sh100,000 na kuongeza: “Hivyo, siyo
vibaya sana na hata wabunge wakiongezewa. Ni jambo linaloweza kueleweka kama
watu watalizungumza jambo hili kwa utulivu.”
Pinda alisema tofauti na
viongozi wa Serikali kama yeye, wabunge wanajigharamia wenyewe nyumba, magari,
mafuta, matengenezo na huduma nyingine za kuwasaidia wananchi, hivyo akataka
jambo hilo lizungumzwe bila jazba.
Uchumi
Akizungumzia mwenendo wa
uchumi, alikiri kwamba mfumuko wa bei ni tatizo kubwa linalotikisa nchini
lakini, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inafanya kila jitihada
kuhakikisha unashuka.
Alisema mfumuko huo umechangiwa na matatizo ya
uchumi wa dunia ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta ambayo kwa sasa pipa moja ni
Dola 100 za Marekani katika soko la dunia na matatizo ya mgawo wa
umeme.
Alisema kipindi cha Julai mwaka jana, mfumuko ulikuwa asilimia 13,
Septemba asilimia 16.8, na kushuka kidogo hadi 12.7 ikilinganishwa na asilimia
5.5 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2010.
Hata hivyo, alisema
mwelekeo wa ukuaji wa uchumi si mbaya kwani lengo kwa mwaka 2011 ilikuwa ni
ukuaji wa asilimia sita, lakini robo ya kwanza ya mwaka huo uchumi ulikuwa kwa
asilimia 6.8, ya pili asilimia 6.7 na robo ya tatu iliyoishia Septemba ilikuwa
kwa asilimia 6.3, hivyo kuonyesha uchumi mpana wa taifa bado uko
imara.
Alisema katika kipindi hicho, sekta ya ujenzi ilichangia kwa
asilimia 13.2 mawasiliano asilimia 12.9, sekta ya fedha asilimia 11.3 na sekta
ya biashara ilichangia kwa asilimia saba.
Kuhusu chakula, alisema
ingawa baadhi ya mikoa kama Arusha na Kilimanjaro mazao kama mahindi
yameathiriwa na ukame, bado uwezo wa nchi kujitosheleza kwa chakula kuelekea
kipindi cha Januari hadi Februari bado upo kwani maeneo ya kanda ya ziwa
yanatarajiwa kuzalisha mazao ya kutosha.
Akizungumzia mpango wa dharura
wa umeme uliopitishwa na Bunge alisema unaendelea vizuri ingawa hadi sasa
zimepatikana megawati 270 kati ya 300 zilizokuwa zimekusudiwa, ambazo ni sawa na
asilimia 90.
Katika Bunge la Bajeti la mwaka jana, Serikali iliomba Sh1.2
trilioni za mpango huo wa dharura wa kukabiliana na mgawo wa umeme, ambazo
zingeanza kuzalisha umeme kuanzia Agosti hadi Desemba, kwa awamu ya
kwanza.
Jairo
Kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge katika sakata la
aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo alisema kwa sasa
hatua za Serikali ziko Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ili atoe
mapendekezo yake ya kitaalamu.
Habari na Ramadhan Semtawa
No comments:
Post a Comment