MWENYEKITI wa kampuni za IPP, Reginald Mengi, amesema anakerwa na wapambanaji
wa ufisadi kunyamaza kimya kwa kile alichokiita kuhongwa na mafisadi au
wameanzisha mikakati inayolenga kuzorotesha nguvu ya vita dhidi ya ufisadi.
Licha ya Mengi kutowataja wapambanaji hao, kauli hiyo inaelekea kuwalenga
baadhi ya wanasiasa ambao walijimbapambua kuwa ni wapambanaji wa ufisadi hasa
katika Bunge la tisa lililokuwa chini ya Spika wake Samuel Sitta.
Katika Bunge hilo wabunge waliojipambanua kuwa ni wapambanaji wa ufisadi ni
Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), Anne Kilango Malecela (Same Mashariki), James
Lambeli (Kahama), Lucas Selelii (Nzega), Beatrice Shelukindo (Kilindi) na
Christopher Ole Sendeka (Simanjiro).
Mengi alitoa kauli hiyo juzi katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es
Salaam kwenye tafrija ya chakula cha mchana kilichoandaliwa na IPP kwa ajili ya
watu wenye ulemavu.
Alisema katika siku za hivi karibuni wapambanaji wa ufisadi, ikiwa ni pamoja
na vyombo vya habari, wamenyamazishwa kwa njia mbalimbali kutokana na nguvu za
mafisadi kifedha.
Alisema ingawa vitendo vya ufisadi vimeongezeka kwa nguvu na kasi kubwa,
nguvu na kasi ya wananchi kwa kushirikiana na vyombo vya habari katika vita hiyo
zimepungua ambapo hivi sasa kelele za kulaani ufisadi hazisikiki kama awali.
“Kuna watu wanaofikiri kwamba kupungua kwa kelele hizo kunaashiria kupungua
au kutokomea kwa ufisadi, kumbe si kweli bali ni kutokana na sababu mbalimbali
ikiwamo ya rushwa ya fedha za mafisadi,” alisema.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni kutochukuliwa kwa hatua kwa watu
wanaohusishwa na vitendo vya ufisadi ambao wanajulikana kwa majina lakini
wameachwa wakiendelea kula maisha ya raha na yenye jeuri.
“Ripoti nyingi za uchunguzi uliofanywa na vyombo vya habari zimefichua
ufisadi mkubwa wa aina mbalimbali ambao haukupata kukanushwa, kwa mfano Kagoda
na Meremeta, ikiwa na maana kwamba ripoti hizo ni za kweli. Ripoti hizi ni za
muda mrefu sana, lakini hadi sasa waliohusishwa na ufisadi huo hawajachukuliwa
hatua.
“Wananchi wanashangaa kuona mchota fedha za EPA anakiri uporaji huo na
anatamba amerudisha fedha, lakini hachukuliwi hatua yoyote, eti kwa sababu
hakuna ushahidi. Kama kurudisha si ushahidi, ni ushahidi wa aina gani
unatakiwa?” alihoji.
Alisema wananchi wanashangaa wanapoona wauzaji wa rada iliyonunuliwa kwa bei
ya kulangua wanarejesha nchini fedha walizoongeza katika uuzaji huo lakini
serikali ya Tanzania haijawachukulia hatua zozote za kisheria waliofanikisha
rada hiyo kununuliwa kwa bei ghali.
Mengi alisema mfumo mzima wa jamii umechafuliwa na ufisadi unaohusisha
viongozi wa serikali, wanasiasa na baadhi ya vyombo vya habari katika vitendo
vya rushwa na viongozi wa umma katika wizi na uporaji wa mali za umma.
Aliongeza kuwa kutokana na kutochukuliwa hatua za kisheria dhidi ya wale
wanaohusishwa na ufisadi na uchafuzi uliosababishwa na ufisadi katika mfumo wa
jamii, wananchi wamekata tamaa ya ushindi katika mapambano dhidi ya ufisadi.
Alionya kuwa ufisadi unavunja amani na ni mchezo hatari na wa mauti, hivyo ni
lazima vitendo vya ufisadi vichukuliwe hatua za kisheria haraka
vinapobainika.
Pamoja na hayo, alieleza kuwa mapambano dhidi ya ufisadi ni lazima yawe
endelevu na kwamba dhamira ya kutokomeza ufisadi huo bado wanayo ingawa
mapambano ya awali yalizaa matunda yasiyoridhisha.
“Mafanikio haya yawe chachu ya kuongeza nguvu katika mapambano na tusikubali
kukata tamaa kutokana na kutoridhishwa na kiwango cha hatua zilizochukuliwa.
Kukata tamaa ni kukubali kushindwa. Bado hatujashindwa.
“Tusikubali kurubuniwa na nguvu ya kifedha za mafisadi, tusikubali
kunyamazishwa. Tukikaa kimya tumewasaidia mafisadi na kuwasaliti ndugu zetu
walalahoi.
Mbio za urais
Alisema mbio za kutaka kuwania urais hasa kupitia chama tawala (CCM),
zimefikia hatua mbaya kutokana na baadhi ya wanasiasa na watendaji kusahau
kuwatumikia wananchi.
Alisema baadhi ya viongozi wa umma wenye dhamana ya kushughulikia matatizo ya
wananchi wameyapa kisogo matatizo hayo na badala yake kushughulikia mambo yao
binafsi, kiasiasa na kiuchumi.
“Badala ya kushindana katika kuwasaidia wananchi wanashindana katika
kujitajirisha na kutafuta madaraka ya kisiasa kuelekea mwaka 2015,” alisema
Mengi.
Alisema sababu hiyo na nyinginezo zinachangia maisha ya wananchi kuwa magumu
na kubainisha kuwa zipo sababu ambazo haziepukiki, lakini zipo ambazo zinaweza
kuepukika.
Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo aliwashukia watendaji wa halmashauri
wa miji na wilaya kwa ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo.
Alisema miradi mingi ya maendeleo haitekelezwi na hata kama ikitekelezwa
inakuwa ya kiwango cha chini na kwa gharama kubwa na kusababisha hasara kubwa,
jambo ambao linaashiria kuwapo kwa rushwa katika utoaji wa zabuni.
“Halmashauri za miji na za wilaya ni kitovu cha maendeo ya jamii, lakini
maendeleo katika halmashauri nyingi yamekuwa hafifu na ushahidi umeonyesha
kwamba baadhi ya viongozi wa umma katika halmashauri hizo wamekuwa wabadhirifu,
waporaji na wezi wa fedha za maendeleo,” alisema.
na Tamali Vullu
|
No comments:
Post a Comment