Shughuli za Bunge zikiendelea Bungeni
WAKATI Bunge likiendelea kuomboleza vifo vya wabunge wake wawili, Regia Mtema
(Viti Maalumu Chadema) na Jeremiah Sumari Arumeru Mashariki CCM), limepata pigo
jingine baada ya mfanyakazi wake, Nicolaus Luther Senge kufariki dunia kwa
kupigwa risasi na askari polisi katika tukio ambalo lilisababisha vifo vya watu
watatu.
Hata hivyo, kumekuwa na taarifa za kutatanisha na zenye kupingana kati ya
polisi na Bunge kuhusu jina halisi la mfanyakazi huyo na mahali ambako mwili
wake umehifadhiwa.
Habari zilizotufikia jana zimeeleza kuwa Senge (49) alifariki
dunia usiku wa kuamkia jana katika mauaji yaliyofanyika kwenye kikao cha
wanafamilia Kibaha mkoani Pwani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu amethibitisha kifo hicho lakini
akamtaja mtumishi huyo wa Bunge kuwa ni Nkolo Senge.
Kamanda Mangu alisema katika tukio hilo lililotokea nyumbani kwa Pendael
Senge ambaye ni Mratibu wa Tasaf Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, wengine
waliofariki dunia ni Andrew Nkolo (30) na askari polisi Nicodemus Senge ambaye
ndiye anayetuhumiwa kuwaua wenzake.
Alisema siku ya tukio, watu hao walifika nyumbani kwa Pendael ambaye ni baba
yao mdogo kwa ajili ya kupatanishwa juu ya ugomvi wa urithi wa ekari mbili za
ardhi zilizoko kijijini kwao Singida.
“Ugomvi huo ulianzia Singida ambako walishtakiana lakini hakimu akawataka
waumalize kiukoo. Ndipo Pendaheli ambaye ni baba yao mdogo akaamua kuwaita
nyumbani kwake ili wazungumzie suala hilo,” alisema Kamanda Mangu na
kuendelea:
“Wakiwa kweye kikao hicho kabla ya kufikia mwafaka, Nicodemus ambaye ni
askari polisi wa Kituo cha Usalama Magomeni, Dar es Salaam alichomoa bastola
yake na kuwamiminia risasi ndugu zake hao kisha kujimaliza mwenyewe.”
Kwa mujibu wa Kamanda Mangu, miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika
Hospitali ya Tumbi, Kibaha na hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio
hilo.
Kauli ya Ofisi ya Bunge
Naibu Spika wa Bunge,
Job Ndugai amethibitisha kutokea kwa kifo cha mfanyakazi huyo wa Bunge na
kueleza kuwa hadi jana mchana, lakini akasema maiti yake ilikuwa imehifadhiwa
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Ndugai alisema Ofisi ya Bunge imesikitishwa na kifo hicho kilichotokea usiku
wa kuamkia jana, siku chache baada ya taasisi hiyo ya kutunga sheria kupoteza
wabunge wawili.
“Kwa sasa nipo Arusha lakini taarifa za kifo cha Senge nilizipata jana. Bado
sina taarifa zaidi kuhusu kifo hicho kwa sababu kimetokea kwa njia ambayo lazima
ihusishe uchunguzi wa kipolisi,” alisema Ndugai.
Hilo ni pigo jingine kwa taasisi hiyo katika kipindi cha juma moja baada ya
Mtema kufariki dunia Januari 14, kwa ajali ya gari iliyotokea Ruvu, Kibaha na
Sumari alifariki dunia Januari 17, mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mrefu
saratani ya ubongo.
Kauli ya familia
Baba mdogo wa marehemu hao Pendael Senge
naye alithibitisha mauaji hayo na kueleza kuwa yalitokana na ugomvi wa
shamba.
Pendael alisema askari huyo aliwaua ndugu yake Nicolaus Senge ambaye alikuwa
mtumishi wa Ofisi ya Bunge, pamoja na binamu yake Andrew Nkolo (mtoto wa
shangazi yake).
Akisimulia tukio hilo Pendael alisema kabla ya mauaji hayo, ndugu hao
walifika nyumbani kwake Kongowe Kibaha kwa ajili ya kikao cha usuluhishi
kuhusiana na ugomvi huo wa shamba. Hata hivyo, alisema usuluhishi huo
ulishindikana na badala yake ukazuka ugomvi baina ya ndugu hao uliwafanya
wapigane ngumi kabla ya wanandugu kuwaamulia.
Alisema muda mfupi baada ya ndugu kuwaamulia, askari huyo aliwapiga risasi
ndugu zake kisha naye kujimaliza.
Alisema chanzo cha ugomvi huo ni shamba la
ekari mbili lililoko katika Kijiji cha Ilunda Wilaya ya Iramba, Singida...
“Shamba hilo ni la mpwa wangu Andrew ambalo alirithishwa na mama yake
aliyefariki dunia takriban miaka 15 iliyopita,” alisema Pendael na kuongeza:
“Lakini kwa kuwa Andrew anafanya shughuli zake za Steshenari Dar es Salaam,
basi binamu yake Nicodemus Senge akajenga nyumba katika kiwanja hicho.”
Alisema baada ya Nicodemus kujenga katika kiwanja cha Andrew, walishtakiana
katika baraza la ardhi kijijini hapo ambalo liliwaagiza wazungumze wenyewe
kwanza ili kuona kama wanaweza kufikia mwafaka.
“Kwa kuwa wote wako hapa Dar es Salaam ndipo jana wakaamua kuja kwangu kwa
ajili ya kufanya kikao cha usuluhishi. Wao walifika saa 10 na baada ya ndugu
wengine kufika saa 12 jioni ndipo tukaanza mazungumzo:
“Niliwasihi kuwa
nikiwa baba yao mdogo ningefurahi kuona jambo hilo linamalizika kindugu,”
alisema Pendaeli
Hata hivyo, alisema wakati wa mazungumzo hayo Nicodemus
akamshutumu ndugu yake Nicodemus (wa Bunge) kuwa ndiye anayempa msaada binamu
yake wa kifedha na kiushauri.
“Alikuja juu (polisi) na kuongea kwa hasira sana. Mimi baada ya kuona kuwa
hakuna uelewano tena nilishauri kuwa ni vyema tuliachie baraza la ardhi liamue,”
alisema Pendaeli na kuongeza:
“Nico wa Bunge na Andrew walikuwa upande mmoja na huyu askari na baadhi ya
ndugu wengine walikuwa pia upande mmoja, hivyo wakaanza kupigana ngumi lakini
watu wakawasihi wakaacha.”
“Lakini kabla ya kuondoka huyu askari akaomba maji, walipomletea akakataa
glasi akanywea kwenye kidumu kile cha lita tano. Alipokunywa mara moja tu
akapiga chini lile dumu kisha akakimbia hadi kwenye gari alimokuwa Nico wa Bunge
akampiga risasi moja ya usoni kisha akamfuata Andrew akampiga risasi ya begani,
wakati akikimbia akampiga risasi nyingine kiunoni, akaanguka na kufariki dunia,”
alisema Pendaeli.
Baada ya matukio alisema watu wote walikimbia akiwamo askari huyo ambaye hata
hivyo, alisema alikimbia kama mita 50 kutoka nyumbani hapo kisha naye akajipiga
risasi kifuani na kufariki dunia papohapo.
“Nilikwenda kutoa taarifa kituo cha polisi na askari walipofika na kumpekua
mfukoni mwake (muuaji) wakakuta kikaratasi kilichosema: mtu yeyote asisumbuliwe
kwa mauaji haya,” alisema Pendaeli.
Habari hii imeandaliwa na Sanjito Msafiri na Julieth Ngarabali,
Kibaha, Aidan Mhando, James Magai
No comments:
Post a Comment